Wednesday, September 30, 2009

Mwisho wa mwezi

Mwisho wa mwezi ni mambo, tena kubwa burudani,
Mfukoni hakujambo, na raha hadi moyoni,
Pesa sabuni ya roho.

Pesa sabuni ya roho, nazo siku zimefika,
Pesa inao uroho, tamaaye kuzishika,
Tamu za mwisho wa mwezi.

Tamu za mwisho wa mwezi, kwani ushazisotea,
Umefanya sana kazi, hakiyo wakikugea,
Ifurahi familia.

Ifurahi familia, rudi nyumbani mapema,
Pesa ikikuzingua, kwenye shimo utazama,
Eti pesa ni shetani.

Eti pesa ni shetani, hasa ukishazipata,
Hulali hata nyumbani, matako kulia mbwata,
Mfalme ndiyo wewe.

Mfalme ndiyo wewe, na kizungu waongea,
Na hadhira usikiwe, na sifa kukutolea,
Huo ndo mwisho wa mwezi.

Huo ndo mwisho wa mwezi, wa mwingi umaridadi,
U chakari hujiwezi, kichwa maji kuzidi,
Akibayo kukauka.

Akibayo kukauka, hujali kuhusu kesho,
Wewe ni wa uhakika,
Mwezi ufikapo mwisho,
Mwisho wa mwezi ni raha.

Saturday, September 26, 2009

Mpenzi rudi hima

Kusubiri nimechoka, na muda wazidi kwenda,
Mwenzio nataabika, mwili wazidi kukonda,
Raha iliniponyoka, wewe mbali umekwenda,
Urudi basi mpenzi, nakungojea kwa hamu.

Nakungojea kwa hamu, siku utakayorudi,
Unipe mashamshamu, kwani u wangu waridi,
Mapenzi yako matamu, nipate kuyafaidi,
Kwani nimekuchagua, mwingine simtamani.

Mwingine simtamani, nd'o maana nakungoja,
U ndani mwangu moyoni, wewe pekee mmoja,
Wewe huna kifani, urudi tuwe pamoja,
Ona nachanganyikiwa, natamani kukuona.

Natamani kukuona, wewe unipaye raha,
Vinginevyo raha sina, nitakosa hata siha,
Juwa nakupenda sana, wewe u yangu furaha,
Mpenzi usikawie, bure nitamwaga chozi.

Bure nitamwaga chozi, kukuona nikikosa,
Peke yangu sijiwezi, penzi lako lanitesa,
Rudi wangu laazizi, unipaye mi' hamasa,
Nangoja leo na kesho, fanya urudi mapema.

Fanya urudi mapema, upweke wanielemea,
Jitahidi fanya hima, urudi kuniokoa,
Nisije kupata homa, na kuzidi kuumia,
Tabibu wangu ni wewe, rudi ili unitibu.

Rudi ili unitibu, maradhi ya moyo wangu,
Maradhi yan'onisibu, ni wewe mpenzi wangu,
Wewe u wangu muhibu, shahidi yangu ni Mungu,
Mpenzi usichelewe, homa itanizidia.

Homa itanizidia, endapo utachelewa,
Hivyo nakusubiria, raha nataka kupewa,
Useme nikasikia, kwamba hima utakuwa,
Umekuja kunitibu, kabla sijatibuka.

Sunday, September 20, 2009

Utu wema

Ndiyo haswa sifa yako,
Iliyo moyoni mwako,
Wema kwa rafiki zako,
Mola amekujalia.

Wema wako wa moyoni,
Ni kitu chenye thamani,
Mwinginewe hafanani,
Hakika najivunia.

Wema wako wenye dhati,
Usiojali wakati,
Wema mwingi kibati,
Yeyote kufurahia.

Roho yenye utajiri,
Nzuri kushinda johari,
Kuwa nawe ni fahari,
Kwa maisha ya dunia.

Umepewa utu wema,
Wenye thamani daima,
Moyo wangu wanituma,
Sifazo kukupatia.

Kwa Mola nakuombea,
Azidi kukupatia,
Heri na fanaka pia,
Katika hii dunia.

