Sunday, November 22, 2009

Hongera bwana Given

Salamu nakuletea, rafiki yangu Given,
Neema nakuombea, kheri nyingi duniani,
Mola amekunyo’shea, kukupa matumaini,
Hongera bwana Given, kwa kumpata mtoto.

Mola amekubarikia, tangu ungali tumboni,
Njia kakufungulia, mapitoyo duniani,
Heshi kukusimamia, daima uwe mwangani,
Hongera bwana Given, kwa kumpata mtoto.

Mke mwema umepewa, chaguo lako moyoni,
Naye heshima katowa, kaleta nuru nyumbani,
Na Mola mkajaliwa, kwa upendo na amani,
Hongera bwana Given, kwa kumpata mtoto.

Kweli Mungu kajalia, tangia mimba tumboni,
Afya kaisimamia, maradhi yawe pembeni,
Siku itapofikia, sote tuzame rahani,
Hongera bwana Given, kwa kumpata mtoto.

Na siku ikafikia, toto kaja duniani,
Mkeo kakuzalia, kwayo kheri na amani,
Kama alivyojalia, muumba wetu Manani,
Hongera bwana Given, kwa kumpata mtoto.

Nasi tunafurahia, twamkaribisha mgeni,
Daima tutamwombea, maishaye duniani,
Vema apate kukua, kwingine awe kifani,
Hongera bwana Given, kwa kumpata mtoto.

Somo ninakupatia, kwa bintiyo wa thamani,
Kwa wema ukamlea, akuwe kwenye imani,
Aishike njema njia, kwenu awe tumaini,
Hongera bwana Given, kwa kumpata mtoto.

Nasi tunapaswa pia, kutokuketi pembeni,
Bali ni kusaidia, kuilea yake shani,
Apate kufurahia, siku zote maishani,
Hongera bwana Given, kwa kumpata mtoto.

Beti kenda naishia, rafiki toka zamani,
Siachi kukuombea, baraka kwake Manani,
Kheri kwa shemeji pia, ninasema hongereni,
Hongera bwana Given, kwa kumpata mtoto.


Nakupa pongezi nyingi rafiki yangu wa miaka nenda miaka rudi bwana Given Awadh Msigwa na mkeo kwa kubarikiwa kupata mtoto wa kike hapo jana tarehe 21 Novemba 2009. Maneno yoyote hayawezi kuelezea furaha na hisia zangu. Ninamwomba Mwenyezi Mungu awajalie furaha tele na kheri ili muweze kumlea binti yenu kwa uzuri na hali ipendezayo ili maisha yake yajae mafanikio, furaha na amani.
Pamoja sana mkuu, furaha yako furaha yangu pia.
Amina.

5 comments:

  1. Nami nasema HONGERA rafiki yetu maaan rafiki yako mtani ni rafiki yangu au nimekosea.

    ReplyDelete
  2. asante sana mkuu kwa shairi zuri..najisikia furaha sana kupata nafasi ya kuitwa baba ktk kipindi cha maishsha yangu chini y a jua.

    ReplyDelete
  3. Nasi tunaungana nawe kutoa pongezi za heri kwa rafikiyo.

    ReplyDelete