Sunday, November 22, 2009

Hongera bwana Given

Salamu nakuletea, rafiki yangu Given,
Neema nakuombea, kheri nyingi duniani,
Mola amekunyo’shea, kukupa matumaini,
Hongera bwana Given, kwa kumpata mtoto.

Mola amekubarikia, tangu ungali tumboni,
Njia kakufungulia, mapitoyo duniani,
Heshi kukusimamia, daima uwe mwangani,
Hongera bwana Given, kwa kumpata mtoto.

Mke mwema umepewa, chaguo lako moyoni,
Naye heshima katowa, kaleta nuru nyumbani,
Na Mola mkajaliwa, kwa upendo na amani,
Hongera bwana Given, kwa kumpata mtoto.

Kweli Mungu kajalia, tangia mimba tumboni,
Afya kaisimamia, maradhi yawe pembeni,
Siku itapofikia, sote tuzame rahani,
Hongera bwana Given, kwa kumpata mtoto.

Na siku ikafikia, toto kaja duniani,
Mkeo kakuzalia, kwayo kheri na amani,
Kama alivyojalia, muumba wetu Manani,
Hongera bwana Given, kwa kumpata mtoto.

Nasi tunafurahia, twamkaribisha mgeni,
Daima tutamwombea, maishaye duniani,
Vema apate kukua, kwingine awe kifani,
Hongera bwana Given, kwa kumpata mtoto.

Somo ninakupatia, kwa bintiyo wa thamani,
Kwa wema ukamlea, akuwe kwenye imani,
Aishike njema njia, kwenu awe tumaini,
Hongera bwana Given, kwa kumpata mtoto.

Nasi tunapaswa pia, kutokuketi pembeni,
Bali ni kusaidia, kuilea yake shani,
Apate kufurahia, siku zote maishani,
Hongera bwana Given, kwa kumpata mtoto.

Beti kenda naishia, rafiki toka zamani,
Siachi kukuombea, baraka kwake Manani,
Kheri kwa shemeji pia, ninasema hongereni,
Hongera bwana Given, kwa kumpata mtoto.


Nakupa pongezi nyingi rafiki yangu wa miaka nenda miaka rudi bwana Given Awadh Msigwa na mkeo kwa kubarikiwa kupata mtoto wa kike hapo jana tarehe 21 Novemba 2009. Maneno yoyote hayawezi kuelezea furaha na hisia zangu. Ninamwomba Mwenyezi Mungu awajalie furaha tele na kheri ili muweze kumlea binti yenu kwa uzuri na hali ipendezayo ili maisha yake yajae mafanikio, furaha na amani.
Pamoja sana mkuu, furaha yako furaha yangu pia.
Amina.

Saturday, November 14, 2009

Nasema ahsante sana

Nakushuru sana Mungu, mema umenijalia,
Ewe muumbaji wangu, sifa nakurudishia,
Bariki maisha yangu, uniangazie njia,
Nasema ahsante sana.

Nakushukuru sana mama, kwanza ni kwa kunizaa,
Umenilea kwa wema, kwa nyota inayong'aa,
Nitashukuru daima, umeniwashia taa,
Nasema ahsante sana.

Nakushukuru mwandani, mpenzi wa moyo wangu,
Kwangu unayo thamani, kwani u sehemu yangu,
Daima uwe pembeni, sitoweza peke yangu,
Nasema ahsante sana.

Ndugu nawashukuruni, mnanithamini sana,
Tangu mwangu utotoni, tungali tukipendana,
Ninawapenda moyoni, na mbarikiwe sana,
Nasema ahsante sana.

Nashukuru marafiki, Mungu amenijalia,
Tungali tupo lukuki, pamoja twafurahia,
Kwa raha ama kwa dhiki, ndani ya hii dunia,
Nasema ahsante sana.

Siku niliyozaliwa, ambayo naadhimisha,
Furaha niliyojawa, ninyi mmesababisha,
Kwa umoja tumekuwa, imara kwenye maisha,
Nasema ahsante sana.

Upendo ndiyo silaha, hakika tunapendana,
Upendo una furaha, kweli twafurahiana,
Na hivyo huleta raha, raha kifani hakuna,
Nasema ahsante sana.

Ahsante pasi kipimo, nawashukuruni sana,
Upendo pasi kikomo, ninawapendeni sana,
Furaha tele iwemo, maisha marefu sana,
NASEMA AHSANTE SANA.

Nawashukuruni sana, mara zisizo na idadi kwa upendo wenu muuoneshao kwangu, siku zote. Ninatamani kusema maneno mengi kuonesha wingi wa furaha na shukrani zangu kwenu, lakini maneno hayajitoshelezi. Ninasema, nawashukuruni sana, ninawapenda sana, na ninawaombea furaha na mafanikio daima.
Pamoja sana.

Wednesday, November 11, 2009

Nakupa wewe zawadi

Nimekaa nikawaza, nini unastahili,
Jambo lenye kupendeza, jambo lenye kuhawili,
Vema lenye kueleza, kwazo hisia kamili,
Nakupa wewe zawadi, nayo ni pendo la dhati.

Kila nachofikiria, bado siwezi ridhika,
Kiwezacho kufikia, mapenzi yalotukuka,
Mola alokujalia, yale yasomithilika,
Nakupa wewe zawadi, nayo ni pendo la dhati.

Wanifaa kila hali, niwache niseme mie,
Wanipa pendo la kweli, niache nijisikie,
Kwako natulia tuli, wewe nikufurahie,
Nakupa wewe zawadi, nayo ni pendo la kweli.

