Friday, January 29, 2010

Utamu wa Ushairi-I

Mimi nilisema:
Mbuzi wamtishale, Ati mbele aendale,
Ni hakile kukatale, Ubabe uizidile,
Mwachile mbuzi agomale, We ani wamtakale,
Kumbe umnyanyasile, Hebu aibu uionale,
Chambilecho watu wa kale.

Abdallah Mpogole akajibu:
Mbuzi wa kukuna yangu nazile!
Nampitishia pale yalo makali viunga avikatile!
Ubwabwa mkavu sintoweza labda wabara wale!
Maji mengi kwa nazile ni vipi siyachujale!
Mbuzi ataka dezole achagule wapi ale!
Mie basi siwatakile hawakuni uzuri kwa mtogole!
Tui kidogo tu basi mpingile!

Mimi nikasema:
Mpogole weye mtu huishi vituko!
Yakupatani mbuzi wako!
Ukunile nazi chakula chako!
Wapenda wali ka' ndo zindiko!
Wauhangaikia mchele huko na huko!
Nami ntaja niwe mgeni wako!
Unijazie ubwabwa nazizo choroko!
Nijinome mulo kwazo pishi zako!

Abdallah Mpogole akasema:
Mbuzi huyu mbuzi sasa hawezi kazi!
Apenda tu vitamu hataki kula mzizi!
Mbuzi gani mbishi asothamini uzazi!
Sintompa tena nazi na asahau malezi!
Mbuzi huyu tapeli tamfunga kwa wizi!
Apewapo tu mzizi haishi ulizi!
Adai aonewa hali ndo sera ya kazi!

Mimi nikamjibu:
Juu ya nini mbuzi sasa wamtisha!
Una hila weye ugomvi wauanzisha!
Mbuzi, mbuzi gani kazi kachemsha?
Najua ni fitna we waisababisha!
Kama akosa washindwaje mrekebisha!
Wala sikuamini maneno wayazusha!

Abdallah Mpogole akasema:
Sinipande kichwani Mtanga samahani!
Mbuzi anipa tabu majani kuyasaka juani!
Napambana kondeni na miba hayinishi miguuni!
Mbuzi gani kusukumwa na mijeledi mgongoni!
Hakumbuki thamani nliyomtoa maskani!
Taja niua mie kwa mawazo kichwani!
Mtanga ndugu yangu niko sasa ajalini!
Japo nkwachie weye bingwa wa mbuzi mjini!
Baraka zote takupa ila usije haini! ...
Sangwa kanijulisha we mchungaji wa zamani!
Tangu kwa baba tende na mbao wa povu mdomoni!
kideo cha pilau na maandazi kwa nelkoni!
Mtanga ntakubaini siku moja njiani!
Ntafurahi kukuona mfalme masikini!

Mimi nikamjibu:
Mi si masikini bali mfalme tajiri!
Nasifika toka kwa Mbao nna roho nzuri!
Sasa nipo mjini hakika nanawiri!
Na mavazi yangu yashonwa kwa hariri!
Natema maujumbe kama Zaburi!
Mpogole nakujuza uje na lako gari!
Twen'zetu fukwe kwenye upepo wa bahari!
Nikusimulie maisha kwa ushairi!
Najua u mjuzi mwenye kufikiri!
Mpogole we kwangu ni rafiki mzuri!
Mimi kukufahamu naona fahari.

Abdallah Mpogole akaandika:
Nawaza sana siku hiyo!
Taonana na mmahiri wa kwayo!
Si waridi wa mambo hayo!
Bali u makini kwa yapitayo!
Sijakwona kwa surayo!
Japo nafurahi wandikayo!
Wankumbusha malenga wa enzi hiyo!
Waliokosa uchoyo!
Sitaki upoteze yote yaliyo!
Taniumiza sana moyo!
Yanakiri tuandikayo!
Tuweze wapa wasonayo!
Nyama ngumu tuwapayo!
Wenye meno na vibogoyo!
Tuungane kwa mikono tunene kimoyomoyo!
Mtanga ndugu yangu tu matajiri kwa haya tuyatoayo!
Jipange tuifikishe hii ngao ya watu na maishayo!

