Wednesday, July 29, 2009

Salamu wanablog I

Nashika kalamu yangu, salamu nazituma,
Kwenu marafiki zangu, natumai mu wazima,
Nawaombea kwa Mungu, mjaliwe yalo mema,
Salamu wanablog.

Simon Kitururu, huzamia MAWAZONI,
Fikra zake ni huru, pia zina burudani,
Nasi tunamshukuru, hachoki tangu zamani,
Salamu wanablog.

Yupo dadetu Yasinta, yeye hupenda MAISHA,
Kamwe hawezi kusita, mazuri kutuonesha,
Sifa tele azipata, maana huelimisha,
Salamu wanablog.

Christian Bwaya yupo, hutaka tuJIELEWE,
Daima aandikapo, vichwa vyetu tusuguwe,
Ukweli daima upo, muhimu ujadiliwe,
Salamu wanablog.

Mubelwa Bandio pia, MZEE WA CHANGAMOTO,
Haishi kutuambia, mambo yalo motomoto,
Muziki hutupatia, yenye midundo mizito,
Salamu wanablog.

Subi dada yetu sote, wa NUKTA SABA SABA,
Ili mengi tuyapate, blog yake yashiba,
Asichoke asisite, ajaze hata kibaba,
Salamu wanablog.

Chib naye ni rafiki, hutumia HADUBINI,
Kazi yake haichoki, popote ulimwenguni,
Magharibi mashariki, hutujuza kulikoni,
Salamu wanablog.

MWANAMALENGA Kissima, hutuonesha MWANGAZA,
Makala zenye hekima, na mambo kuyachunguza,
Kwa ushairi ni vema, tungo zake zapendeza,
Salamu wanablog.

Serina Serina huyo, ana UPANDE MWINGINE,
Yale ayaandikayo, hupendwa nao wengine,
Kwa mawazo si mchoyo, hufanya tushikamane,
Salamu wanablog.

Koero Mkundi pia, hutuambia VUKANI,
Hachoki kutuletea, yatokeayo nchini,
Daima hukumbushia, tutoke usingizini,
Salamu wanablog.

Ndugu yetu Mumyhery, kabobea kwa MAVAZI,
Vitu vyake ni vizuri, hilo mbona lipo wazi,
Yupo kwenye mstari, hachoki kufanya kazi,
Salamu wanablog.

Kamala tunamjua, wa nyegerage KIJIWENI,
Fikra apambanua, ili tutoke kizani,
Sote tukajitambua, tujijue kina nani,
Salamu wanablog.

Masangu wa Nzunzullima, CHAKULA chake KITAMU,
Hatosahau daima, kutupa yote muhimu,
Ujuzi wake kisima, haisaliti elimu,
Salamu wanablog.

Markus Mpangala, KARIBUNI sana NYASA,
Yeye wala hajalala, mengi ameshayaasa,
Kabobea mijadala, ya jamii na siasa,
Salamu wanablog.

Lumadede mshairi, USHAIRI MAMBOLEO,
Mashairiye mazuri, tena yale ya kileo,
Huukuza ushairi, na kuupa mwelekeo,
Salamu wanablog.

Na MWANASOSHOLOJIA, siachi kumsifia,
Elimu kutugawia, na picha kutuwekea,
Mazuri hutuambia, ndani ya hii dunia,
Salamu wanablog.

Nami MWANANCHI MIMI, wa DIWANI YA FADHILI,
Tungo zangu siwanyimi, nawapenda kiukweli,
Tena mara kumi kumi, tena na kwa kila hali,
Salamu wanablog.

Ambao sijawataja, lipo shairi jingine,
Sote tungali pamoja, kwa mema tuombeane,
Tusichoke zetu hoja, hivyo na tushikamane,
Salamu wanablog.

16 comments:

 1. Shairi zuri sana Fadhili. Kipaji cha ushairi unacho na unakitumia vyema. Asante na hongera.

  Hata hivyo nina kaswali kadogo. Una maoni gani kuhusu ushairi usiofuata kanuni za urari wa vina na mizani - wenyewe wakiita ushairi huru, ghuni, masivina n.k.? Unakubali kwamba nao ni ushairi wa Kiswahili? Nitakueleza baadaye kwa nini nauliza swali hili.

  ReplyDelete
 2. Shairi nimelipenda sana!
  Swali la Masangu kwangu ni nyota tupu!!***
  Hongera kaka Fadhy

  ReplyDelete
 3. Kwli kipaji unacho maana umekaa na kufiri na kuweka kila neno sehemu yake. Nimelipenda sana na nimerudia kusoma hata sijui mara nggapi.Hongera Fadhy

  ReplyDelete
 4. Ahsanteni sana kwa kulipenda shairi hili. Nalitowa kama zawadi kwenu. Nawashukuruni kwa kuwa nami siku zote.

