Monday, July 13, 2009

Uwongo

Nafunga vema anjali, niombe ardhilhali,
Sitaki kuwa anzali, kwa kutokuwa mkweli,
Sikia kote mahali, niyasemayo Fadhili,
Uwongo una karaha, hukupa wewe utumwa.

Uulizwapo maswali, mada usiihawili,
Kujitia ujahili, uwongo kuwa injili,
Jifunze toka awali, siwadanganye ayali,
Uwongo una karaha, hukupa wewe utumwa.

Usiende fulifuli, kuilazimisha hali,
Ili watu wakubali, maneno yaso adili,
Uwongo una fidhuli, hali hauibadili,
Uwongo una karaha, hukupa wewe utumwa.

Mwiko japo desimali, uwongo kuufaili,
Usiuvike mtali, ama kuwasha kandili,
Utashindwa uhimili, utakuangusha chali,
Uwongo una karaha, hukupa wewe utumwa.

Uwongo ni sumu kali, uwongo una muhali,
Tena uuweke mbali, wala si rasilimali,
Siuvalie msuli, ukaupa minajili,
Uwongo una karaha, hukupa wewe utumwa.

6 comments:

 1. De stämmer det är fult att ljuga. Det är inte bra. Bra jobbat tycker om dina dikter.

  ReplyDelete
 2. Khaaaaaaaaa! Da Yasinta mbona "kiNgoni" cha leo hakina vina? Lollll
  Shukrani saana Kaka Fadhy. Najua wanajua kuwa tunajua wanatudanganya. Na kwa kujua huku, wanajitahidi kutujua tujuavyo ili wajue namna ya kutudanganya tena. Lakini watu wanafanywa WATUMWA wa akili na pesa. Wanathamini pesa wanapodanganywa na kuifanya jamii kudhoofika kwa kutojali ukweli na kisha kuchagua uongo badala ya ile iliyo kweli yenye nia ya kutuweka huru.
  Inauma na inakera maana sijui nani mjinga zaidi. Aambiwaye uongo ama yule anayejua kuwa anasema uongo?
  Sote ni watumwa. Nimepata wazo la namna tuchaguavyo na ntaliandikia nikipata nafasi.
  Asante

  ReplyDelete
 3. Hivi kwa mtu ambaye hawezi kudanganya, hali hii wakati mwingine haiwezi kumcost.Kuna mambo ambayo huwa yanalazimu usiri fulani, na ili kuweka siri, uongo ni lazima utumike.
  Hii inakuwaje?

  ReplyDelete
 4. Kuna mtu alisema uwongo ni sehemu ya maisha, bila uwongo mambo hayaendi, na unaweza kujaza hasira hapa duniani.
  Hata huyo aliyeandika kwa lugha ya sweden kachapia ka-uongo!

  ReplyDelete
 5. Hivi si inasemekana asilimia kubwa katika wapenzi kabla penzi halija kubaliwa na mpenzi WATONGOZAJI wengi walichanganya mtongozo na uongo?

  Au hakuna ukweli KUHUSU MAFANIKIO ya UONGO katika KUWAFANIKISHIA WENGI hili SWALA la aisee Dada ule mpango vipi?

  ReplyDelete
 6. Mi nadhani binadamu tumetafuta sababu ili kuhalalisha matumizi ya uwongo. Lakini mara nyingi uwongo unatugharimu. Wakati mwingine hizo zawa gharama za maisha.
  Uwongo niuchukiao kuliko wote ni uwongo wa wapenda majukwaa.
  Na zaidi, ni ule wa watunukiwa mioyo ya wengine.

  ReplyDelete