Wednesday, July 29, 2009

Salamu wanablog I

Nashika kalamu yangu, salamu nazituma,
Kwenu marafiki zangu, natumai mu wazima,
Nawaombea kwa Mungu, mjaliwe yalo mema,
Salamu wanablog.

Simon Kitururu, huzamia MAWAZONI,
Fikra zake ni huru, pia zina burudani,
Nasi tunamshukuru, hachoki tangu zamani,
Salamu wanablog.

Yupo dadetu Yasinta, yeye hupenda MAISHA,
Kamwe hawezi kusita, mazuri kutuonesha,
Sifa tele azipata, maana huelimisha,
Salamu wanablog.

Christian Bwaya yupo, hutaka tuJIELEWE,
Daima aandikapo, vichwa vyetu tusuguwe,
Ukweli daima upo, muhimu ujadiliwe,
Salamu wanablog.

Mubelwa Bandio pia, MZEE WA CHANGAMOTO,
Haishi kutuambia, mambo yalo motomoto,
Muziki hutupatia, yenye midundo mizito,
Salamu wanablog.

Subi dada yetu sote, wa NUKTA SABA SABA,
Ili mengi tuyapate, blog yake yashiba,
Asichoke asisite, ajaze hata kibaba,
Salamu wanablog.

Chib naye ni rafiki, hutumia HADUBINI,
Kazi yake haichoki, popote ulimwenguni,
Magharibi mashariki, hutujuza kulikoni,
Salamu wanablog.

MWANAMALENGA Kissima, hutuonesha MWANGAZA,
Makala zenye hekima, na mambo kuyachunguza,
Kwa ushairi ni vema, tungo zake zapendeza,
Salamu wanablog.

Serina Serina huyo, ana UPANDE MWINGINE,
Yale ayaandikayo, hupendwa nao wengine,
Kwa mawazo si mchoyo, hufanya tushikamane,
Salamu wanablog.

Koero Mkundi pia, hutuambia VUKANI,
Hachoki kutuletea, yatokeayo nchini,
Daima hukumbushia, tutoke usingizini,
Salamu wanablog.

Ndugu yetu Mumyhery, kabobea kwa MAVAZI,
Vitu vyake ni vizuri, hilo mbona lipo wazi,
Yupo kwenye mstari, hachoki kufanya kazi,
Salamu wanablog.

Kamala tunamjua, wa nyegerage KIJIWENI,
Fikra apambanua, ili tutoke kizani,
Sote tukajitambua, tujijue kina nani,
Salamu wanablog.

Masangu wa Nzunzullima, CHAKULA chake KITAMU,
Hatosahau daima, kutupa yote muhimu,
Ujuzi wake kisima, haisaliti elimu,
Salamu wanablog.

Markus Mpangala, KARIBUNI sana NYASA,
Yeye wala hajalala, mengi ameshayaasa,
Kabobea mijadala, ya jamii na siasa,
Salamu wanablog.

Lumadede mshairi, USHAIRI MAMBOLEO,
Mashairiye mazuri, tena yale ya kileo,
Huukuza ushairi, na kuupa mwelekeo,
Salamu wanablog.

Na MWANASOSHOLOJIA, siachi kumsifia,
Elimu kutugawia, na picha kutuwekea,
Mazuri hutuambia, ndani ya hii dunia,
Salamu wanablog.

Nami MWANANCHI MIMI, wa DIWANI YA FADHILI,
Tungo zangu siwanyimi, nawapenda kiukweli,
Tena mara kumi kumi, tena na kwa kila hali,
Salamu wanablog.

Ambao sijawataja, lipo shairi jingine,
Sote tungali pamoja, kwa mema tuombeane,
Tusichoke zetu hoja, hivyo na tushikamane,
Salamu wanablog.

Sunday, July 26, 2009

Wana kosa gani?

Mola nipe ujasiri, jambo nataka kusema,
Kwa waso na roho nzuri, waliokosa huruma,
Ambao hujidhihiri, kwa huo wao unyama,
Mbona mwatupa watoto, kwani wana kosa gani?

Zenu wenyewe anasa, mwafanya mwafurahia,
Mimba mnapozinasa, kwanini mwazichukia?
Kama mngeumbwa tasa, lawama mngezitoa,
Mbona mwatupa watoto, kwani wana kosa gani?

Wao wana kosa gani, kwanini mnawatupa?
Mnawatupa vyooni, wengine kwenye mapipa,
Kama hamwezi thamini, basi mimba mngekwepa,
Mbona mwatupa watoto, kwani wana kosa gani?

