Sunday, July 26, 2009

Wana kosa gani?

Mola nipe ujasiri, jambo nataka kusema,
Kwa waso na roho nzuri, waliokosa huruma,
Ambao hujidhihiri, kwa huo wao unyama,
Mbona mwatupa watoto, kwani wana kosa gani?

Zenu wenyewe anasa, mwafanya mwafurahia,
Mimba mnapozinasa, kwanini mwazichukia?
Kama mngeumbwa tasa, lawama mngezitoa,
Mbona mwatupa watoto, kwani wana kosa gani?

Wao wana kosa gani, kwanini mnawatupa?
Mnawatupa vyooni, wengine kwenye mapipa,
Kama hamwezi thamini, basi mimba mngekwepa,
Mbona mwatupa watoto, kwani wana kosa gani?

Kwani hamwoni uchungu, ama huruma myoyoni?
Mnamkosea Mungu, mwajiweka nuksani,
Yaacheni malimwengu, zishikeni zenu dini,
Mbona mwatupa watoto, kwani wana kosa gani?

Watoto ni malaika, shukuruni kuwazaa,
Msiwape kuteseka, wala mkawakataa,
Watoto ndiyo baraka, kwanini mwajihadaa?
Mbona mwatupa watoto, kwani wana kosa gani?

Nawanyoshea vidole, tabia hiyo muache,
Nawapigia kelele, watoto msiwakache,
Wewe pamoja na yule, watoto msiwafiche,
Mbona mwatupa watoto, kwani wana kosa gani?

6 comments:

 1. Ahsante kwa kulisema hili ni kweli siku hizi kumekuwa na mtindi huu kuzaa na kutupa kwa nini usiwaza kwanza kabla hujashika mimba. Kuliko kutopa roho. Inasikitisha sana na Asante sana kwa somo hili.

  ReplyDelete
 2. Wow!! Shule kamili yenye kufunza na kukumbukika.
  Asante saana Kaka.
  Bless

  ReplyDelete
 3. Asante kwa kutoifumbia macho jamii yetu kwa maovu yanayotia aibu!

  ReplyDelete
 4. Ingekuwa bomba la shule aliyewahi kutupa mtoto angeelezea jinsi gani hilo lilikuwa suluhisho hata kama angefanya hivyo bila kututajia jina lake:-(

  ReplyDelete
 5. Huruma kweli vichanga,hatia iso na kinga.
  Watoto pasi kupanga,acheni huo ujinga.
  Maisha yote ya ndenga,mawazo hutayashinda.
  Damu ile ya kichanga,daima itakuwinda.

  ReplyDelete
 6. Ahsante wadau kwa kulisemea hili. Nimekutana na kisa hivi karibuni, binti wa shule alitupa mtoto.
  Binti huyo alipata mimba na kuficha wazazi wake, sijui hata alifanikiwaje.
  Alijifungua mtoto wa kiume na kumtelekeza kituo cha treni huko Morogoro. Twamshukuru Mungu hatimaye alikamatwa. Adhabu yoyote ambayo ameipata, iwe fundisho kwake yeye na kwa wengine.

  ReplyDelete