Tuesday, January 19, 2010

Pole sana dada Chemi

Nimepata mshituko, habari kuisikia,
Ni pigo kwa moyo wako, na kwa familia pia,
Mola ni faraja kwako, katika hii dunia,
Pole sana dada Chemi, kwa kufiwa na mumeo.

Dunia siyo salama, hapa sisi tunapita,
Leo kuwa na uzima, kesho Mungu atuita,
Mola ni mwema daima, faraja kwake kupata,
Pole sana dada Chemi, kwa kufiwa na mumeo.

Hilo pigo kubwa sana, ila yupo mfariji,
Mola akulinde sana, aujua uhitaji,
Kusali ukikazana, huzuni kwako haiji,
Pole sana dada Chemi, kwa kufiwa na mumeo.

Mumeo yupo salama, mahali pema peponi,
Kwani Muumba ni mwema, ajuaye ni kwa nini,
Imara utasimama, kamwe hutokwenda chini,
Pole sana dada Chemi, kwa kufiwa na mumeo.

Nasi tu pamoja nawe, katika haya majonzi,
Mola katikati awe, kufuta yako machozi,
Imani yako ikuwe, kukutupa hatuwezi,
Pole sana dada Chemi, kwa kufiwa na mumeo.

Nakupa pole nyingi sana dada Chemi kwa kuondokewa na mumeo. Sote tumeguswa sana na msiba huu. Tunakupenda sana. Mungu akufariji na kukutia nguvu katika kipindi hiki kigumu sana kwako. Pia aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.

2 comments:

  1. Ni kweli ni pigo kubwa kuondokewa na mumeo mpendwa. Tupo pamoja kwa njia ya sala marehemu astarehe kwa amani peponi Amina.

    ReplyDelete
  2. Naungana na watu wote kutoa pole

    ReplyDelete