Monday, October 19, 2009

Muungwana ni kitendo

Sikuaga ninakiri, nami nikatokomea,
Msione ni kiburi, kuwa kimenizidia,
Aibu hii dhahiri, kweli nimewakosea.

Msamaha naombeni, maana nimekosea,
Nikaingia mitini, kwa heri sikuw'ambia,
Msinitenge kundini, maana nitafulia.

Majambo yamenikumba, nashindwa kusimulia,
Ila mimi nawaomba, ihsani kunifanyia,
Ili nisiweze yumba, nikateswa na dunia.

Dunia kweli ni shule, kwa yanayotutokea,
Uwe huku ama kule, huwezi kuyakimbia,
Yakupasa usilale, maisha kupigania.

Hivyo mie naja kwenu, najua nimekosea,
Sikuwapeni fununu, yapi yamenitokea,
Siyo maji kwenye kinu, ninachohangaikia.

2 comments:

 1. Ni kweli ghfla ulipotea na wasiwasi ukatukamata, ila tungefurahi kujua ni nini kinakusibu. Kwani ukizingatia tu kama ndugu au marafiki. Nakutakia kila la kheri yote Mungu akunyooshee. Tupo pamoja.

  ReplyDelete
 2. Hapana haiwezekani, Mtanga nakwambia
  Utoweke kijiweni, kuhangaika na njia
  Kuiweka sirini, safari uloishia
  Tuambie ndugu yetu, sababu za kutokomea

  Twasubiri kwa hamu, masikio twapanua
  Hatutakulaumu, ukweli ukipambanua
  Wewe mtu muhimu, kila mtu anajua
  Tuambie ndugu yetu, sababu za kutokomea

  ReplyDelete