Sunday, August 16, 2009

Ahsante sana rafiki

Ahsante sana rafiki, nakuombea kwa Mungu,
Kwenye raha kwenye dhiki, ungali rafiki yangu,
Ubarikiwe.

Rafiki yangu u mwema, tena u mwenye kujali,
Watowa bila kupima, wema bila ubahili,
Uzidishiwe.

Rafiki wanithamini, shida zangu wazijua,
Unanipenda moyoni, kwa pendo linalokua,
Uongezewe.

Rafiki u mfariji, wa muhimu maishani,
Wayajua mahitaji, wajua ufanye nini,
Ubarikiwe.

Rafiki najivunia, zawadi yangu spesho,
Wewe nakufurahia, leo hii hata kesho,
Uzidishiwe.

Rafiki yangu ahsante, sinalo neno zaidi,
Baraka tele upate, mafanikio yazidi,
Uongezewe.

Ahsante sana rafiki.

2 comments:

  1. Inaonyesha huyu rafiki kakutendea jambo jema kweli. Natamani ningekuwa rafiki yako nami nitungiwe shairi kama hili:-)

    ReplyDelete