Zawadi hii pokea, nakupa kwa moyo wote,
Mi ndo nilokuchagua, sikulala nikupate,
Pendo halitopungua, nifae maisha yote,
Nakupa wewe zawadi, nayo ni pendo la kweli.

Nitakwonyesha upendo, tena kutoka moyoni,
Unipime kwa matendo, si maneno mdomoni,
Ufae wangu mwenendo, nisikujaze huzuni,
Nakupa wewe zawadi, nayo ni pendo la kweli.

Nitakwombea daima, Mola azidi jalia,
Ili panapo uzima, pendo lizidi kukua,
Imara tweze simama, ndani ya hii dunia,
Nakupa wewe zawadi, nayo ni pendo la kweli.

Nakupenda sana mie, maneno hayatatosha,
Mpenzi unisikie, wewe ndiye wanitosha,
Njoo ukanitibie, homa yangu kuishusha,
Nakupa wewe zawadi, nayo ni pendo la dhati.

Watasema sana watu, ni maneno tuu hayo,
Kwako siogopi kitu, kwa maneno wasemayo,
Sikuachi wewe katu, kwa mapenzi unipayo,
Nakupa wewe zawadi, nayo ni pendo la dhati.

Zinatosha beti kenda, wewe ninajivunia,
Sitochoka kukupenda, kwa penzi linalokua,
Kokote nitakokwenda, zawadi ‘takutunzia,
Nakupa wewe zawadi, nayo ni pendo la kweli.

Saturday, November 7, 2009

Pamoja daima

Wakati wote wa raha, raha tele mioyoni,
Wakati wa furaha, mimi nawe furahani,
Wakati nyota ya jaha, yaangaza maishani,
Mimi nawe tutakuwa, pamwe daima dawamu.

Furahi pamoja nami, tudumishe urafiki,
Langu kamwe sikunyimi, kwa raha ama kwa dhiki,
U sehemu yangu mimi, kukupoteza sitaki,
Mimi nawe tutakuwa, pamwe daima dawamu.

Maisha yana milima, ni kupanda na kushuka,
Dunia siyo salama, hutokea kuteseka,
Kwangu upate egama, dhoruba ikikufika,
Mimi nawe tutakuwa, pamwe daima dawamu.

Mawimbi yakikupiga, sikwachi uzame chini,
Ukishikwa nao woga, ningali mwako pembeni,
Sikwachi kwenye mafiga, sikwachi kikaangoni,
Mimi nawe tutakuwa, pamwe daima dawamu.

Sikubali uanguke, nitakuwa yako nguzo,
Sitaki utaabike, kama ninao uwezo,
Na wala usidhurike, upatwapo matatizo,
Mimi nawe tutakuwa, pamwe daima dawamu.

Unishike nikushike, tuzidi kuwa imara,
Daima nikukumbuke, nikwepushie madhara,
Nisikuache mpweke, nikuombee nusura,
Mimi nawe tutakuwa, pamwe daima dawamu.

Nikuonyeshe upendo, wa thamani na kujali,
Si maneno ni matendo, yenye dhamira ya kweli,
Twenende wetu mwendo, pamoja kwa kila hali,
Mimi nawe tutakuwa, pamwe daima dawamu.

Maisha yanayo siri, hujui lijalo kesho,
Hutokea ujasiri, kukumbwa navyo vitisho,
Kama ilivyo safari, mambo yote yana mwisho,
Mimi nawe tutakuwa, pamwe daima dawamu.

Rafiki una thamani, siwezi kukupoteza,
Sithubutu abadani, peke kukutelekeza,
Namwomba wetu Manani, an’epushe kuteleza,
Mimi nawe tutakuwa, pamwe daima dawamu.

Kaditama namaliza, rafiki ninakupenda,
Sichoki kukueleza, daima nitakulinda,
Nasi tumwombe Muweza, kokote tunakokwenda
Mimi nawe tutakuwa, pamwe daima dawamu.

Monday, November 2, 2009

Uvivu niondokee

Nimekuwa na uvivu, sijui waja na nini,
Mawazo yawa makavu, sinalo jipya kichwani,
Tabia hii ni mbovu, siipendi asilani,
Uvivu niondokee.

Uvivu wa kuandika, mbona unaniandama?
Na sikutaki ondoka, mbona unanisakama,
Na siwezi kukutaka, wewe si rafiki mwema,
Uvivu niondokee.

Wewe ni mtu mbaya, wala usinizowee,
Tena huna hata haya, hebu uniondokee,
Usidhani nakugwaya, na usinitembelee,
Uvivu niondokee.

Wanifanya mi mjinga, tena niso na maana,
Kwako mi umenifunga, na kunitesa kwa sana,
Hadharani nakupinga, sitaki nikwone tena,
Uvivu niondokee.

Mimi si mtumwa wako, unikome ukomae,
Sizitaki nira zako, kwa haraka utambae,
Rudi huko utokako, kuja kwangu ukatae,
Uvivu niondokee.

Leo ninasema wazi, siku hizi 'meniteka,
Kuendelea siwezi, nasema wazi ondoka,
Nataka kufanya kazi, siachi mi kuandika,
Uvivu niondokee.

Nenda kwangu usirudi, asilani abadani,
Niache mi nifaidi, mawazo pevu kichwani,
Na ninatoa ahadi, sikutaki maishani,
Uvivu usirudi tena.