Saturday, December 5, 2009

Nimetamani

Nimetamani kusema, leo nitasema yote,
Nataka wenye hekima, wayapime hayo yote,
Wanipe zao tuhuma, penye ujinga nifute,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Nataka towa maoni, sijui atayejali,
Nina machungu moyoni, bora niseme ukweli,
Yanotendeka nchini, yanipa hisia kali,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Tumewaona wakuu, ukweli wakiogopa,
Watwona tuna makuu, maswali wanayakwepa,
Watuweka roho juu, machungu wanayotupa,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Pengine hakuna dira, chombo chaenda mrama,
Wasotumia busara, wanaturudisha nyuma,
Kisa walipewa kura, vyao ndivyo vyote vyema,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Nchi ina utajiri, watu bado masikini,
Lipi sasa lina kheri, lenye faraja moyoni,
Tusome kwenye Zaburi, tusome kwenye Quran?
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Walizotowa ahadi, hawawezi tekeleza,
Ilikuwa makusudi, nasi hatwezi uliza?
Wamejaa ukaidi, tena wenye kuchukiza,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Huduma za kijamii, zaonekana anasa,
Na wao hawasikii, weshachuma zao pesa,
Wamefanya nchi hii, ni shamba lao kabisa,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Nenda hospitalini, huduma zimedorora,
Wagonjwa hulala chini, huduma zisizo bora,
Wa kumlaumu ni nani, ni wao ama wizara?
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Hebu nenda vijijini, uone ilivyo hali,
Wagonjwa wafa njiani, huduma zilivyo mbali,
Uwe na kitu fulani, isiwe mali kauli,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Shule sasa si masomo, kumepatwa dudu gani?
Kila siku ni migomo, twajenga taifa gani?
Kwenye viti waliomo, vichwani wawaza nini?
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Inavuja mitihani, bado hatufanyi kitu,
Elimu kipimo gani, naona si malikitu,
Wal'opo madarakani, waj'ona miungu watu,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Madai yao walimu, mwataka kwanza agua,
Mwaona siyo muhimu, ni lipi mnalojua?
Twahitaji kufahamu, hili linatusumbua,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Hii kitu ufisadi, yawapeni raha gani?
Rushwa ndo zenu juhudi, taifa li hali gani?
Zi wapi zenu stadi, usia upo kapuni?
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Mnayo raha moyoni, japo taifa lalia,
Mu vipofu hamuoni, mambo yamewanogea,
Hata mwenu akilini, hamwezi kufikiria,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Natamani ningeweza, kutoa kwenu hukumu,
Tena ningetekeleza, hata mkinishutumu,
Maana mwatumaliza, kwa kufanya hali ngumu,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Hukumu kwenu ninayo, wala si mbali mwakani,
Kura yangu nipigayo, iwe mkuki moyoni,
Si maneno nisemayo, bali kura mkononi,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Tokeni usingizini, nawaambia wenzangu,
Tuamue kwa makini, kwa uweza wake Mungu,
Isiwe kama zamani, tumeshachoka machungu,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Nimesema ya kusema, waungwana kusikia,
Nilosema nimepima, ni kwenu kukadiria,
T'wamue yetu hatima, tumechoka kuumia,
Nimetamani kusema, wacheni nimeshasema.

3 comments:

 1. Ni sasa ni wakati wa kuamka asnte kwa ujumbe huu mzito.

  ReplyDelete
 2. Pengine hakuna dira, chombo chaenda mrama,
  Wasotumia busara, wanaturudisha nyuma,
  Kisa walipewa kura, vyao ndivyo vyote vyema,
  Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.


  :-(

  ReplyDelete