Tuesday, August 25, 2009

Hongera Mubelwa Bandio

Nimeisikia mbiu, alfajiri imelia,
Ili tusijisahau, maisha kupigania,
Ili nasi angalau, mahali tukafikia,
Nakupa zangu pongezi, kaka Mubelwa Bandio.

Mwaka sasa umekwisha, unaandika huchoki,
Wajua haya maisha, hujaa mingi mikiki,
Wengine kuelimisha, ni jambo la kirafiki,
Nakupa zangu pongezi, kaka Mubelwa Bandio.

Upo kwenye mapambano, ujenzi walo taifa,
Hujalala kama pono, wastahili nyingi sifa,
Washika yetu mikono, ili tuzizibe nyufa,
Nakupa zangu pongezi, kaka Mubelwa Bandio.

Mubelwa bado kuchoka, upo kwenye msafara,
Ungali kwenye pilika, kwa zako huru fikra,
Nakuombea baraka, uzidi kuwa imara,
Nakupa zangu pongezi, kaka Mubelwa Bandio.

Ingawa ni mwaka 'moja, umefanya kazi nzuri,
Umejenga vema hoja, umetupa kufikiri,
Umedumisha umoja, umetupa umahiri,
Nakupa zangu pongezi, kaka Mubelwa Bandio.

Niliwahi kuandika, MZEE WA CHANGAMOTO,
Kutwambia hajachoka, mambo yalo motomoto,
Miziki ya uhakika, yenye midundo mizito,
Nakupa zangu pongezi, kaka Mubelwa Bandio.

Nakuombea kwa Mungu, uwe na afya imara,
Kwenye haya malimwengu, akwepushie papara,
Uepushiwe kiwingu, nyota izidi kung'ara,
Nakupa zangu pongezi, kaka Mubelwa Bandio.

Mubelwa mwendo ukaze, usiache harakati,
Mawazo uyaeleze, tena kwa kila wakati,
Ili nasi tujifunze, nawe uwe katikati,
Nakupa zangu pongezi, kaka Mubelwa Bandio.

Na wanablog wote, siachi kuwapongeza,
Heri nyingi mzipate, Mola atawaongoza,
Mlipo pale popote, mengi sana mwatufunza,
Nakupa zangu pongezi, kaka Mubelwa Bandio.

Namaliza kaditama, Mubelwa hongera sana,
Ujaliwe yalo mema, usiku nao mchana,
U rafiki yetu mwema, nasi twakupenda sana,
Nakupa zangu pongezi, kaka Mubelwa Bandio.

4 comments:

 1. Nami nakupongeza, kwa kutimiza mwaka,
  Hongera Mubelwa, kwa kazi ulofanya,
  Umeonyesha, ya kuwa u rafiki mwema,
  MUngu akupe nguvu, ili uzidi kutupa mengi

  ReplyDelete
 2. Dah!! Sijui niseme nini!!!!
  Mother Theresa alisema "I CAN DO NO GREAT THINGS, ONLY SMALL ONE WITH GREAT LOVE" na naomba niwahahakishie kuwa NATHAMINI SAAANA ZAWADI HII KUBWA KULIKO mliyonipatia. Kushirikiana nanyi ni zaidi ya uwezo wa kuandika na kwa hakika ninajivunia kuwafahamu. Ninajifunza na kwa kuwa nina hakika kuwa mko pamoja nami (ama niseme mu-ngao yangu) nazidi kusonga mbele, kifua mbele na maslahi ya wote mbele nikiamini kuwa JESHI LETU LA WACHACHE LENYE KUPIGANIA HAKI laelekea kushinda.
  Nisingekuwa nilivyo bila ninyi na NAWASHUKURU NA KUWATHAMINI SAAAAAANA

  ReplyDelete
 3. Haya Mzee wa mashairi, Umemkuna sana Mzee wa Changamoto

  ReplyDelete
 4. Höngera sana kaka. Ingawa nina miaka miwili unusu nikiblog, nimejifunza mengi sana kwako.
  Kaka Chib, wacha leo Mutiba akenue hadi gego la mwisho.
  Nasi tukenue, maana tupo kwenye harakati.
  Da Yasinta, ahsante sana kwa kutochoka kwako kunitembelea.

  Sana tu, leo na kesho!

  ReplyDelete