Thursday, July 23, 2009

Nakupa salamu

nakupa salamu,
japo wadhani si muhimu,
salamu yangu siyo sumu,
kwamba kesho ujilaumu,
kwanini ukaipokea.

ninakukumbuka daima,
ni kweli ninavyosema,
siwezi hata kupima,
japo moyo unauma,
sana nilikuzowea.

nilikuudhi sana pengine,
na kufanya tusithaminiane,
niseme kipi kingine,
ili tusameheane?
labda utaniambia.

kesho na leo ilianzia jana,
ndo nimefikiri kwa kina,
sote tungali vijana,
tu vitani tunapambana,
maisha kuyapigania.

mi nawe tusijenge chuki,
wala kutishiana mikuki,
uwe wa kweli wetu urafiki,
leo na kesho kwenye hii dunia.

tuyaache yale mengine,
ni rahisi tuelewane,
ilikuwa ni riziki ya mwingine,
kamwe wewe sitokuchukia.

hata kama umenitema,
haifai kujenga uhasama,
ni haki yako kupima vema,
na kumchagua anayekufaa.

mbona mimi sina kinyongo,
kusema ninacho ni uongo,
ama tuseme longolongo,
hayo mie nimeyaridhia.

nakupenda sana sikatai,
lakini kwa mwingine sikuzuii,
kwa sababu kwangu hujisikii,
kukulazimisha ni kukwonea.

pendo,pendo moyo yangu,
ningefarijika wewe kwangu,
uuhifadhi moyo wangu,
mahali salama palipotulia.

nilikuahidi na tena nakuahidi,
sitofanya makusudi,
kukufanyia eti ugaidi,
ama kwako kuwa mkaidi,
ntaonesha nzuri tabia.

sina kinyongo nimeridhika,
japo mbali tumetoka,
si rahisi vikwazo kuvivuka,
mie njiani nimeishia.

moyo wangu una amani,
amani,amani,amani niamini,
kushindwa kwangu mtihani,
makosa sitorudia.

pole nimekuchosha,
kwa e-mail isiyoisha,
maneno mengine nabakisha,
siku nyingine ntayatumia.

siku njema.
wasalaam,
fadhili.


Hiyo ni e-mail niliiandika kwa mtu mmoja mwezi Oktoba 2006, inajieleza vema. Nimependa kuiweka tena kwani kila niisomapo hukumbuka mbali, miaka kadhaa na mwandikiwa e-mail huyo.

6 comments:

 1. Safi sana kaka Fadhy kusema kweli mashairi yako yanaburudisha sana. Ahsante!!

  ReplyDelete
 2. Makofi nimekupigia mieeeee!

  ReplyDelete
 3. Da Yasinta ahsante sana kwa kuburudishwa na mashairi yangu.

  Mtakatifu Simon ahsante sana kwa ubomba wa hili Salamu maalumu kwa alowahi kuwa muhimu.

  Kaka Chib ahsante sana kwa makofi. Nimeyafurahia sana.

  ReplyDelete
 4. Hongera mzee kwa kuwa mkweli kwa nafsi yako

  ReplyDelete
 5. Ahsante sana mkuu Given kwa kunitembelea na kuweka maoni. Najua utakuwa umecheka sana ukizingatia kisa chenyewe unakifahamu.
  Ahsante sana kwa kuwa pamoja nami miaka nenda miaka rudi.

  ReplyDelete