Wednesday, August 26, 2009

Falsafa ya Mlevi I

Na Dkt. Masangu Matondo Nzuzullima


Walimwengu wanasema:
Kuna kujua
Na kujua kwamba unajua
Pia kuna kujua
Na kutojua kwamba unajua
Lakini pia kuna kutojua
Na kujua kwamba hujui
Pia kuna kutojua
Na kutojua kwamba hujui

Walimwengu pia wanasema:
Mtu anayejua
Na kujua kwamba anajua
Yeye ni mwerevu na msomi
Na mtu anayejua
Lakini hajui kwamba anajua
Yeye ni mdadisi na mgunduzi
Mtu asiyejua
Na anajua kwamba hajui
Yeye ni mwanafunzi
Lakini mtu asiyejua
Na hajui kwamba hajui
Yeye ni mpumbavu!

Mimi mlevi ninasema:
Yote haya ni uwongo na uzushi
Mtu anayejua
Na kujua kwamba anajua
Yeye ni mpumbavu!
Kwani wasomi, wanasayansi na wanasiasa
Hawakugeuka Mashing’weng’we,
Na kutufikisha Pagak?

Mimi mlevi nasisitiza
Mtu pekee mwerevu hapa duniani
Ni mtu asiyejua
Na hajui kwamba hajui!

Maneno Magumu:

Mashing’weng’we - mazimwi yalayo watu katika hadithi za Kisukuma
Pagak - kutoka katika kitabu cha Wimbo wa Lawino kilichoandikwa na Okot p'Bitek. Ni mahali ambako mtu akienda harudi yaani kuzimuni.

(c) Dr. Masangu Matondo Nzuzullima

Ahsante sana Prof. Matondo Nzuzullima kwa shairi hili.

5 comments:

 1. Shairi la leo kali: mi sijui kama najua:-)

  ReplyDelete
 2. Ahsante sana Prof Matondo kwa shairi hili. Kweli umenipa kazi ya kufikiri sana, hatimaye nami nimekuandikia 'Mlevi na Falsafa yake.'
  Pia ahsanteni sana Mtakatifu Simon a.k.a Simioni na Sista Yasinta kwa kutochoka klunitembelea.

  ReplyDelete
 3. Asante sana Bwana Fadhili kwa kukubali kuliweka shairi hilo jamvini kwako. Ni uungwana wa hali ya juu. Ninayo mashairi mengi ambayo nilikuwa nayaandika wakati ule nikiwa JKT. Baada ya misukosuko ya ukuruta nilikuwa na tabia ya kujongomea na kwenda kujipumzisha porini katika pori la Makutupora. Ninayo mengi sana na nimeanza kuyahariri ili niyachapishe. Unao mpango wa kuchapisha hii Diwani yako siku moja? Ni mashairi mazuri sana! Endelea usichoke.

  ReplyDelete
 4. Prof Matondo, napenda kukushukuru sana kwa kuwa mmoja wa wanaothamini sana kipaji changu.
  Pia nimefurahi sana kwa kuweza kubadilishana mawazo nami kwa njia ya ushairi. Naomba usisite kunitumia tena na tena tungo zako zenye umahiri wa uandikaji.
  Nakusudia, siku moja niichape Diwani yangu ili kufikisha mawazo yangu kwa jamii isiyopata nafasi ya kuyasoma mtandaoni.
  Siku zote nimekuwa na ndoto za kufanya hivyo, naamini nitafanya 'siku moja.'
  Karibu tena na tena kibarazani kwangu.

  ReplyDelete