Wednesday, December 30, 2009

Wakati mwaka waisha

Mwaka huo wayoyoma, tuwache uende zake,
Wacha uende salama, ulijaa mambo yake,
Tuombacho ni uzima, tupewe baraka zake,
Wakati mwaka waisha, penzi lako haliishi.

Penzi lako haliishi, kama mwaka uishavyo,
Niseme halinichoshi, kama mwaka uchoshavyo,
Wala halikinaishi, vyovyote vile iwavyo,
Wakati mwaka waisha, penzi lako haliishi.

Kwako nimesharidhika, kwingine nif'ate nini?
Nanena kwa uhakika, yanikaayo moyoni,
Sifikiri nitachoka, siku zote maishani,
Wakati mwaka waisha, penzi lako haliishi.

U nuru waniangaza, maisha kunipa raha,
U ua wanipendeza, moyo kujawa furaha,
Sauti yaniliwaza, daima kutoa karaha,
Wakati mwaka waisha, penzi lako haliishi.

U chakula nishibacho, kwingine siwezi kwenda,
U mboni ya langu jicho, daima nitakulinda,
Amini nikisemacho, sidiriki kukutenda,
Wakati mwaka waisha, penzi lako haliishi.

Shida zote za maisha, wewe kwangu ni faraja,
Hofu yangu waishusha, kila tuwapo pamoja,
Daima huniwezesha, kuyavuka madaraja,
Wakati mwaka waisha, penzi lako haliishi.

2 comments:

 1. Hili shairi linaonekana ni la kufungia mwaka. Mtani huyu wifi inabidi usiwache. Ngoja ninukuu,

  "U chakula nishibacho, kwingine siwezi kwenda,
  U mboni ya langu jicho, daima nitakulinda,
  Amini nikisemacho, sidiriki kukutenda,
  Wakati mwaka waisha, penzi lako haliishi." Hapa naona mtani umedhamilia kweli. Nawatakieni kila la kheri.

  ReplyDelete
 2. Mimi nakutakia heri ya mwaka mpya 2010

  ReplyDelete