Saturday, September 26, 2009

Mpenzi rudi hima

Kusubiri nimechoka, na muda wazidi kwenda,
Mwenzio nataabika, mwili wazidi kukonda,
Raha iliniponyoka, wewe mbali umekwenda,
Urudi basi mpenzi, nakungojea kwa hamu.

Nakungojea kwa hamu, siku utakayorudi,
Unipe mashamshamu, kwani u wangu waridi,
Mapenzi yako matamu, nipate kuyafaidi,
Kwani nimekuchagua, mwingine simtamani.

Mwingine simtamani, nd'o maana nakungoja,
U ndani mwangu moyoni, wewe pekee mmoja,
Wewe huna kifani, urudi tuwe pamoja,
Ona nachanganyikiwa, natamani kukuona.

Natamani kukuona, wewe unipaye raha,
Vinginevyo raha sina, nitakosa hata siha,
Juwa nakupenda sana, wewe u yangu furaha,
Mpenzi usikawie, bure nitamwaga chozi.

Bure nitamwaga chozi, kukuona nikikosa,
Peke yangu sijiwezi, penzi lako lanitesa,
Rudi wangu laazizi, unipaye mi' hamasa,
Nangoja leo na kesho, fanya urudi mapema.

Fanya urudi mapema, upweke wanielemea,
Jitahidi fanya hima, urudi kuniokoa,
Nisije kupata homa, na kuzidi kuumia,
Tabibu wangu ni wewe, rudi ili unitibu.

Rudi ili unitibu, maradhi ya moyo wangu,
Maradhi yan'onisibu, ni wewe mpenzi wangu,
Wewe u wangu muhibu, shahidi yangu ni Mungu,
Mpenzi usichelewe, homa itanizidia.

Homa itanizidia, endapo utachelewa,
Hivyo nakusubiria, raha nataka kupewa,
Useme nikasikia, kwamba hima utakuwa,
Umekuja kunitibu, kabla sijatibuka.

7 comments:

 1. Mmm kweli kupenda ni kidonda, Kipenda roha hula nyama mbichi haoni wala hasikii akipenda anapenda.

  Fadhy kuwa na subira na huyo umpendae atarudi tu. Pia je? mnawasiliana na anajua hili au anasema ujumbe wako kwani labda ingekuwa nafuu. Nakutakia kila la kheri umpate mpenzio.

  ReplyDelete
 2. Sinachakuongezea!

  Na sifichi, SHAIRI limenikuna .

  ReplyDelete
 3. Helo Fadhy!! Hiyo hamu ni ipi? Ya binamu kanyama ka hamu ama?

  Wahenga wanasema 'mkamia maji hayanwi'

  waweza kukamia saaana kumbe siku kapanda apolo kwenda kuvinjari, just in case ndo kanyama unakokawadhia...lol!

  ReplyDelete
 4. Kazi nzuri mkuu! Subira yavuta heri! Kuwa mwaminifu daima usikengeuke mzee; hatimaye wako atarudi.

  ReplyDelete
 5. Da Yasinta nimpendaye atarudi. Mawasiliano....nd'o silaha yetu. Namkumbusha tu kuwa asikawie kurudi.

  Mtakatifu Simon nashukuru sana kama umekunwa na tungo hii. Unajua nini kaka? Leo nimekaa na lindi la mawazo, nikimuwaza yeye aliye mbali.

  Chacha Wambura, karibu sana kibarazani kwangu. Nimeufurahia vilivyo ujio wako. Si hamu ya binamu nyama ya hamu. Na wala siyakamii maji. Ila ni hamu japo ya kumtia machoni ili walau nilione tabasamu lake mwanana. Hivyo sijakamia kanyama kake, bali uwepo wake!

  Mkuu Given, nashukuru sana kwa kunitembela na kuacha maoni. karibu tena na tena.

  Wadau wote nawashukuruni sana kwa kutonichoka. Karibuni zaidi na zaidi kibarazani hapa, mahali tunapojivunia utajiri wa ushairi wa lugha adhimu ya Kiswahili.

  Hayati Shaaban Robert, nguli wa ushairi wa Kiswahili alipata kuandika katika 'Kiswahili' Kitabu 'Pambo la Lugha' uk. 27:

  Titi la mama litamu, hata likiwa la mbwa,
  Kiswahili naazimu, sifayo inayofumbwa,
  Kwa wasiokufahamu, niimbe ilivyo kubwa,
  Toka kama chemchemu, furika palipozibwa,
  Titi la mama litamu, jingine halishi hamu.

  ReplyDelete
 6. Da! Mapenzi yahitaji kuvumiliana, subira na mambo kama hayo.Upendo wa dhati ndio wamfanya mtu kuhisi kupungukiwa na kitu pale mwenzi wake anapokuwa mbali.
  Twashukuru kwa ujumbe huu mzuri.

  ReplyDelete
 7. Halihalisi kwa wengine imekaa mkao wa:


  Mpenzi toa taarifa kabla hujarudi hima, usije ukafumania!:-(

  ReplyDelete