Monday, January 25, 2010

Vijinopembe

Mmekosa ya kufanya, kutwa kucha chakuchaku,
Yasowahusu pakanya, umbea ubwakubwaku,
Mnajipa umatonya, mnaishi kwa udaku,
Nini ndugu mwakifanya, hamwishi kujiashua?

Mwayasema ya wenzenu, yenu mwayaficha ndani,
Mwajipa usukununu, roho zenu ufitini,
Mwatwanga maji kwa kinu, mso na haya usoni,
Kama kusema semeni, alopata keshapata.

Roho zenu ni nyeusi, hazifuliki kwa jiki,
Watumwa wa ibilisi, mlojaa unafiki,
Muombeao mikosi, mwasahau zenu dhiki,
Hata ‘singepata mimi, kamwe ‘singekuwa yenu.

Machoni mna masizi, yamewajaza upofu,
Japo kuona ham’wezi, upeo wenu hafifu,
Chakuchaku kama inzi, wenye kupenda uchafu,
Mwajiona mu sahihi, wenye dhambi wengine.

‘Sojali msimikacho, chema mwatuza upupu,
Msojua msemacho, wenye domo lapulapu,
Kile mhangaik’acho, mbona mwalamba patupu,
Ziwaume sana roho, hapa maji marefu.

Maneno maneno yani, yamo hata kwenye khanga,
Mso soni anzuruni, mibwede kama kipanga,
Mejaa uhayawani, mnowacheka wakunga,
Na uzazi ungalipo, msiokuwa na wema.

Wengine watu wazima, ‘lozaliwa mkisema,
Kutwa nzima hemahema, hamjui kuchutama,
Wenye mioyo ya homa, msioujua wema,
Mwadhani mna zaidi, kumbe hamnalo lolote.

Hamwishi uanzuruni, viumbe mso timamu,
Mso mema mawazoni, kujitwika uhakimu,
Hajanisusa Manani, kugeuka mwendazimu,
Sitowapa kifo changu, daima mkingojea.

Msione ukadhani, mawazo’nu mufilisi,
Kunyatia tamaani, neema iso halisi,
Kono liasi begani, alishindwa nduli fisi,
Tabasamu kwangu jadi, lisiwatie ujinga,

Najichekea usoni, tafakuri akilini,
Nyendo’nu zi kitabuni, uropo uhayawani,
Siwapendi mawazoni, ‘mniwezi abadani,
Maneno hayaniui, hakika mmechelewa.

5 comments:

 1. Shairi zuri sana, lakini yaani Mzee Matonya ameshaleta msamiati :-) UMATONYA.

  ReplyDelete
 2. DIWANI, DIWANI, DIWANI AFDHILI,
  HEKIMA,BUSARA NIMEKIRI,
  SUAMBAE WAO UTAJIRI,
  MAISHANI,HEKIMA IMEJIRI,
  KI WAPI KITABU CHA MASHAIRI,
  HAMU MOYONI IMENAWIRI  KAKA FADHY.......SINA JINGINE HEBU WATEMBELEEE WALE e&d limite halafu waonyeshe haya mambo, au pale SOMA CAFE mgahawa wa vitabu jamani unatukosesha uhondo kaka DIWANI ya Fadhy Mtanga, mwananchi wewe ukulikoni

  ReplyDelete
 3. Hili kali MKUU!

  Na kimpangilio wamaneno nimekunwa na:

  ``Mmekosa ya kufanya, kutwa kucha chakuchaku,

  Yasowahusu pakanya, umbea ubwakubwaku,´´

  DUH!

  ReplyDelete