Wednesday, July 22, 2009

Kila dakika

Kila ninapoamka, na nilalapo usiku,
Moyoni sinayo shaka, moyo nimekutunuku,
Furaha nayoitaka, nisoilipia luku,
Nakupenda sitochoka, tena kwa kila dakika.

Siepuki kukuwaza, na moyo wafurahia,
Ya moyoni nakweleza, furaha wanipatia,
Nitafanya naloweza, usipate kuumia,
Nakupenda sitochoka, tena kwa kila dakika.

Chakula changu rohoni, kinishibishacho sana,
Kwangu u mwenye thamani, kifani chako hakuna,
Furaha ya duniani, mimi nawe kupendana,
Nakupenda sitochoka, tena kwa kila dakika.

Wache wengine waseme, nizidishie mahaba,
Tupendane tuwachome, kwa penzi lenye kushiba,
Hata mate wayateme, donge tu litawakaba,
Nakupenda sitochoka, tena kwa kila dakika.

Nasema sibabaishi, we' nd'o nilokuchagua,
Fitina hazinitishi, hazinipi kuugua,
Yao hatujihusishi, bure wanajisumbua,
Nakupenda sitochoka, tena kwa kila dakika.

Ninakupa moyo wote, furaha ukiridhika,
Raha tele uipate, mapenzi ya uhakika,
Niwapo nawe popote, raha isomithilika,
Nakupenda sitochoka, tena kwa kila dakika.

Wacha niyaseme wazi, yote ya mwangu moyoni,
Bila wewe sijiwezi, kwani u wangu rubani,
Mwinginewe simuwazi, u peke yako moyoni,
Nakupenda sitochoka, tena kwa kila dakika.

6 comments:

 1. Naona hilo shairi leo ni kwa mtu ambaye unampenda kweli. Namuonea wivu...lol. Hongera kwa kumpata mtu umpendaye kiasi hicho natumaini naye anakupenda kama umpendavyo.

  ReplyDelete
 2. Nafikiri naye huyo anayependwa, kakichwa kamevimba!

  ReplyDelete
 3. shairi tamu. Naliprint niwe namsomea mpenzi wangu. Nimesoma mashairi yako kaka unatisha.

  ReplyDelete
 4. Mtakatifu Simon nakushukuru kwa kunikumbuka sana.

  Da Yasinta wala usimwonee wivu ni haki yake.

  Kaka Chib mwache tu avimbe kichwa maana ndo furaha yangu.

  Doreen karibu sana. Ahsante sana kwa kulipenda shairi hili. Print bila wasi.

  ReplyDelete
 5. nikweli jamani nampenda sana naye anipenda

  ReplyDelete