Tuesday, December 1, 2009

Muda wetu

Fikara bado kuisha, suluhisho kufikia,
Azma kuifanikisha, kwa hatua kuchukua,
Hali hii inachosha, tuiambie dunia,
Tutumie muda wetu.

Sauti iwafikie, wote huko nako kule,
Mbiu wakaisikie, ili wasikose shule,
Balaa waj'epushie, kwa makini wasilale,
Tutumie muda wetu.

Toka thema'ni na tatu, tuligundua nchini,
Kwamba miongoni mwetu, hakuna kinga mwilini,
Iliwashitua watu, hatutaki rudi chini,
Tutumie muda wetu.

Sote tuelimishane, pasipo kuona haya,
Kisha tusaidiane, tusianguke pabaya,
Na mikono tushikane, tukaishinde miwaya,
Tutumie muda wetu.

Tutulie kwenye ndoa, kuyaepuka majanga,
Tusijitie madoa, kuendekeza ujinga,
Jamii kuiokoa, hivyo gonjwa kulipinga,
Tutumie muda wetu.

Hatua kuzichukua, ni jambo la kupendeza,
Hatua kwayo hatua, gonjwa kuliteketeza,
Jamii kuiokoa, siha njema kueneza,
Tutumie muda wetu.

5 comments:

 1. Ni wengi wametutoka,peponi wapumzike,
  Yatima waongezeka,Ukimwi ni chanzo chake,
  wakati umeshafika,ukweli tuuanike,
  Gonjwa hili linatisha,wandugu tubadilike

  ReplyDelete
 2. Ni kweli gonjwa baya,
  Na wengi tunajua,
  Lakini tunapuuzia,
  Na watu tunakwisha.

  Ina bidi uelimishaji uanze mashuleni. Ili wote waelewe ni hatari gani hii katika maisha.

  ReplyDelete
 3. Na bado watu hawataki kwa makusudi kukubali ya kuwa hili gonjwa ni baya.
  Sijui mpaka wachapwe viboko na mkuu wa wilaya au....

  ReplyDelete
 4. Mimi nadhani watu wengi sasa wanafahamu kuhusu UKIMWI kwani karibu kila mtu ameshaguswa na gonjwa hili. Sijui sababu hasa zinazofanya watu kutochukua tahadhari na kujiepusha nalo wakati wanajua kila kitu.

  ReplyDelete
 5. Wakati ukuta...

  Kama moshi wapita,
  Tutumie wetu m'da
  Kuna mengi ya kufanya,
  Bila magonjwa kuyasambaza

  ReplyDelete