Sunday, February 28, 2010

Moyo wangu tulia

Dunia ina vikwazo, we' moyo wangu tulia,
Ina mengi machukizo, yanoleta kuumia,
Ina mengi matatizo, mlo kujitafutia,
We' moyo wangu tulia, mtumainie Mola.

Maisha ni mapambano, moyo hilo walijua,
Hivyo ni mtafutano, wapaswa kulitambua,
Huwepo mivurugano, ni vema kuigundua,
We' moyo wangu tulia, mtumainie Mola.

Maisha ni kama vita, yapasa uwe na nia,
Moyo wala 'sije tweta, tamaa kujikatia,
Moyo zidi furukuta, malengo kuyafikia,
We' moyo wangu tulia, mtumainie Mola.

Moyo kuna wanadamu, mabaya hukuombea,
Chuki kwako iwe sumu, baya sije watendea,
Ila sala ni muhimu, kwa yote yanotokea,
We' moyo wangu tulia, mtumainie Mola.

Moyo uwe nayo nguvu, mwiko kukata tamaa,
Uwe na uvumilivu, hata ushinde na njaa,
Pia uwe msikivu, na kumaizi hadaa,
We' moyo wangu tulia, mtumainie Mola.

Mola wetu husikia, zidi mtumainia,
Moyo uzidi tulia, maisha wapigania,
Moyo utafurahia, lengo litapotimia,
We' moyo wangu tulia, mtumainie Mola.

Monday, February 15, 2010

Pendo langu kwako wewe

Uketi chini mpenzi, ya moyoni nikwambie,
Daima nitakuenzi, uhai uniishie,
Hutoipata simanzi, nataka ufurahie,
Pendo langu kwako wewe, halipimwi kwa mizani.

Halipimwi kwa mizani, uzitowe wazidia,
Pendo linayo thamani, hakuna cha kufikia,
Hata kwa mizani gani, huwezi kulipimia,
Pendo langu kwako wewe, hutolikuta dukani.

Hutolikuta dukani, ati labda lauzwa,
Pendo li ndani moyoni, kwalo pendo nimemezwa,
Kwani halina kifani, kwa kitu likaigizwa,
Pendo langu kwako wewe, kwa mwingine hulikuti.

Kwa mwingine hulikuti, pendo akakupatia,
Nina pendo lenye dhati, ya moyo uloridhia,
Pendo liso na wakati, daima kufurahia,
Pendo langu kwako wewe, ling'aalo kama nyota.

Ling'aalo kama nyota, maishani kuwa nuru,
Pendo raha kulipata, kufaidi kwa uhuru,
Pendo chozi kunifuta, kwa nini nisishukuru,
Pendo langu kwako wewe, liishi zote dawamu.

Liishi zote dawamu, linipe raha ya moyo,
Pendo hili na lidumu, kwa furaha linipayo,
Pendo hili mbona tamu, kwa tamu niipatayo,
Pendo langu kwako wewe, kamwe halina mipaka.

Kamwe halina mipaka, pendo mali yako yote,
Kukupenda sitochoka, pendo ulimi na mate,
Juwa kwangu umefika, wala us'ende kokote,
Pendo langu kwako wewe, waache waone wivu.

Waache waone wivu, kwa pendo ninalokupa,
Sisi tule zetu mbivu, pendo lizidi nenepa,
Kwako niwe msikivu, sitowaza kukutupa,
Pendo langu kwako wewe, wacha lizidi shamiri.

Wacha lizidi shamiri, wacha pendo na ling'ae,
Kukupata ni fahari, wengine uwakatae,
Pendo kwako li mahiri, unifae nikufae,
Pendo langu kwako wewe, mbona linanipa raha.

Mbona linanipa raha, ni bahati sana mie,
Pendo lajaa furaha, wacha nilifurahie,
Kwa pendo nipate siha, nishibe na nichanue,
Pendo langu kwako wewe, ni mwisho wa mambo yote.

Thursday, February 11, 2010

Wasiwasi na Neno zuri

Humkosesha mtu raha, wasiwasi unakera,
Huleta nyingi karaha, hata kw'ongeza hasira,
Huwezi fanya madaha, wafungwa nayo nira,
Wasiwasi.

Wasiwasi ni utumwa, wa kuusumbua moyo,
Huleta kama kuumwa, yale yakusumbuayo,
Moyo wahisi kuchomwa, kwa yale yautesayo,
Wasiwasi.

Wasiwasi unaghasi, unakosesha amani,
Kutengwa unakuhisi, kama mwokozi humwoni,
Huharibu mitikasi, na kukurudisha chini,
Wasiwasi.

Neno zuri ndiyo dawa, wasiwasi huondoa,
Furaha moyoni huwa, hofu yako kuitoa,
Faraja wewe kupewa, na raha isiyo poa,
Neno zuri.

Ni hedaya neno zuri, muhimu kwayo dunia,
Upatapo ni fahari, moyo wako hutulia,
Haliyo iwapo shwari, mamboyo wajifanyia,
Neno zuri.

Neno zuri ni muhimu, kila mtu ahitaji,
Kulipata kuna hamu, neno zuri hufariji,
Neno zuri kweli tamu, hulifaidi mlaji,
Neno zuri.

Sunday, February 7, 2010

Langu neno

Niliseme kwa nguvu ulisikie,
Ama tu wengine niwaachie,
Wakwambie,
Asokuwepo nisimjue,
Wataka umsaidie?

Maisha, maisha yaishie?
Kipi hasa ukitumikie?
Wauliza tu ama wan'uliza mie?
Wataka nikujibie.

Langu wacha likuingie,
Ama wataka usiumie?
Lipo lino tuhadithie.

Kwa nini uwaachie,
Wao wao wakutumie,
Ila wao nd'o wayafaidie,
We' na yako njaa uwaangalie,
Ili kesho wakusifie!

Umung'unyungu si kiti ukalie,
Ukikaa 'sikae utumbukie,
Ukitumbukia awepo akuinue,
Akuinue na bakshishi yake mpatie.

Hiki chake kingine cha mwenzangu mie!

Alotoka kapa asiambulie,
Aje alo chano nimsaidie.