Kwani hamwoni uchungu, ama huruma myoyoni?
Mnamkosea Mungu, mwajiweka nuksani,
Yaacheni malimwengu, zishikeni zenu dini,
Mbona mwatupa watoto, kwani wana kosa gani?

Watoto ni malaika, shukuruni kuwazaa,
Msiwape kuteseka, wala mkawakataa,
Watoto ndiyo baraka, kwanini mwajihadaa?
Mbona mwatupa watoto, kwani wana kosa gani?

Nawanyoshea vidole, tabia hiyo muache,
Nawapigia kelele, watoto msiwakache,
Wewe pamoja na yule, watoto msiwafiche,
Mbona mwatupa watoto, kwani wana kosa gani?

Thursday, July 23, 2009

Nakupa salamu

nakupa salamu,
japo wadhani si muhimu,
salamu yangu siyo sumu,
kwamba kesho ujilaumu,
kwanini ukaipokea.

ninakukumbuka daima,
ni kweli ninavyosema,
siwezi hata kupima,
japo moyo unauma,
sana nilikuzowea.

nilikuudhi sana pengine,
na kufanya tusithaminiane,
niseme kipi kingine,
ili tusameheane?
labda utaniambia.

kesho na leo ilianzia jana,
ndo nimefikiri kwa kina,
sote tungali vijana,
tu vitani tunapambana,
maisha kuyapigania.

mi nawe tusijenge chuki,
wala kutishiana mikuki,
uwe wa kweli wetu urafiki,
leo na kesho kwenye hii dunia.

tuyaache yale mengine,
ni rahisi tuelewane,
ilikuwa ni riziki ya mwingine,
kamwe wewe sitokuchukia.

hata kama umenitema,
haifai kujenga uhasama,
ni haki yako kupima vema,
na kumchagua anayekufaa.

mbona mimi sina kinyongo,
kusema ninacho ni uongo,
ama tuseme longolongo,
hayo mie nimeyaridhia.

nakupenda sana sikatai,
lakini kwa mwingine sikuzuii,
kwa sababu kwangu hujisikii,
kukulazimisha ni kukwonea.

pendo,pendo moyo yangu,
ningefarijika wewe kwangu,
uuhifadhi moyo wangu,
mahali salama palipotulia.

nilikuahidi na tena nakuahidi,
sitofanya makusudi,
kukufanyia eti ugaidi,
ama kwako kuwa mkaidi,
ntaonesha nzuri tabia.

sina kinyongo nimeridhika,
japo mbali tumetoka,
si rahisi vikwazo kuvivuka,
mie njiani nimeishia.

moyo wangu una amani,
amani,amani,amani niamini,
kushindwa kwangu mtihani,
makosa sitorudia.

pole nimekuchosha,
kwa e-mail isiyoisha,
maneno mengine nabakisha,
siku nyingine ntayatumia.

siku njema.
wasalaam,
fadhili.


Hiyo ni e-mail niliiandika kwa mtu mmoja mwezi Oktoba 2006, inajieleza vema. Nimependa kuiweka tena kwani kila niisomapo hukumbuka mbali, miaka kadhaa na mwandikiwa e-mail huyo.

Wednesday, July 22, 2009

Kila dakika

Kila ninapoamka, na nilalapo usiku,
Moyoni sinayo shaka, moyo nimekutunuku,
Furaha nayoitaka, nisoilipia luku,
Nakupenda sitochoka, tena kwa kila dakika.

Siepuki kukuwaza, na moyo wafurahia,
Ya moyoni nakweleza, furaha wanipatia,
Nitafanya naloweza, usipate kuumia,
Nakupenda sitochoka, tena kwa kila dakika.

Chakula changu rohoni, kinishibishacho sana,
Kwangu u mwenye thamani, kifani chako hakuna,
Furaha ya duniani, mimi nawe kupendana,
Nakupenda sitochoka, tena kwa kila dakika.

Wache wengine waseme, nizidishie mahaba,
Tupendane tuwachome, kwa penzi lenye kushiba,
Hata mate wayateme, donge tu litawakaba,
Nakupenda sitochoka, tena kwa kila dakika.

Nasema sibabaishi, we' nd'o nilokuchagua,
Fitina hazinitishi, hazinipi kuugua,
Yao hatujihusishi, bure wanajisumbua,
Nakupenda sitochoka, tena kwa kila dakika.

Ninakupa moyo wote, furaha ukiridhika,
Raha tele uipate, mapenzi ya uhakika,
Niwapo nawe popote, raha isomithilika,
Nakupenda sitochoka, tena kwa kila dakika.

Wacha niyaseme wazi, yote ya mwangu moyoni,
Bila wewe sijiwezi, kwani u wangu rubani,
Mwinginewe simuwazi, u peke yako moyoni,
Nakupenda sitochoka, tena kwa kila dakika.

