Wednesday, August 26, 2009

Falsafa ya Mlevi I

Na Dkt. Masangu Matondo Nzuzullima


Walimwengu wanasema:
Kuna kujua
Na kujua kwamba unajua
Pia kuna kujua
Na kutojua kwamba unajua
Lakini pia kuna kutojua
Na kujua kwamba hujui
Pia kuna kutojua
Na kutojua kwamba hujui

Walimwengu pia wanasema:
Mtu anayejua
Na kujua kwamba anajua
Yeye ni mwerevu na msomi
Na mtu anayejua
Lakini hajui kwamba anajua
Yeye ni mdadisi na mgunduzi
Mtu asiyejua
Na anajua kwamba hajui
Yeye ni mwanafunzi
Lakini mtu asiyejua
Na hajui kwamba hajui
Yeye ni mpumbavu!

Mimi mlevi ninasema:
Yote haya ni uwongo na uzushi
Mtu anayejua
Na kujua kwamba anajua
Yeye ni mpumbavu!
Kwani wasomi, wanasayansi na wanasiasa
Hawakugeuka Mashing’weng’we,
Na kutufikisha Pagak?

Mimi mlevi nasisitiza
Mtu pekee mwerevu hapa duniani
Ni mtu asiyejua
Na hajui kwamba hajui!

Maneno Magumu:

Mashing’weng’we - mazimwi yalayo watu katika hadithi za Kisukuma
Pagak - kutoka katika kitabu cha Wimbo wa Lawino kilichoandikwa na Okot p'Bitek. Ni mahali ambako mtu akienda harudi yaani kuzimuni.

(c) Dr. Masangu Matondo Nzuzullima

Ahsante sana Prof. Matondo Nzuzullima kwa shairi hili.

Tuesday, August 25, 2009

Hongera Mubelwa Bandio

Nimeisikia mbiu, alfajiri imelia,
Ili tusijisahau, maisha kupigania,
Ili nasi angalau, mahali tukafikia,
Nakupa zangu pongezi, kaka Mubelwa Bandio.

Mwaka sasa umekwisha, unaandika huchoki,
Wajua haya maisha, hujaa mingi mikiki,
Wengine kuelimisha, ni jambo la kirafiki,
Nakupa zangu pongezi, kaka Mubelwa Bandio.

Upo kwenye mapambano, ujenzi walo taifa,
Hujalala kama pono, wastahili nyingi sifa,
Washika yetu mikono, ili tuzizibe nyufa,
Nakupa zangu pongezi, kaka Mubelwa Bandio.

Mubelwa bado kuchoka, upo kwenye msafara,
Ungali kwenye pilika, kwa zako huru fikra,
Nakuombea baraka, uzidi kuwa imara,
Nakupa zangu pongezi, kaka Mubelwa Bandio.

Ingawa ni mwaka 'moja, umefanya kazi nzuri,
Umejenga vema hoja, umetupa kufikiri,
Umedumisha umoja, umetupa umahiri,
Nakupa zangu pongezi, kaka Mubelwa Bandio.

Niliwahi kuandika, MZEE WA CHANGAMOTO,
Kutwambia hajachoka, mambo yalo motomoto,
Miziki ya uhakika, yenye midundo mizito,
Nakupa zangu pongezi, kaka Mubelwa Bandio.

Nakuombea kwa Mungu, uwe na afya imara,
Kwenye haya malimwengu, akwepushie papara,
Uepushiwe kiwingu, nyota izidi kung'ara,
Nakupa zangu pongezi, kaka Mubelwa Bandio.

Mubelwa mwendo ukaze, usiache harakati,
Mawazo uyaeleze, tena kwa kila wakati,
Ili nasi tujifunze, nawe uwe katikati,
Nakupa zangu pongezi, kaka Mubelwa Bandio.

Na wanablog wote, siachi kuwapongeza,
Heri nyingi mzipate, Mola atawaongoza,
Mlipo pale popote, mengi sana mwatufunza,
Nakupa zangu pongezi, kaka Mubelwa Bandio.

Namaliza kaditama, Mubelwa hongera sana,
Ujaliwe yalo mema, usiku nao mchana,
U rafiki yetu mwema, nasi twakupenda sana,
Nakupa zangu pongezi, kaka Mubelwa Bandio.

