Saturday, August 8, 2009

Tujisahihishe

Leo nimeyakumbuka, kabla jua kuzama,
Maana yametufika, tulishindwa kuyapima,
Jambo ninalolitaka, tuseme tangu mapema.

Pale tulipokosea, wakati uliopita,
Ni dhambi tukirudia, hatutoacha kujuta,
Lazima tuweke nia, vinginevyo tutasota.

Tumechoka bla bla, twataka kuona kazi,
Tuwakatae kabla, wale kazi hawawezi,
Twahitaji mbadala, tufute yetu machozi.

Tumewapa madaraka, wamefanya ufisadi,
Tamaa imewashika, imewapa ukaidi,
Wanajua twateseka, wanafanya makusudi.

Hizo kofia na kanga, wala visiturubuni,
Vinatujaza ujinga, kutufanya masikini,
Tunapaswa kuvipinga, akili iwe vichwani.

Tusidanganyike tena, kosa siyo mara mbili,
Rushwa tuseme hapana, tuchague kwa akili,
Ya uchaguzi wa jana, leo yametukatili.

Sauti ninaipaza, uliko ikufikie,
Napenda kukukataza, makosa usirudie,
Ukirudia teleza, lazima uijutie.

Kalamu naweka chini, yangu nimeshayasema,
Uyaweke akilini, fikiri na kuyapima,
Piga hatua fulani, uchague kwa hekima.

5 comments:

 1. Hongera mkuu kwa shairi zuri lenye ujumbe kama waraka wa "WAKATORIKI!

  ReplyDelete
 2. Ujumbe mzuri sana. Shida yetu sote ni kuwafikia walengwa tunaojaribu kuwapigania.

  ReplyDelete
 3. Ahsanteni sana wadau, mkuu Given (miaka mingi sana pamoja), mkuu Masangu, dada Yasinta na mkuu Chib.

  Nawashukuruni sana kwa kuwa bega kwa bega nami katika hizi harakati za kuizindua jamii yetu.

  ReplyDelete