Saturday, August 22, 2009

Mola tuongoze

Dunia tambara bovu, wahenga walishanena,
Yataka uvumilivu, na kukuomba Rabana,
Dunia mti mkavu, majaribu mengi sana,
Mola utuongoze.

Dunia hii hadaa, huhadaa ulimwengu,
Hata kwa walo shujaa, huonja yake machungu,
Ulaghai umejaa, kwenye hayo malimwengu,
Mola utuongoze.

Tukiwa sisi pekee, hatutoweza kushinda,
Hivyo utusimamie, mambo yasije kupinda,
Ili mbele twendelee, tuponye vyetu vidonda,
Mola utuongoze.

Tupe mioyo misafi, tusiwe na majivuno,
Tuondolee ulafi, hata panapo vinono,
Imani iwapo safi, twalitimiza agano,
Mola utuongoze.

Twepushie ufitini, majungu tusiabudu,
Tushibe njema imani, tusiwe wala vibudu,
Chuki isiwe myoyoni, wala kupenda ghadhabu,
Mola utuongoze.

Mali zisitulaghai, tukajawa na kiburi,
Tukakwona haufai, tukajawa ufahari,
Tupe yalo anuai, tujifunze kufikiri,
Mola utuongoze.

Mola utuongoze, wewe utusimamie,
Twataka tusiteleze, wewe utupiganie,
Mola utuelekeze, na tukutumainie,
Mola utuongoze.

4 comments:

 1. Mola tuongoze safi sana shairi nzuri sana ni vema kumwomba Mola.

  ReplyDelete
 2. Mola ndo kila kitu! Hongera mkuu shairi lako zuri sana.

  ReplyDelete
 3. Mola tupe uelekeo,mawio hata machweo,
  usitutupe na mkono,daima pote tuwapo,
  twahitaji wako mwongozo,kwa yote tuyafanyayo.

  ReplyDelete
 4. Eee Mola tuongoze!

  Hivi na wezi ni Ruksa kuomba mola waibe mswano?Maana nahisi awaongozaye anawasaidia kweli katika muongozo maeneo fulani au hata Bongo!:-(

  ReplyDelete