Thursday, September 17, 2009

Mola wangu nisamehe

Mola unayenipenda, unipaye afya njema,
Mlinzi ninapokwenda, wanijalia uzima,
Kwa dhambi ninazotenda, unionee huruma,
Mola wangu unisamehe.

Matendo yangu mabaya, tena yenye kuchukiza,
Nitendayo bila haya, wengine kuwaumiza,
Kwa kila lililo baya, na bado nikajikweza,
Mola wangu nisamehe.

Niyatendayo sirini, najidanganya mwenyewe,
Japo watu hawaoni, lakini waona wewe,
Nisipoteze imani, naomba nikombolewe,
Mola wangu nisamehe.

Machafu mawazo yangu, na mengine ya moyoni,
Husuda kwao wenzangu, ugomvi na majirani,
Usin'ache peke yangu, nitaishia njiani,
Mola wangu nisamehe.

Maneno yangu machafu, maneno yenye kuudhi,
Mimi si mkamilifu, sipendi nikose radhi,
Siitaki tena hofu, dhambi isiwe maradhi,
Mola wangu nisamehe.

Mola wangu naja kwako, baraka unijalie,
Niokoe mja wako, dunia 'sinizuzue,
Na utukufu ni wako, Mola wangu nisikie,
Mola wangu nisamehe.

4 comments:

 1. Mungu wangu nisamehe,kwa mengi nayokosea,
  Mkonowo niwekee,mema nipate tambua,
  Na mabaya niepushe,mwana nilie potea,
  Mabaya sihesabie,mazuri zidi jalia.

  ReplyDelete
 2. Nanukuu "Mola wangu naja kwako, baraka unijalie,
  Niokoe mja wako, dunia 'sinizuzue,
  Na utukufu ni wako, Mola wangu nisikie,
  Mola wangu nisamehe." mwisho wa kunukuu. Nimepaenda hapa.

  Mungu wangu usiniti vishawishini,
  Maovuni uniokoe uniongoze na mazuri
  Na nakuomba uwabari watu wa dunia hii wote.

  ReplyDelete
 3. Kaka tupo pamoja, hapa huwa najifunza kiswahili cha kimwambao..
  Ahsante kwa mashairi murua

  ReplyDelete
 4. Nitanukuu:
  'Machafu mawazo yangu, na mengine ya moyoni,Husuda kwao wenzangu, ugomvi na majirani,Usin'ache peke yangu, nitaishia njiani,
  Mola wangu nisamehe.'
  Mwisho wa kunukuu...

  Nami nashuka ubeti wangu hapa.....

  Nimasafi mawazo yangu, na mengine ya moyoni, heshima kwao wenzangu, na upendo na majirani, kamwe hawatoniacha njiani, na mola wangu ananilinda, eee Mola wangu endelea kunilinda.....LOL

  nami nimo....

  ReplyDelete