Wednesday, November 11, 2009

Nakupa wewe zawadi

Nimekaa nikawaza, nini unastahili,
Jambo lenye kupendeza, jambo lenye kuhawili,
Vema lenye kueleza, kwazo hisia kamili,
Nakupa wewe zawadi, nayo ni pendo la dhati.

Kila nachofikiria, bado siwezi ridhika,
Kiwezacho kufikia, mapenzi yalotukuka,
Mola alokujalia, yale yasomithilika,
Nakupa wewe zawadi, nayo ni pendo la dhati.

Wanifaa kila hali, niwache niseme mie,
Wanipa pendo la kweli, niache nijisikie,
Kwako natulia tuli, wewe nikufurahie,
Nakupa wewe zawadi, nayo ni pendo la kweli.

Zawadi hii pokea, nakupa kwa moyo wote,
Mi ndo nilokuchagua, sikulala nikupate,
Pendo halitopungua, nifae maisha yote,
Nakupa wewe zawadi, nayo ni pendo la kweli.

Nitakwonyesha upendo, tena kutoka moyoni,
Unipime kwa matendo, si maneno mdomoni,
Ufae wangu mwenendo, nisikujaze huzuni,
Nakupa wewe zawadi, nayo ni pendo la kweli.

Nitakwombea daima, Mola azidi jalia,
Ili panapo uzima, pendo lizidi kukua,
Imara tweze simama, ndani ya hii dunia,
Nakupa wewe zawadi, nayo ni pendo la kweli.

Nakupenda sana mie, maneno hayatatosha,
Mpenzi unisikie, wewe ndiye wanitosha,
Njoo ukanitibie, homa yangu kuishusha,
Nakupa wewe zawadi, nayo ni pendo la dhati.

Watasema sana watu, ni maneno tuu hayo,
Kwako siogopi kitu, kwa maneno wasemayo,
Sikuachi wewe katu, kwa mapenzi unipayo,
Nakupa wewe zawadi, nayo ni pendo la dhati.

Zinatosha beti kenda, wewe ninajivunia,
Sitochoka kukupenda, kwa penzi linalokua,
Kokote nitakokwenda, zawadi ‘takutunzia,
Nakupa wewe zawadi, nayo ni pendo la kweli.

4 comments:

 1. Nanukuu "Zawadi hii pokea, nakupa kwa moyo wote,
  Mi ndo nilokuchagua, sikulala nikupate,
  Pendo halitopungua, nifae maisha yote,
  Nakupa wewe zawadi, nayo ni pendo la kweli" mwisho wa kunukuu. Huyu wifi ana bahati kweli kuandikiwa shairi kama hili nategemee umemsomea au umemwambia haya yote mie nasubiri kadi ya harusi tu...lol. Pia nakutakia kila la kheri.

  ReplyDelete
 2. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!November 11, 2009 at 6:51 PM

  yawezekana pia wanadanganyana ili akipate hicho akimanicho....lol

  good piece...lol

  ReplyDelete
 3. Kaka, sidhani kama naweza kuupoteza muda wangu na kuandika shairi ili kumdanganya mtu. Ninachoshukuru ninayemwandikia ananifahamu vema tabia yangu. Kabla sijaandika shairi limhusulo, huwa namwambia vile nijisikiavyo.
  Hivyo ndivyo ilivyo.

  ReplyDelete
 4. enyi waume wapendeni wake zenu...hongera mkuu kwa kutimiza andiko hilo ushauri wangu kwako ni kwamba kaza buti mpaka fainali

  ReplyDelete