Friday, September 4, 2009

Huba

Nijaze mie mahaba,
Ili nile nikashiba,
Nipe mapenzi ya huba,
Nitosheke na dunia.

Nipe chakula kitamu,
Kinijaze mi’ wazimu,
Kinipandishe stimu,
Nibaki sikilizia.

Nigee mapenzi yote,
Yaniingie nidate,
Raha kamili nipate,
Raha isiyopungua.

Niambie wanipenda,
Siposema nitakonda,
Hata homa kunipanda,
Moyoni nikaumia.

Nifanye nifurahie,
Katu mi’ nisiumie,
Mapenzi nijivunie,
Na raha kujisikia.

Nipe mimi peke yangu,
Usimpe na mwenzangu,
Umeumbwa uwe wangu,
Mungu amenipatia.

Kunipenda usichoke,
Wanifanya niridhike,
Na moyo uburudike,
U wangu najivunia.

5 comments:

 1. Naamini kama bado hujaoa basi huyo wako yupo anakusubiri. Na naamini mtakuwa na maisha mazuri na atakupenda na utampenda na watoto mtazaa. Nakutakia yote mema. Ila namwonea wivu:-)

  ReplyDelete
 2. Ana heri mwandani wako! Hii ni kutokana na ukweli kwamba kizazi cha sasa watu wengi kuwa ndivyo sivyo.

  ReplyDelete
 3. Nimfurahia hapa...

  Nipe mimi peke yangu,
  Usimpe na mwenzangu,

  Kisha nikishetoka tu kwa Da Yasinta nakusoma kuhusu wanaume watanzania :-D
  Hata mie namuonea wivu!

  ReplyDelete
 4. Nipe mimi peke yangu,
  Usimpe na mwenzangu,

  Those two lines just standout on the poem. Nilifikiri nitasema kwanza lakini Serina alikuwa ashaona

  ReplyDelete
 5. Kauli hizo Mkuu!

  Lazima mtu aanze kuvuta majani na kujikanyaga, kama unastukia naongea nini:-)

  ReplyDelete