  Kaka mkubwa Masangu, naomba kujibu swali lako. Kwa maoni yangu, mashairi ya masivina hayana ladha haswa ya kishairi. Ingawa nayo ni sehemu ya mashairi, mi nadhani yanafanya tungo kutonoga.

  Ingawa kuna wakati nami huandika masivina, kusema ukweli huwa siyafurahii. Mashairi yanayozingatia urari wa vina na mizani yana raha ya lugha. Raha kuyafikiri. Raha kuyaandika. Raha hata unapoyasoma.

  Huo ni mtazamo wangu. Ningependa kufahamu kwa nini umeuliza hivyo.

  Ahsante sana.

  ReplyDelete
 5. Si tu mtungaji lakini pia msomaji wa mashairi mengi (nisamehe kwa kiswahili yangu ya Nairobi)

  ReplyDelete
 6. Fadhy, huu sasa upendeleomtu unatunga mashairi mazuri hivyo kama unakunywa maji tu.Hongera sana.Ingekuwa kipaji hiki unahonga kukipata,labda ningejifanya "fisadi" nami nikipate.

  ReplyDelete
 7. Masal Kheir malenga Fadhy.
  Leo nikiwa uani pale najisomea zangu kijigazeti, mara nimwone Mzee na Changamoto yake wangu wangu hima kunifahamisha kuwa kikaoni humu mambo yamekuwa kimasomaso, ndo hivyo nikajinyanya kutoka kwenye mkeka, kigulu na njia ndo hata nafika hapa nakuta wajumbe wamechukua nafasi zao, nami najisogeza niketi hapa hapa leo sibanduki.
  We bwana Fadhili mwenye heri, pokea zangu za dhati shukrani. Walahi umejaaliwa kipaji toka kwake Manani, yeyote kukiloga hawezi.
  Shukran za dhati zikufikie Fadhy, malenga wetu mjuzi.

  ReplyDelete
 8. Mengi wamesema wezangu lkn nafasi yanu sitaki niipoteza HONGERA SANA KAKA FADHI KWA SHAIRI ZURI KIPAJI NI CHAKO LKN MATUNDA TWALA SOTE MUNGU AKUBARIKI SANA.

  ReplyDelete
 9. Asante Papaa Fadhy a.k.a Mzee wa kutunogesha!

  Sasa niseme nini zaidi Papaa wakati unajua sio mimi peke yangu hapa kijiweni NANOGEWA?

  ReplyDelete
 10. Hongera nakupa Fadhy,kweli tuzo wastahili.
  Nimependa hiyo kazi,hakika unatujali.
  Zawadi ilo na hadhi,dhahabu kitu si mali.


  Shairi limesimama,maujuzi kila kona.
  Mara nyingi nalisoma,na vina vinanikuna.
  Hongera tena nasema,kichwa ulikipasua.

  ReplyDelete
 11. Bwana Fadhili: Nimeuliza kwa sababu hata mimi sasa masivina yameanza kunitatanisha. Ninayapenda sana mashairi ya Kezilahabi katika Kichomi na Karibu Ndani. Nayapenda kwa sababu kutokana na maudhui na falsafa yake iliyokomaa na jinsi Kezilahabi mwenyewe anavyosema anachokisema - basi mtu unajikuta umesahau mambo ya fani. Lakini sasa kuna watu kama Kithaka wa Mberia kutoka Kenya. Ukiona mashairi yake utashangaa - pengine ndiyo ugunduzi na kutaka kuandika Historia. Ukipata muda, hebu tazama mashairi yake ambayo yamejadiliwa katika karatasi hii na uniambie kama unakubali kwamba bado ni mashairi ya Kiswahili. Tazama hii karatasi:

  http://www.ifeas.uni-mainz.de/SwaFo/SF_15_07_Indede.pdf

  ReplyDelete
 12. Kaka Masangu, nashukuru sana kwa ufuatiliaji wako wa mashairi.

  Ntaisoma kwa tuo ili nitoe maoni yangu.

  ReplyDelete
 13. Mimi sikufagilii,sote twaruka kwa mbawa moja, nahesabu mbili moja hima niweke kwenye hoja, vingenevyo takuvua koja uwe kama kioja.

  ReplyDelete
 14. Waalaika salaam, shukran kwa kutukumbuka, kila la heri

  ReplyDelete
 15. Ahsanteni sana wadau wote, nimefurahi sana kwa namna mlivyolipokea shairi hili kwa mikono miwili. Pia nawashukuruni sana kwa kuwa nami daima. Mungu awabariki sana ili muishi maisha ya amani, furaha na mafanikio tele katika yale myafanyayo.
  Nawapendeni nyote.
  Pamoja daima.

  ReplyDelete