Thursday, July 2, 2009

Ewe wangu muhibu

Siri yangu waijua, wewe usiniadhibu,
Ya moyoni nakwambia, yenye nguvu ya ajabu,
Ndiwe nayekuwazia, mara nyingi kwa hesabu.

Tangu nilipokujua, moyo ulipata ta'bu,
Nikashindwa kukwambia, nakuhitaji muhibu,
Pengine 'ngenishushua, kuwa nakosa adabu.

Wajua yalotokea, mengi hayana hesabu,
Nakubali nd'o dunia, ilojaa uharabu,
Mwenye moja ama mia, makatavu hayahibu.

Kwa mdomo 'mekwambia, nalihitaji tabibu,
Tabibu 'naenijua, 'ngenitibu kwa karibu,
Si tabibu wa bandia, 'taetaka kujaribu.

Nami nimekutakia, kwa pendo na usahibu,
Kwa mengi wanivutia, ukarimuwo dhahabu,
Nami nakufurahia, u nukato mahabubu.

Tunu ninakuletea, siyafanyi majaribu,
Nalotaka nakwambia, ili upate ratibu,
Moyo umeuingia, tuzo yako ni thawabu.

Kwako kweli nina nia, kwa herufi na irabu,
Mema utaniambia, n'uelewe ughaibu,
Baya sitokufanyia, usilolitaka taibu.

Nadhani 'menisikia, kwa rai na taratibu,
Rai 'meniishia, kwa mapenzi nimeghibu,
Kama nimekukosea, naahidi nitatubu.

Ni hayo tu!

3 comments:

 1. Bro Fadhy, nakushauri uanze kuuza tungo zako kwa waimbaji hasa wa taarab!! :-)

  ReplyDelete
 2. Kweli kwako nimefika,
  sijui lini n'tatoka.
  meli mapenzi 'shafika,mimi nanga n'shaweka.
  Siwezi eleza fika,kwanini kwako kufika.
  Hima nitakudanganya,kama taweza eleza.
  penzi ni kuhamasika,ndicho hasa nachofanya.
  daima sitakuchoka,milele sitakwazika.

  ReplyDelete
 3. Ningefurahi kama ningeweza kuandika nimpendaye shairi kama hili. Kazi nzuri sana kaka Fadhy.

  ReplyDelete