Nami nikamjuza:
Mpogole wazolo lakubalika!
Haya tusemayo si budi kuhifadhika!
Iwepo kumbukumbu hata wakituzika!
Wote watusomao waweze kuburudika!
Tuyatunze haya pasi na shaka!
Ujuzi mkubwa hapa watumika!
Tusiiache fani hata ipite miaka.

Haya ni majibizano niliyoyafanya na rafiki yangu Abdallah Mpogole katika Facebook. Nimependa kuwashirikisha utamu huu wa ushairi wa Kiswahili. Hakika huko majibizano yamepamba moto. Nitawaletea yote wadau wangu kadiri ya tujibizanavyo.
Tunawashukuru sana Albert Kissima, Da Subi na marafiki wengine wa Facebook kwa kutuunga mkono. Hakika ushairi wa Kiswahili uhai na wenye utamu uso kifani.

Monday, January 25, 2010

Vijinopembe

Mmekosa ya kufanya, kutwa kucha chakuchaku,
Yasowahusu pakanya, umbea ubwakubwaku,
Mnajipa umatonya, mnaishi kwa udaku,
Nini ndugu mwakifanya, hamwishi kujiashua?

Mwayasema ya wenzenu, yenu mwayaficha ndani,
Mwajipa usukununu, roho zenu ufitini,
Mwatwanga maji kwa kinu, mso na haya usoni,
Kama kusema semeni, alopata keshapata.

Roho zenu ni nyeusi, hazifuliki kwa jiki,
Watumwa wa ibilisi, mlojaa unafiki,
Muombeao mikosi, mwasahau zenu dhiki,
Hata ‘singepata mimi, kamwe ‘singekuwa yenu.

Machoni mna masizi, yamewajaza upofu,
Japo kuona ham’wezi, upeo wenu hafifu,
Chakuchaku kama inzi, wenye kupenda uchafu,
Mwajiona mu sahihi, wenye dhambi wengine.

‘Sojali msimikacho, chema mwatuza upupu,
Msojua msemacho, wenye domo lapulapu,
Kile mhangaik’acho, mbona mwalamba patupu,
Ziwaume sana roho, hapa maji marefu.

Maneno maneno yani, yamo hata kwenye khanga,
Mso soni anzuruni, mibwede kama kipanga,
Mejaa uhayawani, mnowacheka wakunga,
Na uzazi ungalipo, msiokuwa na wema.

Wengine watu wazima, ‘lozaliwa mkisema,
Kutwa nzima hemahema, hamjui kuchutama,
Wenye mioyo ya homa, msioujua wema,
Mwadhani mna zaidi, kumbe hamnalo lolote.

Hamwishi uanzuruni, viumbe mso timamu,
Mso mema mawazoni, kujitwika uhakimu,
Hajanisusa Manani, kugeuka mwendazimu,
Sitowapa kifo changu, daima mkingojea.

Msione ukadhani, mawazo’nu mufilisi,
Kunyatia tamaani, neema iso halisi,
Kono liasi begani, alishindwa nduli fisi,
Tabasamu kwangu jadi, lisiwatie ujinga,

Najichekea usoni, tafakuri akilini,
Nyendo’nu zi kitabuni, uropo uhayawani,
Siwapendi mawazoni, ‘mniwezi abadani,
Maneno hayaniui, hakika mmechelewa.

Tuesday, January 19, 2010

Pole sana dada Chemi

Nimepata mshituko, habari kuisikia,
Ni pigo kwa moyo wako, na kwa familia pia,
Mola ni faraja kwako, katika hii dunia,
Pole sana dada Chemi, kwa kufiwa na mumeo.

Dunia siyo salama, hapa sisi tunapita,
Leo kuwa na uzima, kesho Mungu atuita,
Mola ni mwema daima, faraja kwake kupata,
Pole sana dada Chemi, kwa kufiwa na mumeo.

Hilo pigo kubwa sana, ila yupo mfariji,
Mola akulinde sana, aujua uhitaji,
Kusali ukikazana, huzuni kwako haiji,
Pole sana dada Chemi, kwa kufiwa na mumeo.