Thursday, September 17, 2009

Mola wangu nisamehe

Mola unayenipenda, unipaye afya njema,
Mlinzi ninapokwenda, wanijalia uzima,
Kwa dhambi ninazotenda, unionee huruma,
Mola wangu unisamehe.

Matendo yangu mabaya, tena yenye kuchukiza,
Nitendayo bila haya, wengine kuwaumiza,
Kwa kila lililo baya, na bado nikajikweza,
Mola wangu nisamehe.

Niyatendayo sirini, najidanganya mwenyewe,
Japo watu hawaoni, lakini waona wewe,
Nisipoteze imani, naomba nikombolewe,
Mola wangu nisamehe.

Machafu mawazo yangu, na mengine ya moyoni,
Husuda kwao wenzangu, ugomvi na majirani,
Usin'ache peke yangu, nitaishia njiani,
Mola wangu nisamehe.

Maneno yangu machafu, maneno yenye kuudhi,
Mimi si mkamilifu, sipendi nikose radhi,
Siitaki tena hofu, dhambi isiwe maradhi,
Mola wangu nisamehe.

Mola wangu naja kwako, baraka unijalie,
Niokoe mja wako, dunia 'sinizuzue,
Na utukufu ni wako, Mola wangu nisikie,
Mola wangu nisamehe.

Thursday, September 10, 2009

Usichoke

Maisha ni kama vita, usichoke kupigana,
Hata kama ukigota, endelea kupambana,
Bado muda wa kutweta, bado ni mapema sana,
Usichoke mwanakwetu.

Nenda shule ukasome, uongeze maarifa,
Ukiwa huko jitume, uliinue taifa,
Nenda kakazane shime, utajipatia sifa,
Usichoke mwanakwetu.

Amka wahi kazini, ili uongeze tija,
Ujuzi wako kichwani, taifa linaungoja,
Ujitume ofisini, na wenzako kwa pamoja,
Usichoke mwanakwetu.

Pigana pasi kuchoka, yapiganie maisha,
Jitihada zako weka, ustawi kufanikisha,
Kwa dhamira ya hakika, malengo kufanikisha,
Usichoke mwanakwetu.

Mwiko kukata tamaa, bado ni ndefu safari,
Kurudi nyuma kataa, pambana nazo hatari,
Tumia kila wasaa, maisha kutafakari,
Usichoke mwanakwetu.

Usifanye masikhara, maisha hayendi hivyo,
Kwa hiyo kuwa imara, vile iwezekanavyo,
Nawe utazidi ng'ara, namna itakiwavyo,
Usichoke mwanakwetu.

Friday, September 4, 2009

Huba

Nijaze mie mahaba,
Ili nile nikashiba,
Nipe mapenzi ya huba,
Nitosheke na dunia.

Nipe chakula kitamu,
Kinijaze mi’ wazimu,
Kinipandishe stimu,
Nibaki sikilizia.

Nigee mapenzi yote,
Yaniingie nidate,
Raha kamili nipate,
Raha isiyopungua.

Niambie wanipenda,
Siposema nitakonda,
Hata homa kunipanda,
Moyoni nikaumia.

Nifanye nifurahie,
Katu mi’ nisiumie,
Mapenzi nijivunie,
Na raha kujisikia.

Nipe mimi peke yangu,
Usimpe na mwenzangu,
Umeumbwa uwe wangu,
Mungu amenipatia.

Kunipenda usichoke,
Wanifanya niridhike,
Na moyo uburudike,
U wangu najivunia.

Tuesday, September 1, 2009

Mlevi na Falsafa yake

Kwamba asiyejua,
Na hajui kwamba hajui
Ndiye mwerevu zaidi,
Hapa duniani,
Wataka kushangaa?

Bora asiyejua,
Na anajua kwamba hajui,
Kwani tungesemaje?
Ilhali wengine,
Wametuvisha vidoto!

Wasomi na wanasayansi,
Nd'o walogeuka,
Wamekuwa wanasiasa
Sasa wameshatonoka
Wakukumbuke wewe,
Kwa lipi hasa
Ulilonalo?

Maana ya maneno:
Vidoto - vipande vya nguo maalumu wafungwavyo ngamia machoni wasafiripo jangwani.
Tonoka - kuwa na hali nzuri kwa sababu ya mafanikio fulani.