Monday, October 26, 2009

Rafiki yupo shidani, Mola wangu mnusuru

Ninapiga goti chini, niitoe sala yangu,
Ya dhati toka moyoni, mbele zako ewe Mungu,
Unionaye sirini, na kujua shida zangu,
Rafiki yupo shidani, Mola wangu mnusuru.

Nafikiri naumia, nashindwa la kulifanya,
Mambo yaliyotukia, hakika yanachanganya,
Hivyo ninakulilia, kwake ukawe mponya,
Rafiki yupo shidani, Mola wangu mnusuru.

Maisha si utabiri, ya kesho tukayajua,
Ni vigumu kubashiri, kitakachotusumbua,
Mambo huenda sifuri, na maradhi kuugua,
Rafiki yupo shidani, Mola wangu mnusuru.

Mola wewe mfariji, ufariji moyo wake,
Rafiki yu mhitaji, iangaze njia yake,
Wewe ndiwe mwema jaji, tazama matendo yake,
Rafiki yupo shidani, Mola wangu mnusuru.

Mola wewe kiongozi, umuongoze daima,
Chuki dhidiye zi wazi, umjalie uzima,
Aweze ruka viunzi, abaki kuwa salama,
Rafiki yupo shidani, Mola wangu mnusuru.

Ewe wetu Maulana, umnusuru rafiki,
Angali shidani sana, umuondolee dhiki,
Rafiki tunapendana, huzuni haipimiki,
Rafiki yupo shidani, Mola wangu mnusuru.

Popote alipokosa, Rabana mhurumie,
Wadhalimu wamtesa, ya Karimu umwokoe,
Wanamjengea visa, kilio ukisikie,
Rafiki yupo shidani, Mola wangu mnusuru.

Muumba wangu Manani, uzidi kutujalia,
Nina imani moyoni, kwani wewe husikia,
Hutuachi twende chini, ahsante nakupatia,
Rafiki yupo shidani, Mola wangu mnusuru.

9 comments:

 1. Mola kama inawezekana katika hili , msikilize kijana wako Fadhy .

  ReplyDelete
 2. Wakati mwingine - na pengine niseme mara nyingi - maji yaweza kuwa mazito kuliko damu na huu ni mfano mmojawapo. Mola ameshakisikia kilio chako, nira za maadui zitalegea na mambo ya rafiki yatafunguka!

  ReplyDelete
 3. nawashukuruni nyote, kaka zangu James Adolwa, Simoni Kitururu, Masangu Nzunzullima. Shukrani pia kwa JamZest. kiukweli kuna marafiki ambao ni zaidi ya ndugu. kuna marafiki unaoweza kushibana nao hata wakawa sehemu ya maisha yako. marafiki hawa, matatizo yao ni yako pia. rafiki yangu huyu nimeshibana naye kuliko maelezo yanavyoweza kusema. kwa bahati mbaya amekumbwa na masahibu makubwa sana. siachi kumwombea. ahsanteni kwa sala zenu. naamini mambo hayo yatakwisha haraka. eeh Mwenyezi Mungu, nakuomba umsimamie rafiki yangu kipenzi. pia umpe faraja. ninakushukuru kwani wewe ni mwaminifu siku zote. amina.

  ReplyDelete
 4. Fadhy sala zako tayari Muumba kazipokea. Na nakutakia uwe na nguvu hizo hizo ulizonazo. Ni kweli rafiki ni bora kuliko...Baba umpe nguvu Fadhy ya kuweza kumsaidia rafiki yake. pi mpe nguvu huyo rafiki asipoteze imani yake. Amina.

  ReplyDelete
 5. Pole sana kaka Fadhy na pia umpe pole sana rafiki yako.Rafiki yako ni rafiki yetu pia,sote kwa pamoja tumuelekezee sala zetu. Mungu amuongezee ujasiri, amani, furaha na uvumilivu ktk wakati alionao.

  ReplyDelete