Tuesday, January 5, 2010

Heri Yasinta Ngonyani

Leo unaikumbuka, sikuyo ya kuzaliwa,
Ni siku yenye Baraka, furaha tele kujawa,
Furaha iso pimika, shukurani kuzitowa,
Heri Yasinta Ngonyani, sikuyo ya kuzaliwa.

Mwanaharakati wetu, utujuzaye maisha,
Wewe ni darasa kwetu, maarifa yaso kwisha,
Wafunza juu ya utu, mengi watuelimisha,
Heri Yasinta Ngonyani, sikuyo ya kuzaliwa.

Yasinta usiyechoka, asubuhi na jioni,
Nyumbani kuwajibika, halafu pia kazini,
Kisha huachi andika, kutujuza kulikoni,
Heri Yasinta Ngonyani, sikuyo ya kuzaliwa.

We’ ni mwanaharakati, daima usiyechoka,
Wautumia wakati, pasipo yoyote shaka,
Maisha kuwa na chati, daraja la uhakika,
Heri Yasinta Ngonyani, sikuyo ya kuzaliwa.

Baraka nakuombea, ubarikiwe daima,
Mola kukuongezea, uwe mwenye afya njema,
Shida kukuepushia, daima uwe salama,
Heri Yasinta Ngonyani, sikuyo ya kuzaliwa.

Pia yako familia, ibarikiwe amani,
Mola ‘tawasimamia, furaha ijae ndani,
Na izidi kuchanua, kama maua shambani,
Heri Yasinta Ngonyani, sikuyo ya kuzaliwa.

Leo naishia hapa, dada Yasinta Ngonyani,
Mola wetu atakupa, siku nyingi duniani,
Nasi hatutokutupa, asilani abadani
Heri Yasinta Ngonyani, sikuyo ya kuzaliwa.

2 comments:

  1. Mtani, Ahsante kwa beti hizi tamu kwa kunitakia mema. Ubarikiwe ana. Ahsante sana kwa zawadi hii nzuri.

    ReplyDelete
  2. Na kwa baraka twasindikisha maneneo mazuri ya Fadhy
    Heri Yasinta Ngoyani, sikuyo ya kuzaliwa

    ReplyDelete