Thursday, September 10, 2009

Usichoke

Maisha ni kama vita, usichoke kupigana,
Hata kama ukigota, endelea kupambana,
Bado muda wa kutweta, bado ni mapema sana,
Usichoke mwanakwetu.

Nenda shule ukasome, uongeze maarifa,
Ukiwa huko jitume, uliinue taifa,
Nenda kakazane shime, utajipatia sifa,
Usichoke mwanakwetu.

Amka wahi kazini, ili uongeze tija,
Ujuzi wako kichwani, taifa linaungoja,
Ujitume ofisini, na wenzako kwa pamoja,
Usichoke mwanakwetu.

Pigana pasi kuchoka, yapiganie maisha,
Jitihada zako weka, ustawi kufanikisha,
Kwa dhamira ya hakika, malengo kufanikisha,
Usichoke mwanakwetu.

Mwiko kukata tamaa, bado ni ndefu safari,
Kurudi nyuma kataa, pambana nazo hatari,
Tumia kila wasaa, maisha kutafakari,
Usichoke mwanakwetu.

Usifanye masikhara, maisha hayendi hivyo,
Kwa hiyo kuwa imara, vile iwezekanavyo,
Nawe utazidi ng'ara, namna itakiwavyo,
Usichoke mwanakwetu.

10 comments:

 1. Ni kweli Inabidi tusikate tamaaa katika maisha ni lazima kujaribu kufanya kila liwezekanali ili maisha yaende safi. Lakini kunakuwa na wakti unachoka na unakata tamaa. Ahsante kwa hili shairi kwani mimi nilikuwa najihisi kuchoka sasa baada ya kusoma hapa nimepata nguvu na natuini zitabaki. shukrani.

  ReplyDelete
 2. inabidi ili shairi liwekwe kila mahali watu walisome.

  ReplyDelete
 3. Nashukuru da Yasinta kuwa lengo la kuliandika shairi hili ili kuhamasisha watu katika mapambano ya maisha limefanikiwa kwako.
  Kaka Chib nashukuru kwa kuona umuhimu wa tungo hii. Ruksa kuiweka popote.
  Tusichoke. Bado ni mapema sana.

  ReplyDelete
 4. Kweli bado ni mapema, hata jua halijazama, wanakwetu hatuna budi kujituma.
  Walishasema, kuwa mwanangu uyaone, si majumba,sasa ni nini?
  ni maisha tu.
  Kila la heri.

  ReplyDelete
 5. Nafuata ushauri wa kaka Chib ni kweli inabidi wengi wasome kwa hiyo nachukua na kuweka pale kwangu. Nadhani hautajali mtani.

  ReplyDelete
 6. Maisha ni kila kitu, maisha si mtu kitu, maisha yataka utu, maisha huendelea..

  Maisha ya zama butu, maisha binafsi ya mtu,usiyachunguze katu,maisha kujongelea....

  Maisha enyi watu, kumbukeni wenu utu, katu msije na vitu,balaa kukaribia....

  Maisha dunia si kitu, sote twahaha na watu,tusichunguze katu,tupate kufanikiwa.....

  ReplyDelete
 7. Kissima karibu sana Mwanamalenga wangu. Ila nitafurahi kama utaongeza bidii katika kuandika mashairi kibarazani kwako pale. Tunapaswa kuhakikisha sana ya ushairi inainuka zaidi na zaidi.

  Da Yasinta nimepita kibarazani kwako na kuona "Usichoke" nakushukuru sana.

  Kaka Mkwinda hatujakamatana kitambo. Karibu sana mwanakwetu. Pia shukrani mara alfu lela ulela kwa kibwagizo chako muruwa. Hakika sanaa ya ushairi ipo juu, juu mno.

  Mtakatifu Simon, pamoja kama kawa, leo na kesho, na mtondo, na mtondogoo.........duh.....!!!

  Nawashukuruni wajameni. Msichoke.

  ReplyDelete
 8. ahsante kaka James. Usichoke. Nami sitochoka.

  ReplyDelete