Monday, January 18, 2010

Heri kwa Mama Yetu

Shukrani nazitowa, kwa muumba wa dunia,
Na furaha nimejawa, siku kuifurahia,
Siku mama kuzaliwa, afya tele kumjalia,
Twakushukuru Muumba, na kumpongeza mama.

Mungu umetujalia, mama mwema sana kwetu,
Ambaye twajivunia, katika maisha yetu,
Kwa wema ametulea, na kutufudisha utu,
Hivyo tunayo sababu, ya kufurahia sana.

Mama twakupenda sana, wewe ni mlezi bora,
Kwa hilo tunajivuna, wafanya sisi imara,
Hatuchoki kukazana, kwa juhudi na busara,
Kwani umetufundisha, tumtegemee Mungu.

Mungu akupe furaha, nayo amani daima,
Maisha yawe ya raha, pia yenye afya njema,
Ing'ae nyota ya jaha, uchume yaliyo mema,
Kwani sisi twakujali, naye Mungu akulinda.

2 comments:

 1. nanukuu "Mama twakupenda sana, wewe ni mlezi bora,
  Kwa hilo tunajivuna, wafanya sisi imara,
  Hatuchoki kukazana, kwa juhudi na busara,
  Kwani umetufundisha, tumtegemee Mungu." ni kweli kabisa mama wewe ni mlezi bora kwani mafanikio tunayaona. Hongera sana mama. Oh! kumbe tumezaliwa mwezi mmoja.!!

  ReplyDelete
 2. Nakutakia kila la kheri Mama Fadhy katika siku yako ya kuzaliwa!

  ReplyDelete