Saturday, November 7, 2009

Pamoja daima

Wakati wote wa raha, raha tele mioyoni,
Wakati wa furaha, mimi nawe furahani,
Wakati nyota ya jaha, yaangaza maishani,
Mimi nawe tutakuwa, pamwe daima dawamu.

Furahi pamoja nami, tudumishe urafiki,
Langu kamwe sikunyimi, kwa raha ama kwa dhiki,
U sehemu yangu mimi, kukupoteza sitaki,
Mimi nawe tutakuwa, pamwe daima dawamu.

Maisha yana milima, ni kupanda na kushuka,
Dunia siyo salama, hutokea kuteseka,
Kwangu upate egama, dhoruba ikikufika,
Mimi nawe tutakuwa, pamwe daima dawamu.

Mawimbi yakikupiga, sikwachi uzame chini,
Ukishikwa nao woga, ningali mwako pembeni,
Sikwachi kwenye mafiga, sikwachi kikaangoni,
Mimi nawe tutakuwa, pamwe daima dawamu.

Sikubali uanguke, nitakuwa yako nguzo,
Sitaki utaabike, kama ninao uwezo,
Na wala usidhurike, upatwapo matatizo,
Mimi nawe tutakuwa, pamwe daima dawamu.

Unishike nikushike, tuzidi kuwa imara,
Daima nikukumbuke, nikwepushie madhara,
Nisikuache mpweke, nikuombee nusura,
Mimi nawe tutakuwa, pamwe daima dawamu.

Nikuonyeshe upendo, wa thamani na kujali,
Si maneno ni matendo, yenye dhamira ya kweli,
Twenende wetu mwendo, pamoja kwa kila hali,
Mimi nawe tutakuwa, pamwe daima dawamu.

Maisha yanayo siri, hujui lijalo kesho,
Hutokea ujasiri, kukumbwa navyo vitisho,
Kama ilivyo safari, mambo yote yana mwisho,
Mimi nawe tutakuwa, pamwe daima dawamu.

Rafiki una thamani, siwezi kukupoteza,
Sithubutu abadani, peke kukutelekeza,
Namwomba wetu Manani, an’epushe kuteleza,
Mimi nawe tutakuwa, pamwe daima dawamu.

Kaditama namaliza, rafiki ninakupenda,
Sichoki kukueleza, daima nitakulinda,
Nasi tumwombe Muweza, kokote tunakokwenda
Mimi nawe tutakuwa, pamwe daima dawamu.

5 comments:

 1. PAMOJA DAIMA! nimependa kicha hiki cha habari. nanukuu
  "Furahi pamoja nami, tudumishe urafiki,
  Langu kamwe sikunyimi, kwa raha ama kwa dhiki,
  U sehemu yangu mimi, kukupoteza sitaki,
  Mimi nawe tutakuwa, pamwe daima dawamu." mwisho wa kunuuu. Rafiki yako ana raha kweli kuandikiwa mashairi matamu kama haya. Natumai huyo rafiki anasoma hili shairi

  ReplyDelete
 2. big up sana..... kazi nzuri mkuu.

  ReplyDelete
 3. big up sana..... kazi nzuri mkuu.

  ReplyDelete
 4. Ahsante sana da Yasinta na Anon kwa kulipenda shairi hili. Ningetamani nyote mngezisoma hisia halisi wakati nikiandika, lakini maneno yaliyomo yanaeleza vema.
  Pamoja daima.

  ReplyDelete
 5. Sina la kuongezea hapa Fadhy... shukran kwa ushairi mtamu.

  ReplyDelete