Sunday, December 20, 2009

Niwapo kimya

Mambo huweza nitinga, niisakapo riziki,
Ukahisi nakutenga, ukahisi sikutaki,
Juwa nasaka mpunga, ili tuishinde dhiki,
Niwapo kimya mpenzi, usidhani sikupendi.

Najua unaumia, kwani huishi lalama,
Nami ninakusikia, huku moyo ‘kiniuma,
Najaribu kuzuia, kwa maneno ninasema,
Niwapo kimya mpenzi, usidhani sikupendi.

Pendo nimekupa wewe, moyo umekuridhia,
Naomba unielewe, baya sitokufanyia,
Hata dawa niwekewe, sikubali kuk’wachia,
Niwapo kimya mpenzi, usidhani sikupendi.

Salamu kweli muhimu, daima kukumbukana,
Huleta mashamshamu, nayo mapenzi kufana,
Ukimya unayo sumu, kama utazidi sana,
Niwapo kimya mpenzi, usidhani sikupendi.

Wewe ni chaguo langu, unipaye mie raha,
Kwenye huu ulimwengu, hunipa mie furaha,
Kukukosa ni uchungu, kukukosa ni karaha,
Niwapo kimya mpenzi, usidhani sikupendi.

Cha moyo changu kidani, daima nikuwazaye,
Nizame mwako dimbwini, ni mimi nikufaaye,
Wewe kwangu kama mboni, mwenye thamani uwaye,
Niwapo kimya mpenzi, usidhani sikup;endi.

4 comments:

 1. Shairi limetulia, mpaka raha usomapo. Natumaini huyo uliyemwandikia amefurahi.

  ReplyDelete
 2. Subira yavuta heri,sikia wangu mwandani,
  Ninayavuka mapori,nakuwaza asilani,
  Kuwa nawe ni fahari,wewe wangu maishani,
  Tafadhali nisubiri,nimetingwa niamini.

  ReplyDelete
 3. Kaka Fadhy
  Kwa niaba ya familia yangu na wapenda mema wote nakutakia kila lililo jema wakati huu wa sikukuu na usalama kuelekea mwaka mpya
  Baraka kwako

  ReplyDelete
 4. Mpenzi unasikia lakini kauli mwanana za Mkuu Fadhy?

  ReplyDelete