Saturday, August 22, 2009

Mola tuongoze

Dunia tambara bovu, wahenga walishanena,
Yataka uvumilivu, na kukuomba Rabana,
Dunia mti mkavu, majaribu mengi sana,
Mola utuongoze.

Dunia hii hadaa, huhadaa ulimwengu,
Hata kwa walo shujaa, huonja yake machungu,
Ulaghai umejaa, kwenye hayo malimwengu,
Mola utuongoze.

Tukiwa sisi pekee, hatutoweza kushinda,
Hivyo utusimamie, mambo yasije kupinda,
Ili mbele twendelee, tuponye vyetu vidonda,
Mola utuongoze.

Tupe mioyo misafi, tusiwe na majivuno,
Tuondolee ulafi, hata panapo vinono,
Imani iwapo safi, twalitimiza agano,
Mola utuongoze.

Twepushie ufitini, majungu tusiabudu,
Tushibe njema imani, tusiwe wala vibudu,
Chuki isiwe myoyoni, wala kupenda ghadhabu,
Mola utuongoze.

Mali zisitulaghai, tukajawa na kiburi,
Tukakwona haufai, tukajawa ufahari,
Tupe yalo anuai, tujifunze kufikiri,
Mola utuongoze.

Mola utuongoze, wewe utusimamie,
Twataka tusiteleze, wewe utupiganie,
Mola utuelekeze, na tukutumainie,
Mola utuongoze.

Tuesday, August 18, 2009

Haya sasa

Mpira uliochezwa, umefika ukingoni,
Mpira umemalizwa, dakika zake tisini,
Kwa wale waliolizwa, warudi tu majumbani,
Maana imeshaelezwa, upinge wewe ni nani?
Kazi sasa imekwisha, twendelee na mengine.

Na refa ndiye mwamuzi, akisema imetoka,
Kama kamaliza kazi, kwamba ana uhakika,
Hajui yako majonzi, hajui wahuzunika,
La kufanya huliwezi, ni lazima kuridhika?
Kwani dua lake kuku, halitompata mwewe!

Sunday, August 16, 2009

Ahsante sana rafiki

Ahsante sana rafiki, nakuombea kwa Mungu,
Kwenye raha kwenye dhiki, ungali rafiki yangu,
Ubarikiwe.

Rafiki yangu u mwema, tena u mwenye kujali,
Watowa bila kupima, wema bila ubahili,
Uzidishiwe.

Rafiki wanithamini, shida zangu wazijua,
Unanipenda moyoni, kwa pendo linalokua,
Uongezewe.

Rafiki u mfariji, wa muhimu maishani,
Wayajua mahitaji, wajua ufanye nini,
Ubarikiwe.

Rafiki najivunia, zawadi yangu spesho,
Wewe nakufurahia, leo hii hata kesho,
Uzidishiwe.

Rafiki yangu ahsante, sinalo neno zaidi,
Baraka tele upate, mafanikio yazidi,
Uongezewe.

Ahsante sana rafiki.

Tuesday, August 11, 2009

Heri umoja

Naliandika shairi, kwa vyama vya upinzani,
Viongozi wafikiri, wafikiri kwa makini,
Maana mambo si shwari, mageuzi hatuoni,
Wakati umeshafika, twataka mabadiliko.

Wenyewe mkilumbana, mshindwe kuwa wamoja,
Watawala hukazana, kuziuwa zenu hoja,
Mnapaswa kupambana, tumeshachoka kungoja,
Twataka mbadilike, yawe mageuzi kweli.

Zilizopita chaguzi, kushinda hamkuweza,
Twalaumu viongozi, kote walikoteleza,
Tatizo lingali wazi, umoja mwatelekeza,
Ni ngumu ninyi kushinda, msipotaka umoja.

Umoja huleta nguvu, hivyo nanyi unganeni,
Msioneane wivu, haya mambo jifunzeni,
Maana ni upumbavu, mnazidi shuka chini,
Umoja wawezekana, mkiwa na nia moja.

Kwa kila mtu na lwake, mtazidi kuchemsha,
Vema jambo lifanyike, vinginevyo mtakesha,
Na mwakani muanguke, kwa anguko la kutisha,
Hima amkeni sasa, wakati hausubiri.

