Thursday, July 9, 2009

Kisarawanda

Kilimani niliranda, kungoja pijo kupanda,
Wala sikufanya inda, kukupa sasamlanda,
Kinani kisarawanda, mbona kingali kisafi?

Presha haikupanda, niliamini kushinda,
Sikuchoka kukuwinda, kwako sera kuziunda,
Kinani kisarawanda, mbona kingali kisafi?

Uliniambia u kinda, limbuko umelilinda,
Pasi kuvua kirinda, yakini ukajizinda,
Kinani kisarawanda, mbona kingali kisafi?

Makini wa yako winda, kukataa japo wanda,
Na kwamba wala si chanda, kilogusa lako ganda,
Kinani kisarawanda, mbona kingali kisafi?

Nimekusubiri nyonda, ningali ninakupenda,
Sithubutu kukutenda, kwangu bado hujabunda,
Usijali kisarawanda, kwamba kingali kisafi.

Wala usijipe chonda, bure ukapata donda,
Hili nalo nakufunda, yalopita yamekwenda,
Usijali kisarawanda, kwamba kingali kisafi.

6 comments:

 1. Sina uhakika kingali safi kisarawanda
  ,na naogopa chunguza.

  Mwenzangu nona ushachunguza ndio maana wadai kisafi.

  Hivi hakina hina Kisarawanda ingawa bado wadai kwamba kingali safi?

  DUH!

  ReplyDelete
 2. Leo nimetoka bila kitu. Ila nipo pamoja nawe kakangu!

  ReplyDelete
 3. Pole da Yasinta kwa kutoka patupu. Naomba nilifafanue shairi hili.

  Shairi linamhusu ghulamu, kijana wa kiume, akimweleza bi arusi wake siku ya arusi.

  Kisarawanda-ni nguo ama kitambaa cheupe kinachotandikwa kitandani siku ya mume kupewa mke ili kuthibitisha ubikira wa bi arusi.

  Mshairi anapouliza, kinani kisarawanda, mbona kingali kisafi?
  Anamhoji bi arusi wake kuna nini hata kitambaa hakijachafuka?

  Mshairi aliahidiwa kuwa bibie hajaguswa. Nd'o maana mshairi alingoja sana ili aje afaidi. Aliranda kilimani, akingoja pijo kupanda.

  Mshairi anaposema, "uliniambia u kinda, limbuko umelilinda."
  anasema bibie alisema yu mbichi, uke ameulinda.

  "pasi kuvua kirinda, yakini ukajizinda."
  anasema kwamba bibie hakuvua nguo za ndani akasimama imara.

  Lakini pamoja na kukuta tofauti na alivyoahidiwa, mshairi bado anamhakikishia nyonda (mpenzi) wake angali anampenda na kwamba hatomtenda, kwani kwake mpenzi huyo hajabunda (hajashindwa mtihani)

  Beti la mwisho, mshairi anamwomba mpenziwe asijipe chonda (huzuni) bure akaumia. Anamhakikishia kuwa aloyafanya nyuma yamepita yeye hatoyajali.

  Anaposema, "usijali kisarawanda, kwamba kingali kisafi"
  Mshairi anamhakikishia bi arusi kuwa hana haja ya kupata fedheha ati kwa sababu ile nguo haijachafuka.

  Ndivyo mshairi alivyokusudia kusema. Ni stori tu, nimeshinda leo kamusi, katika kuipitia nikakutana na neno lililonivutia namna lilivyo. Nikatamani kuliandikia shairi. Nashukuru nimejaribu.

  Ahsanteni kwa kuzidi kuwa pamoja nami.

  Ni hayo tu!

  ReplyDelete
 4. Ahsante sana tena sana kwa kufafanua. Kwani sasa nimefaidi shairi maana napenda sana mashairi. Upimaji huu kazi kweli mpaka wanaweka kitambaa cheupe kupima kama kweli u bikira. Haya asante tena Fadhy shairi nzuri.

  ReplyDelete
 5. Kama si kufafanua, basi nami ningetoka kapa.
  Nami nafurahi kwa ufafanuzi.

  ReplyDelete