Saturday, November 14, 2009

Nasema ahsante sana

Nakushuru sana Mungu, mema umenijalia,
Ewe muumbaji wangu, sifa nakurudishia,
Bariki maisha yangu, uniangazie njia,
Nasema ahsante sana.

Nakushukuru sana mama, kwanza ni kwa kunizaa,
Umenilea kwa wema, kwa nyota inayong'aa,
Nitashukuru daima, umeniwashia taa,
Nasema ahsante sana.

Nakushukuru mwandani, mpenzi wa moyo wangu,
Kwangu unayo thamani, kwani u sehemu yangu,
Daima uwe pembeni, sitoweza peke yangu,
Nasema ahsante sana.

Ndugu nawashukuruni, mnanithamini sana,
Tangu mwangu utotoni, tungali tukipendana,
Ninawapenda moyoni, na mbarikiwe sana,
Nasema ahsante sana.

Nashukuru marafiki, Mungu amenijalia,
Tungali tupo lukuki, pamoja twafurahia,
Kwa raha ama kwa dhiki, ndani ya hii dunia,
Nasema ahsante sana.

Siku niliyozaliwa, ambayo naadhimisha,
Furaha niliyojawa, ninyi mmesababisha,
Kwa umoja tumekuwa, imara kwenye maisha,
Nasema ahsante sana.

Upendo ndiyo silaha, hakika tunapendana,
Upendo una furaha, kweli twafurahiana,
Na hivyo huleta raha, raha kifani hakuna,
Nasema ahsante sana.

Ahsante pasi kipimo, nawashukuruni sana,
Upendo pasi kikomo, ninawapendeni sana,
Furaha tele iwemo, maisha marefu sana,
NASEMA AHSANTE SANA.

Nawashukuruni sana, mara zisizo na idadi kwa upendo wenu muuoneshao kwangu, siku zote. Ninatamani kusema maneno mengi kuonesha wingi wa furaha na shukrani zangu kwenu, lakini maneno hayajitoshelezi. Ninasema, nawashukuruni sana, ninawapenda sana, na ninawaombea furaha na mafanikio daima.
Pamoja sana.

7 comments:

 1. Kaka
  Kama ni wema kwako ni kwa kuwa u mwema kwetu
  Tunashukuru kwa kuwa namna ulivyo na TUNAJIVUNIA KUWA NAWE
  Blessings

  ReplyDelete
 2. Nakuombea kwa siku hii ya leo kwa SALA hii:- Mungu akubariki, akuongoze, akufariji na akusaidie katika mambo yako. Hongera kwa siku ya KUZALIWA FADHILI.

  ReplyDelete
 3. Hongera kaka Fadhy, Mungu akubari, akuongoze na akufanikishe kuadhisha siku hii mara nyingi zaidi ya nyingi. Mungu akulinde, akuongoze vema, akupe amani, upendo na mafanikio zaidi na zaidi ktk maisha.

  ReplyDelete
 4. Nami nasema ahsante,
  Kwa kuniinua kimawazo,
  Kwa ushauri bila kikwazo,
  Hata mie maneno yamenipotea kwa leo
  Ahsante Fadhy...
  Shukran jazila.

  ReplyDelete
 5. Hongera sana twakutatakia maisha marefu mema, Happy Birthday

  ReplyDelete