Mumeo yupo salama, mahali pema peponi,
Kwani Muumba ni mwema, ajuaye ni kwa nini,
Imara utasimama, kamwe hutokwenda chini,
Pole sana dada Chemi, kwa kufiwa na mumeo.

Nasi tu pamoja nawe, katika haya majonzi,
Mola katikati awe, kufuta yako machozi,
Imani yako ikuwe, kukutupa hatuwezi,
Pole sana dada Chemi, kwa kufiwa na mumeo.

Nakupa pole nyingi sana dada Chemi kwa kuondokewa na mumeo. Sote tumeguswa sana na msiba huu. Tunakupenda sana. Mungu akufariji na kukutia nguvu katika kipindi hiki kigumu sana kwako. Pia aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.

Monday, January 18, 2010

Heri kwa Mama Yetu

Shukrani nazitowa, kwa muumba wa dunia,
Na furaha nimejawa, siku kuifurahia,
Siku mama kuzaliwa, afya tele kumjalia,
Twakushukuru Muumba, na kumpongeza mama.

Mungu umetujalia, mama mwema sana kwetu,
Ambaye twajivunia, katika maisha yetu,
Kwa wema ametulea, na kutufudisha utu,
Hivyo tunayo sababu, ya kufurahia sana.

Mama twakupenda sana, wewe ni mlezi bora,
Kwa hilo tunajivuna, wafanya sisi imara,
Hatuchoki kukazana, kwa juhudi na busara,
Kwani umetufundisha, tumtegemee Mungu.

Mungu akupe furaha, nayo amani daima,
Maisha yawe ya raha, pia yenye afya njema,
Ing'ae nyota ya jaha, uchume yaliyo mema,
Kwani sisi twakujali, naye Mungu akulinda.

Saturday, January 16, 2010

Simon Kitururu

Nipeni mie kalamu, karatasi nayo pia,
Nitume zangu salamu, rafiki kumfikia,
Ni siku yake muhimu, anaisherehekea,
Kheri kwayo siku yako, Simon Kitururu.

Miaka iliyopita, wewe ungali tumboni,
Mamayo akakuleta, ndani humu duniani,
Mama kijana kapata, ni shangwe toka moyoni,
Kheri kwayo siku yako, Simon Kitururu.

Dunia hii dunia, ndaniye na wewe umo,
Umri kuufikia, hadi utu wa makamo,
Maisha wapigania, kwawo wako msimamo,
Kheri kwayo siku yako, Simon Kitururu.

Kwako naziomba duwa, ujaliwe afya njema,
Kokote unakokuwa, uzidi kuwa salama,
Siwepo kukusumbua, maradhi wala unyama,
Kheri kwayo siku yako, Simon Kitururu.

Ujaliwe marafiki, wenye upendo wa dhati,
Ili katika mikiki, uwashike japo shati,
Usipate wanafiki, wapendao kwa nyakati,
Kheri kwayo siku yako, Simon Kitururu.

Ujaliwe familia, yenye wingi wa furaha,
Mola kuisimamia, ithibati njema siha,
Nawe kuipigania, kwayo shida nayo raha,
Kheri kwayo siku yako, Simon Kitururu.

Furahi bila kuchoka, hii ndiyo siku yako,
Nduguzo kuwakumbuka, ikawe hulka yako,
Upendwe ukapendeka, kokote kule wendako,
Kheri kwayo siku yako, Simon Kitururu.

Kalamu naweka chini, hongera rafiki yangu,
Duwa ingali moyoni, nikuombee kwa Mungu,
Daima uwe rahani, wepushwe nayo machungu,
Kheri kwayo siku yako, Simon Kitururu.

Sunday, January 10, 2010

Hamna hamna

Wasema hakuna kitu, mbona siye twakiona,
Wasema hakuna kutu, ilhali yaonekana,
Wadhani si malikitu, kwavo kwa kudanganyana,
Humo hamna hamna, basi ndimo mliwamo.

