Monday, October 26, 2009

Rafiki yupo shidani, Mola wangu mnusuru

Ninapiga goti chini, niitoe sala yangu,
Ya dhati toka moyoni, mbele zako ewe Mungu,
Unionaye sirini, na kujua shida zangu,
Rafiki yupo shidani, Mola wangu mnusuru.

Nafikiri naumia, nashindwa la kulifanya,
Mambo yaliyotukia, hakika yanachanganya,
Hivyo ninakulilia, kwake ukawe mponya,
Rafiki yupo shidani, Mola wangu mnusuru.

Maisha si utabiri, ya kesho tukayajua,
Ni vigumu kubashiri, kitakachotusumbua,
Mambo huenda sifuri, na maradhi kuugua,
Rafiki yupo shidani, Mola wangu mnusuru.

Mola wewe mfariji, ufariji moyo wake,
Rafiki yu mhitaji, iangaze njia yake,
Wewe ndiwe mwema jaji, tazama matendo yake,
Rafiki yupo shidani, Mola wangu mnusuru.

Mola wewe kiongozi, umuongoze daima,
Chuki dhidiye zi wazi, umjalie uzima,
Aweze ruka viunzi, abaki kuwa salama,
Rafiki yupo shidani, Mola wangu mnusuru.

Ewe wetu Maulana, umnusuru rafiki,
Angali shidani sana, umuondolee dhiki,
Rafiki tunapendana, huzuni haipimiki,
Rafiki yupo shidani, Mola wangu mnusuru.

Popote alipokosa, Rabana mhurumie,
Wadhalimu wamtesa, ya Karimu umwokoe,
Wanamjengea visa, kilio ukisikie,
Rafiki yupo shidani, Mola wangu mnusuru.

Muumba wangu Manani, uzidi kutujalia,
Nina imani moyoni, kwani wewe husikia,
Hutuachi twende chini, ahsante nakupatia,
Rafiki yupo shidani, Mola wangu mnusuru.

Monday, October 19, 2009

Muungwana ni kitendo

Sikuaga ninakiri, nami nikatokomea,
Msione ni kiburi, kuwa kimenizidia,
Aibu hii dhahiri, kweli nimewakosea.

Msamaha naombeni, maana nimekosea,
Nikaingia mitini, kwa heri sikuw'ambia,
Msinitenge kundini, maana nitafulia.

Majambo yamenikumba, nashindwa kusimulia,
Ila mimi nawaomba, ihsani kunifanyia,
Ili nisiweze yumba, nikateswa na dunia.

Dunia kweli ni shule, kwa yanayotutokea,
Uwe huku ama kule, huwezi kuyakimbia,
Yakupasa usilale, maisha kupigania.

Hivyo mie naja kwenu, najua nimekosea,
Sikuwapeni fununu, yapi yamenitokea,
Siyo maji kwenye kinu, ninachohangaikia.

Monday, October 5, 2009

Upweke

Upweke jama adhabu, upweke unasumbua,
Upweke ni maghilibu, kukufanya kuugua,
Watamani wa karibu, nenolo taelijua,
Upweke.

Upweke hutesa sana, umpendaye awe mbali,
Utamuwazia sana, hata mara alfu mbili,
Kwa usiku na mchana, maumivu ni makali,
Upweke.

Upweke unakondesha, chakula hukitamani,
Upweke unahenyesha, simanzi tele moyoni,
Homa pia hupandisha, na mwokozi humuoni,
Upweke.

Upweke tele mateso, hata machozi kulia,
Moyoni ni manyanyaso, nao moyo kuumia,
Wala si kimasomaso, kwani huleta udhia,
Upweke.

Upweke ni kama jela, huleta nyingi simanzi,
Huwezi hata kulala, maisha tele majonzi,
Utapiga hata sala, uruke vyote viunzi,
Upweke.

Upweke sawa na shimo, mtu ukatumbukia,
Nako shimoni uwamo, wateswa nayo dunia,
Kwani hauna makamo, kuweza kuvumilia,
Upweke.