Friday, July 17, 2009

Niandike

Kalamu nimeishika, kasheshe ipo kichwani,
Natamani kuandika, sijui kitu lakini,
Kukaa nimeshachoka, n'andike kitu fulani,
Niandike nini?

Mapenzi nimeandika, tangu siku za zamani,
Yale yaliyonifika, na yale ya majirani,
Na kwake nilozimika, nimesema ya moyoni,
Niandike nini?

Watoto wan'oteseka, kutwa nzima mitaani,
Wote wan'ohangaika, sijawaweka pembeni,
Ingawa sijaridhika, bado utata kichwani,
Niandike nini?

Kote ninakozunguka, naona mambo fulani,
Akili inanichoka, nije na mtindo gani,
Ama mada ya hakika, mfurahi mioyoni,
Niandike nini?

Kwenye siasa kwafuka, mbio za majukwaani,
Wakati nd'o unafika, ziwe zao kampeni,
Nalo nikiliandika, nitakosa kosa gani?
Niandike nini?

Sarah atanifunika, Chib alishabaini,
Ni vema kuchakarika, isije fika jioni,
Tungo zisije kauka, hata ziwe milioni,
Niandike nini?

Enyi msomithilika, marafiki wa moyoni,
Tungo msiozichoka, kila siku bulogini,
Semeni kwa'yo hakika, ushauri wa thamani,
Niandike nini?

6 comments:

 1. Ahsante kwa tungo nzuri, nimechekelea kwa kuona na jina langu limo. Ha ha haaa

  ReplyDelete
 2. Ahsante kwa beti hizi andika chochote ukifikiliacho ambacho hujaandika.

  ReplyDelete
 3. Niandike nini ushaandika,
  tungo yenyewe imeshika,
  kila kunapokucha,
  hutokosa cha kuweka,
  tumeshindaje itatosha,
  salamu tutaridhika.

  ReplyDelete
 4. hizi beti zimefika saba si umeandika?

  ReplyDelete
 5. Ahsante kaka Chib, da Yasinta, kaka Kissima na 'mamkwe' Mumyhery.
  Nd'o hivyo wakati nashika kalamu nilitamani kuandika shairi. Kichwani sikuwa na idea yoyote.
  Nilipowaza kuwauliza 'niandike nini' nilinuwia kuandika walau ubeti mmoja ama beti mbili tu.
  Nilipomaliza beti ya pili nikajikuta naendelea. Ulevi mwingine bwana!
  Kwa dhati ya moyo, nakushukuruni sana kwa kutochoka kwenu kuwa sambamba nami.
  Pamoja daima.

  ReplyDelete
 6. kazi nzuri sana. Hongera mno.

  ReplyDelete