Wednesday, December 30, 2009

Wakati mwaka waisha

Mwaka huo wayoyoma, tuwache uende zake,
Wacha uende salama, ulijaa mambo yake,
Tuombacho ni uzima, tupewe baraka zake,
Wakati mwaka waisha, penzi lako haliishi.

Penzi lako haliishi, kama mwaka uishavyo,
Niseme halinichoshi, kama mwaka uchoshavyo,
Wala halikinaishi, vyovyote vile iwavyo,
Wakati mwaka waisha, penzi lako haliishi.

Kwako nimesharidhika, kwingine nif'ate nini?
Nanena kwa uhakika, yanikaayo moyoni,
Sifikiri nitachoka, siku zote maishani,
Wakati mwaka waisha, penzi lako haliishi.

U nuru waniangaza, maisha kunipa raha,
U ua wanipendeza, moyo kujawa furaha,
Sauti yaniliwaza, daima kutoa karaha,
Wakati mwaka waisha, penzi lako haliishi.

U chakula nishibacho, kwingine siwezi kwenda,
U mboni ya langu jicho, daima nitakulinda,
Amini nikisemacho, sidiriki kukutenda,
Wakati mwaka waisha, penzi lako haliishi.

Shida zote za maisha, wewe kwangu ni faraja,
Hofu yangu waishusha, kila tuwapo pamoja,
Daima huniwezesha, kuyavuka madaraja,
Wakati mwaka waisha, penzi lako haliishi.

Sunday, December 20, 2009

Niwapo kimya

Mambo huweza nitinga, niisakapo riziki,
Ukahisi nakutenga, ukahisi sikutaki,
Juwa nasaka mpunga, ili tuishinde dhiki,
Niwapo kimya mpenzi, usidhani sikupendi.

Najua unaumia, kwani huishi lalama,
Nami ninakusikia, huku moyo ‘kiniuma,
Najaribu kuzuia, kwa maneno ninasema,
Niwapo kimya mpenzi, usidhani sikupendi.

Pendo nimekupa wewe, moyo umekuridhia,
Naomba unielewe, baya sitokufanyia,
Hata dawa niwekewe, sikubali kuk’wachia,
Niwapo kimya mpenzi, usidhani sikupendi.

Salamu kweli muhimu, daima kukumbukana,
Huleta mashamshamu, nayo mapenzi kufana,
Ukimya unayo sumu, kama utazidi sana,
Niwapo kimya mpenzi, usidhani sikupendi.

Wewe ni chaguo langu, unipaye mie raha,
Kwenye huu ulimwengu, hunipa mie furaha,
Kukukosa ni uchungu, kukukosa ni karaha,
Niwapo kimya mpenzi, usidhani sikupendi.

Cha moyo changu kidani, daima nikuwazaye,
Nizame mwako dimbwini, ni mimi nikufaaye,
Wewe kwangu kama mboni, mwenye thamani uwaye,
Niwapo kimya mpenzi, usidhani sikup;endi.

Friday, December 18, 2009

Rafiki nenda salama

Huzuni imetushika, hakika twakulilia,
Rafiki umetutoka, umeiacha dunia,
Majonzi yalotufika, vigumu kuelezea,
Rafiki nenda salama, upumzike kwa amani.

Tulikupenda hakika, Mungu akawa zaidi,
Leo wewe kututoka, hatulii makusudi,
Mioyo imepondeka, tungetamani urudi,
Rafiki nenda salama, upumzike kwa amani.

Ingekuwapo rufani, kututoka tungepinga,
Ila haiwezekani, Mola ndiye anapanga,
Dunia tu safarini, siku mwamba tunagonga,
Rafiki nenda salama, upumzike kwa amani.

Kweli tulikuzowea, na tukakupenda pia,
Mema ukituombea, katika hii dunia,
Leo umetukimbia, hat’wachi kukulilia,
Rafiki nenda salama, upumzike kwa amani.

Haupo nasi kimwili, lakini kiroho upo,
Ituwie kila hali, tukumbuke tusalipo,
Kwa matendo na akili, na kinywa kitamkapo,
Rafiki nenda salama, upumzike kwa amani.

Wewe umetangulia, kwani dunia si yetu,
Nasi tunafuatia, tutakukuta mwenzetu,
Parapanda italia, nawe katikati yetu,
Rafiki nenda salama, upumzike kwa amani.

Buriani Patricia, upumzike kwa amani,
Mola atakujalia, palipo pema peponi,
Twazidi kukuombea, siku zote duniani,
RAFIKI NENDA SALAMA, UPUMZIKE KWA AMANI.

Leo Ijumaa, Disemba 18, 2009 ni siku ambayo rafiki yetu Patricia Semiti anasindikizwa kupumzika kwenye nyumba yake ya milele. Mola ndiwe muweza wa yote. Mola ndiwe mfariji mkubwa. Tunakuomba uipokee roho yake na kuipa pumziko la amani.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina lake libarikiwe. Amina.

Thursday, December 17, 2009

Ua limetoweka bustanini

Ua jema la thamani,
Lilopendeza machoni,
Mbona halionekani?
Kwani li wapi jamani?
Mimi nataka kujuwa.

Ninataka kuliona,
Ni ua lililofana,
Ua kifani hakuna,
Ua la pekee sana,
Ua lenye kuvutia.

Nafika bustanini,
Ua hilo silioni,
Kwani li wapi jamani,
Wahka tele moyoni,
Silioni hilo ua.

Nani huyo kalichuma,
Mbona kungali mapema?
Twalitaka ua jema,
Ndivyo twaweza kusema,
Na watu wakasikia.

Ningali mi’ mashakani,
Ua li upande gani?
Kusini, Kaskazini?
Bado tunalitamani,
Tupate lifurahia.

