Monday, August 3, 2009

Mbali nawe

Jua linapochomoza, kila siku asubuhi,
Hunifanya kukuwaza, unipae kufurahi,
Maneno nayokweleza, ni ukweli si kebehi,
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisokipenda.

Wewe u sehemu yangu, nuru yangu maishani,
Nilopewa na Mungu, niwe nayo duniani,
Nitayaonja machungu, kama 'tanipiga chini,
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisokipenda.

Daima uwapo mbali, hata ni kwa siku moja,
Nitakesha mi' silali, nikeshe nikikungoja,
Tukae sote wawili, tufurahi kwa pamoja,
Kuwa mbali na wewe, ni kitu nisokipenda.

Huhisi nina adhabu, napokuwa mbali nawe,
Maisha kuniadhibu, hadi nichanganyikiwe,
Wewe nd'o wangu muhibu, sina tena mwinginewe,
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisokipenda.

Nakuwa mi' na upweke, nazo karaha moyoni,
Nayo maji yasishuke, niyanywapo mdomoni,
Yanifanya nita'bike, nijawe nayo huzuni,
Kuwa mbali na wewe, ni kitu nisokipenda.

Nakosa mie furaha, nakumbwa nao unyonge,
Maisha yawa karaha, kunifanya nisiringe,
Wala sifanyi mzaha, nisemayo 'siyapinge,
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisokipenda.

Sogea kwangu karibu, e pambo la wangu moyo,
Pendo 'silolihesabu, amini niyasemayo,
Ya moyo wangu dhahabu, unipaye pasi choyo,
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisokipenda.

7 comments:

 1. kweli kupenda ni kama kidonda
  na kweli kupenda ni gharama
  na inauma sana kama umendaye yupo mbali, Roho inauma na mateso yanakuwepo.

  ReplyDelete
 2. Sikatai kupenda lkn wengine huumiza! Ni heri kujipenda kwanza ili moyoni usiumie! Mungu awabariki sana muwe na nia moja daima; kazi nzuri mzee.

  ReplyDelete
 3. KUISHI MBALI MUHALI, BALI IWE KULIHALI,KWA MAISHA KUTAFAKARI IWE MMOJA AU WAWILI MUHIMU KUOMBA JALALI, KUWA MPWEKE IDHILALI

  ReplyDelete
 4. Pole sana kaka Fadhy,wa ubani kuwa mbali,
  Mbona huo mtihani,huna budi kukabili,
  Uvumilivu yabidi,atarudi usijali.

  ReplyDelete
 5. Ahsanteni sana wadau,
  Kamwe hamnisahau.

  ReplyDelete