Wala kura siyo chache, ila mwagawana mno,
Ubinafsi muache, na mshikane mikono,
Na hilo tusiwafiche, ushindi huwa mnono,
Si ndoto za alinacha, amkeni usingizini.

Wananchi wawapenda, ila hawana imani,
Vyamani mnavurunda, niaje madarakani?
Kama mwataka kushinda, basi hebu unganeni,
Nasi tutawapa kura, mtashinda kwa kishindo.

Nyote mwataka gombea, dunia hay'endi hivyo,
Umoja mkiwekea, kama sisi tutakavyo,
Kura tutawapatia, vyovyote vile iwavyo,
Hima ninatowa wito, wapinzani unganeni.

Mjuwe chama tawala, hakilali usingizi,
Vipi ninyi mnalala, mmeshamaliza kazi?
Mtazishindaje hila, umoja hamuuwezi?
Mtazidi kuchemsha, kama msipoungana.

Kaditama nimefika, ni beti kumi kwa leo,
Ujumbe niloandika, ubadili mwelekeo,
Ili hatamu kushika, yahitajika upeo,
Umoja ndiyo silaha, kwani umoja ni nguvu.

Saturday, August 8, 2009

Tujisahihishe

Leo nimeyakumbuka, kabla jua kuzama,
Maana yametufika, tulishindwa kuyapima,
Jambo ninalolitaka, tuseme tangu mapema.

Pale tulipokosea, wakati uliopita,
Ni dhambi tukirudia, hatutoacha kujuta,
Lazima tuweke nia, vinginevyo tutasota.

Tumechoka bla bla, twataka kuona kazi,
Tuwakatae kabla, wale kazi hawawezi,
Twahitaji mbadala, tufute yetu machozi.

Tumewapa madaraka, wamefanya ufisadi,
Tamaa imewashika, imewapa ukaidi,
Wanajua twateseka, wanafanya makusudi.

Hizo kofia na kanga, wala visiturubuni,
Vinatujaza ujinga, kutufanya masikini,
Tunapaswa kuvipinga, akili iwe vichwani.

Tusidanganyike tena, kosa siyo mara mbili,
Rushwa tuseme hapana, tuchague kwa akili,
Ya uchaguzi wa jana, leo yametukatili.

Sauti ninaipaza, uliko ikufikie,
Napenda kukukataza, makosa usirudie,
Ukirudia teleza, lazima uijutie.

Kalamu naweka chini, yangu nimeshayasema,
Uyaweke akilini, fikiri na kuyapima,
Piga hatua fulani, uchague kwa hekima.

Monday, August 3, 2009

Mbali nawe

Jua linapochomoza, kila siku asubuhi,
Hunifanya kukuwaza, unipae kufurahi,
Maneno nayokweleza, ni ukweli si kebehi,
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisokipenda.

Wewe u sehemu yangu, nuru yangu maishani,
Nilopewa na Mungu, niwe nayo duniani,
Nitayaonja machungu, kama 'tanipiga chini,
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisokipenda.

Daima uwapo mbali, hata ni kwa siku moja,
Nitakesha mi' silali, nikeshe nikikungoja,
Tukae sote wawili, tufurahi kwa pamoja,
Kuwa mbali na wewe, ni kitu nisokipenda.

Huhisi nina adhabu, napokuwa mbali nawe,
Maisha kuniadhibu, hadi nichanganyikiwe,
Wewe nd'o wangu muhibu, sina tena mwinginewe,
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisokipenda.

Nakuwa mi' na upweke, nazo karaha moyoni,
Nayo maji yasishuke, niyanywapo mdomoni,
Yanifanya nita'bike, nijawe nayo huzuni,
Kuwa mbali na wewe, ni kitu nisokipenda.

Nakosa mie furaha, nakumbwa nao unyonge,
Maisha yawa karaha, kunifanya nisiringe,
Wala sifanyi mzaha, nisemayo 'siyapinge,
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisokipenda.

Sogea kwangu karibu, e pambo la wangu moyo,
Pendo 'silolihesabu, amini niyasemayo,
Ya moyo wangu dhahabu, unipaye pasi choyo,
Kuishi mbali na wewe, ni kitu nisokipenda.