Kigumu kitendawili,
Ulipojiri ukweli,
Iwapo ardhilhali,
Sote hatupo kamili,
Katika hii dunia.

Ua mbali limekwenda,
Huku laacha kidonda,
Simanzi tele kupanda,
Maana hatukupenda,
Ua likatukimbia.

Saa kumbe zasogea,
Simanzi kutuletea,
Na ndivyo inatokea,
Ua letu kupotea,
Huku nasi twaumia.

Mola ua lipokee,
Pale pema likakae,
Adhabu liepushie,
Rehema ulijalie,
Nasi tunaliombea.

Amina.

Mshituko wa kifo cha ghafla cha rafiki yetu na mwanafunzi mwenzetu wa Mkwawa High School, Marehemu Patricia Semiti ni mkubwa. Simanzi imetushika isivyoweza kupimika. Tumempoteza rafiki mwema na mwenye kujali. Trish, japo kimwili hupo nasi tena, kiroho u pamoja nasi daima. Trish, tutakupenda daima. Tutakuwa nawe daima katika sala zetu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aipokee roho yako na kukuangazia mwanga wa milele. Upumzike kwa amani. Amina.

Saturday, December 5, 2009

Nimetamani

Nimetamani kusema, leo nitasema yote,
Nataka wenye hekima, wayapime hayo yote,
Wanipe zao tuhuma, penye ujinga nifute,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Nataka towa maoni, sijui atayejali,
Nina machungu moyoni, bora niseme ukweli,
Yanotendeka nchini, yanipa hisia kali,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Tumewaona wakuu, ukweli wakiogopa,
Watwona tuna makuu, maswali wanayakwepa,
Watuweka roho juu, machungu wanayotupa,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Pengine hakuna dira, chombo chaenda mrama,
Wasotumia busara, wanaturudisha nyuma,
Kisa walipewa kura, vyao ndivyo vyote vyema,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Nchi ina utajiri, watu bado masikini,
Lipi sasa lina kheri, lenye faraja moyoni,
Tusome kwenye Zaburi, tusome kwenye Quran?
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Walizotowa ahadi, hawawezi tekeleza,
Ilikuwa makusudi, nasi hatwezi uliza?
Wamejaa ukaidi, tena wenye kuchukiza,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Huduma za kijamii, zaonekana anasa,
Na wao hawasikii, weshachuma zao pesa,
Wamefanya nchi hii, ni shamba lao kabisa,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Nenda hospitalini, huduma zimedorora,
Wagonjwa hulala chini, huduma zisizo bora,
Wa kumlaumu ni nani, ni wao ama wizara?
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Hebu nenda vijijini, uone ilivyo hali,
Wagonjwa wafa njiani, huduma zilivyo mbali,
Uwe na kitu fulani, isiwe mali kauli,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Shule sasa si masomo, kumepatwa dudu gani?
Kila siku ni migomo, twajenga taifa gani?
Kwenye viti waliomo, vichwani wawaza nini?
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Inavuja mitihani, bado hatufanyi kitu,
Elimu kipimo gani, naona si malikitu,
Wal'opo madarakani, waj'ona miungu watu,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Madai yao walimu, mwataka kwanza agua,
Mwaona siyo muhimu, ni lipi mnalojua?
Twahitaji kufahamu, hili linatusumbua,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Hii kitu ufisadi, yawapeni raha gani?
Rushwa ndo zenu juhudi, taifa li hali gani?
Zi wapi zenu stadi, usia upo kapuni?
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Mnayo raha moyoni, japo taifa lalia,
Mu vipofu hamuoni, mambo yamewanogea,
Hata mwenu akilini, hamwezi kufikiria,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Natamani ningeweza, kutoa kwenu hukumu,
Tena ningetekeleza, hata mkinishutumu,
Maana mwatumaliza, kwa kufanya hali ngumu,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Hukumu kwenu ninayo, wala si mbali mwakani,
Kura yangu nipigayo, iwe mkuki moyoni,
Si maneno nisemayo, bali kura mkononi,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Tokeni usingizini, nawaambia wenzangu,
Tuamue kwa makini, kwa uweza wake Mungu,
Isiwe kama zamani, tumeshachoka machungu,
Nimetamani kusema, wacha niyaseme haya.

Nimesema ya kusema, waungwana kusikia,
Nilosema nimepima, ni kwenu kukadiria,
T'wamue yetu hatima, tumechoka kuumia,
Nimetamani kusema, wacheni nimeshasema.

Tuesday, December 1, 2009

Muda wetu

Fikara bado kuisha, suluhisho kufikia,
Azma kuifanikisha, kwa hatua kuchukua,
Hali hii inachosha, tuiambie dunia,
Tutumie muda wetu.

Sauti iwafikie, wote huko nako kule,
Mbiu wakaisikie, ili wasikose shule,
Balaa waj'epushie, kwa makini wasilale,
Tutumie muda wetu.

Toka thema'ni na tatu, tuligundua nchini,
Kwamba miongoni mwetu, hakuna kinga mwilini,
Iliwashitua watu, hatutaki rudi chini,
Tutumie muda wetu.

Sote tuelimishane, pasipo kuona haya,
Kisha tusaidiane, tusianguke pabaya,
Na mikono tushikane, tukaishinde miwaya,
Tutumie muda wetu.

Tutulie kwenye ndoa, kuyaepuka majanga,
Tusijitie madoa, kuendekeza ujinga,
Jamii kuiokoa, hivyo gonjwa kulipinga,
Tutumie muda wetu.

Hatua kuzichukua, ni jambo la kupendeza,
Hatua kwayo hatua, gonjwa kuliteketeza,
Jamii kuiokoa, siha njema kueneza,
Tutumie muda wetu.