Monday, October 5, 2009

Upweke

Upweke jama adhabu, upweke unasumbua,
Upweke ni maghilibu, kukufanya kuugua,
Watamani wa karibu, nenolo taelijua,
Upweke.

Upweke hutesa sana, umpendaye awe mbali,
Utamuwazia sana, hata mara alfu mbili,
Kwa usiku na mchana, maumivu ni makali,
Upweke.

Upweke unakondesha, chakula hukitamani,
Upweke unahenyesha, simanzi tele moyoni,
Homa pia hupandisha, na mwokozi humuoni,
Upweke.

Upweke tele mateso, hata machozi kulia,
Moyoni ni manyanyaso, nao moyo kuumia,
Wala si kimasomaso, kwani huleta udhia,
Upweke.

Upweke ni kama jela, huleta nyingi simanzi,
Huwezi hata kulala, maisha tele majonzi,
Utapiga hata sala, uruke vyote viunzi,
Upweke.

Upweke sawa na shimo, mtu ukatumbukia,
Nako shimoni uwamo, wateswa nayo dunia,
Kwani hauna makamo, kuweza kuvumilia,
Upweke.

6 comments:

 1. Afadhali kuumwa kichwa kuliko kuwa mpweke. Maana ukuwa mpweke basi unakuwa na mawazo chungu nzima. Shairi hili limetulia kweli na kama u mpweke ukisoma hili upweke unapungua,

  ReplyDelete
 2. Aisifuye mvua imemnyea! Pole sana mkuu lkn usijari sana kwani kila mtihani majibu yake yapo mhimu uvumilivu! Hata wote wakikuacha MUNGU yuko nawe daima.

  ReplyDelete
 3. Inasemekana lakini kuwa UPWEKE ndio kijulisho bado unapenda kwa kuwa kwa kuzoea upendacho kipo unaweza usijistukie umeshaacha kukipenda!

  ReplyDelete
 4. nilidhani mpweke ni mimi
  nilidhani niko peke yangu
  nilihdani ninayo kasoro
  ukweli nilikosea, tulio wapweke tuko wengi

  ReplyDelete
 5. UPWEKE SAWA NA JOKA
  LIUMALO POLE POLE

  HUTOKOMA KUTESEKA
  MOYONI HUZUNI TELE

  SURAYO TASAWIJIKA
  MAWAZO YAKUTAWALE


  UPWEKE MARADHI SIYO
  USIOMBE UKUKUMBE

  ReplyDelete