Friday, December 18, 2009

Rafiki nenda salama

Huzuni imetushika, hakika twakulilia,
Rafiki umetutoka, umeiacha dunia,
Majonzi yalotufika, vigumu kuelezea,
Rafiki nenda salama, upumzike kwa amani.

Tulikupenda hakika, Mungu akawa zaidi,
Leo wewe kututoka, hatulii makusudi,
Mioyo imepondeka, tungetamani urudi,
Rafiki nenda salama, upumzike kwa amani.

Ingekuwapo rufani, kututoka tungepinga,
Ila haiwezekani, Mola ndiye anapanga,
Dunia tu safarini, siku mwamba tunagonga,
Rafiki nenda salama, upumzike kwa amani.

Kweli tulikuzowea, na tukakupenda pia,
Mema ukituombea, katika hii dunia,
Leo umetukimbia, hat’wachi kukulilia,
Rafiki nenda salama, upumzike kwa amani.

Haupo nasi kimwili, lakini kiroho upo,
Ituwie kila hali, tukumbuke tusalipo,
Kwa matendo na akili, na kinywa kitamkapo,
Rafiki nenda salama, upumzike kwa amani.

Wewe umetangulia, kwani dunia si yetu,
Nasi tunafuatia, tutakukuta mwenzetu,
Parapanda italia, nawe katikati yetu,
Rafiki nenda salama, upumzike kwa amani.

Buriani Patricia, upumzike kwa amani,
Mola atakujalia, palipo pema peponi,
Twazidi kukuombea, siku zote duniani,
RAFIKI NENDA SALAMA, UPUMZIKE KWA AMANI.

Leo Ijumaa, Disemba 18, 2009 ni siku ambayo rafiki yetu Patricia Semiti anasindikizwa kupumzika kwenye nyumba yake ya milele. Mola ndiwe muweza wa yote. Mola ndiwe mfariji mkubwa. Tunakuomba uipokee roho yake na kuipa pumziko la amani.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina lake libarikiwe. Amina.

4 comments:

 1. Poleni kwa msiba.
  Patricia apumzike pema.
  Amin!

  ReplyDelete
 2. "Mola ndiwe muweza wa yote. Mola ndiwe mfariji mkubwa. Tunakuomba uipokee roho yake na kuipa pumziko la amani.
  Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina lake libarikiwe. Amina." Nawapa pole wafiwa wote poleni sana kwa msiba marehemu apumzike kwa amani.

  ReplyDelete
 3. Rafiki yetu Gal Patra, Trish, Patricia Neema Semiti amepumzika katika nyumba yake ya milele pale Kinondoni leo jioni. Mungu amjalie pumziko la amani milele yote.
  Amina.

  ReplyDelete
 4. Poleni sana kaka. Mungu awape ujasiri katika kipindi hiki. Sisi ni mavumbi na tutarudi mavumbini. Jina la bwana lihimidiwe.
  Roho ya marehemu Patricia ipumzike kwa amani. Amen.

  ReplyDelete