Monday, November 2, 2009

Uvivu niondokee

Nimekuwa na uvivu, sijui waja na nini,
Mawazo yawa makavu, sinalo jipya kichwani,
Tabia hii ni mbovu, siipendi asilani,
Uvivu niondokee.

Uvivu wa kuandika, mbona unaniandama?
Na sikutaki ondoka, mbona unanisakama,
Na siwezi kukutaka, wewe si rafiki mwema,
Uvivu niondokee.

Wewe ni mtu mbaya, wala usinizowee,
Tena huna hata haya, hebu uniondokee,
Usidhani nakugwaya, na usinitembelee,
Uvivu niondokee.

Wanifanya mi mjinga, tena niso na maana,
Kwako mi umenifunga, na kunitesa kwa sana,
Hadharani nakupinga, sitaki nikwone tena,
Uvivu niondokee.

Mimi si mtumwa wako, unikome ukomae,
Sizitaki nira zako, kwa haraka utambae,
Rudi huko utokako, kuja kwangu ukatae,
Uvivu niondokee.

Leo ninasema wazi, siku hizi 'meniteka,
Kuendelea siwezi, nasema wazi ondoka,
Nataka kufanya kazi, siachi mi kuandika,
Uvivu niondokee.

Nenda kwangu usirudi, asilani abadani,
Niache mi nifaidi, mawazo pevu kichwani,
Na ninatoa ahadi, sikutaki maishani,
Uvivu usirudi tena.

4 comments:

  1. Nilikuwa nikifikiri umeacha kuandik. Nashukuru kama umeufukuza uvivu. Ahsante.

    ReplyDelete
  2. Kwa jina la NANIHII pepo la uvivu wa kuandika TOKA!

    Nshakuombea mkuu - na kumbuka ni wale tu wenye imani isemekanao kufaidika na sala!:-(

    ReplyDelete