Wasema lisilowepo, lililopo hulisemi,
Mbona hata usemapo, wang'ata sana ulimi,
Kwanini itokeapo, manenoyo huyapimi,
Humo hamna hamna, basi ndimo mliwamo.

Husemwa ada ya mja, ni kusema sema mno,
Hata pasipo na hoja, pia pasipo maono,
Hatochoka kubwabwaja, hata kutowa agano,
Humo hamna hamna, basi ndimo mliwamo.

Waficha yalo ya kweli, kwani wamwachia nani?
Ufikiri mara mbili, changanua mawazoni,
Dunia kuibadili, si maneno mdomoni,
Humo hamna hamna, basi ndimo mliwamo.

Tuna macho twayaona, yote yanayotendeka,
Hata ungesema sana,vigumu kuaminika,
Hatupendi danganyana, hayo tumeshayachoka,
Humo hamna hamna, basi ndimo mliwamo.

Eti hakuna uchafu, ilhali tuna kinyaa,
Si vema ukajisifu, watu wanakushangaa,
Haina umaarufu, ikiwa itachakaa,
Humo hamna hamna, basi ndimo mliwamo.

Humo ndimo mliwamo, twajua toka kitambo,
Hatukupenda uwemo, tulijua yako mambo,
Uwapo mwenye makamo, lifumbue hili fumbo,
Humo hamna hamna, basi ndimo mliwamo.

Sisemi tena zaidi, nimependa kumaliza,
Sivunji yangu ahadi, nawe utanieleza,
Tumechoka makusudi, hatutokuendekeza,
Humo hamna hamna, basi ndimo mliwamo.

Tuesday, January 5, 2010

Heri Yasinta Ngonyani

Leo unaikumbuka, sikuyo ya kuzaliwa,
Ni siku yenye Baraka, furaha tele kujawa,
Furaha iso pimika, shukurani kuzitowa,
Heri Yasinta Ngonyani, sikuyo ya kuzaliwa.

Mwanaharakati wetu, utujuzaye maisha,
Wewe ni darasa kwetu, maarifa yaso kwisha,
Wafunza juu ya utu, mengi watuelimisha,
Heri Yasinta Ngonyani, sikuyo ya kuzaliwa.

Yasinta usiyechoka, asubuhi na jioni,
Nyumbani kuwajibika, halafu pia kazini,
Kisha huachi andika, kutujuza kulikoni,
Heri Yasinta Ngonyani, sikuyo ya kuzaliwa.

We’ ni mwanaharakati, daima usiyechoka,
Wautumia wakati, pasipo yoyote shaka,
Maisha kuwa na chati, daraja la uhakika,
Heri Yasinta Ngonyani, sikuyo ya kuzaliwa.

Baraka nakuombea, ubarikiwe daima,
Mola kukuongezea, uwe mwenye afya njema,
Shida kukuepushia, daima uwe salama,
Heri Yasinta Ngonyani, sikuyo ya kuzaliwa.

Pia yako familia, ibarikiwe amani,
Mola ‘tawasimamia, furaha ijae ndani,
Na izidi kuchanua, kama maua shambani,
Heri Yasinta Ngonyani, sikuyo ya kuzaliwa.

Leo naishia hapa, dada Yasinta Ngonyani,
Mola wetu atakupa, siku nyingi duniani,
Nasi hatutokutupa, asilani abadani
Heri Yasinta Ngonyani, sikuyo ya kuzaliwa.

Saturday, January 2, 2010

Mwaka Mpya

Mwaka mpya umefika,
Mungu tunamshukuru,
Maana yeye ndiye kapenda,
Mwaka huu kuuona,
Tunasema ahsante.

Wengi walipenda,
Lakini hawakuweza,
Kuiona nuru mpya,
Yake mwaka mchanga,
Hawakuweza kabisa.

Si kwamba tu wema,
Hatuna mema hata kidogo,
Ila ni mapenzi yake,
Muumba wa mbingu na dunia,
Hakika ni mapenzi yake.

Tuzidi mwomba yeye,
Atujaalie zaidi na zaidi,
Ili tuweze kuiona,
Miaka mipya mingi mingine,
Maana yeye ndiye awezaye.

Heri kwenu nyote!