Friday, July 17, 2009

Niandike

Kalamu nimeishika, kasheshe ipo kichwani,
Natamani kuandika, sijui kitu lakini,
Kukaa nimeshachoka, n'andike kitu fulani,
Niandike nini?

Mapenzi nimeandika, tangu siku za zamani,
Yale yaliyonifika, na yale ya majirani,
Na kwake nilozimika, nimesema ya moyoni,
Niandike nini?

Watoto wan'oteseka, kutwa nzima mitaani,
Wote wan'ohangaika, sijawaweka pembeni,
Ingawa sijaridhika, bado utata kichwani,
Niandike nini?

Kote ninakozunguka, naona mambo fulani,
Akili inanichoka, nije na mtindo gani,
Ama mada ya hakika, mfurahi mioyoni,
Niandike nini?

Kwenye siasa kwafuka, mbio za majukwaani,
Wakati nd'o unafika, ziwe zao kampeni,
Nalo nikiliandika, nitakosa kosa gani?
Niandike nini?

Sarah atanifunika, Chib alishabaini,
Ni vema kuchakarika, isije fika jioni,
Tungo zisije kauka, hata ziwe milioni,
Niandike nini?

Enyi msomithilika, marafiki wa moyoni,
Tungo msiozichoka, kila siku bulogini,
Semeni kwa'yo hakika, ushauri wa thamani,
Niandike nini?

Monday, July 13, 2009

Uwongo

Nafunga vema anjali, niombe ardhilhali,
Sitaki kuwa anzali, kwa kutokuwa mkweli,
Sikia kote mahali, niyasemayo Fadhili,
Uwongo una karaha, hukupa wewe utumwa.

Uulizwapo maswali, mada usiihawili,
Kujitia ujahili, uwongo kuwa injili,
Jifunze toka awali, siwadanganye ayali,
Uwongo una karaha, hukupa wewe utumwa.

Usiende fulifuli, kuilazimisha hali,
Ili watu wakubali, maneno yaso adili,
Uwongo una fidhuli, hali hauibadili,
Uwongo una karaha, hukupa wewe utumwa.

Mwiko japo desimali, uwongo kuufaili,
Usiuvike mtali, ama kuwasha kandili,
Utashindwa uhimili, utakuangusha chali,
Uwongo una karaha, hukupa wewe utumwa.

Uwongo ni sumu kali, uwongo una muhali,
Tena uuweke mbali, wala si rasilimali,
Siuvalie msuli, ukaupa minajili,
Uwongo una karaha, hukupa wewe utumwa.

Friday, July 10, 2009

Ilani

Kitanda usikiache, nje ukakimbilia,
Ukatema zako cheche, kwingine kuzitumia,
Usipandikize miche, holela kujiotea.

Pia usingoje kuche, ili uruke na njia,
Nyumbani usikukache, mbali kukakunogea,
Nje usiwapekeche, wako nani wamwachia?

Hiyo ya nje mikweche, shida itakuletea,
Itasababisha wiche, ukabaki jijutia,
Usijifanye mkoche, huko ukachokonoa.

Maisha ni siku chache, ndani ya hii dunia,
Chakula cha nje kiache, wadudu wameingia,
Ni kheri nisikufiche, kwa maneno kukwambia.

Thursday, July 9, 2009

Kisarawanda

Kilimani niliranda, kungoja pijo kupanda,
Wala sikufanya inda, kukupa sasamlanda,
Kinani kisarawanda, mbona kingali kisafi?

Presha haikupanda, niliamini kushinda,
Sikuchoka kukuwinda, kwako sera kuziunda,
Kinani kisarawanda, mbona kingali kisafi?

Uliniambia u kinda, limbuko umelilinda,
Pasi kuvua kirinda, yakini ukajizinda,
Kinani kisarawanda, mbona kingali kisafi?

Makini wa yako winda, kukataa japo wanda,
Na kwamba wala si chanda, kilogusa lako ganda,
Kinani kisarawanda, mbona kingali kisafi?

Nimekusubiri nyonda, ningali ninakupenda,
Sithubutu kukutenda, kwangu bado hujabunda,
Usijali kisarawanda, kwamba kingali kisafi.

Wala usijipe chonda, bure ukapata donda,
Hili nalo nakufunda, yalopita yamekwenda,
Usijali kisarawanda, kwamba kingali kisafi.

Thursday, July 2, 2009

Kipaji kipya

Vita

Vita inapotokea, wananchi hukimbia,
Wananchi huumia, bila hata ya hatia,
Watoto wanaumia, hata wanawake pia,
Watu wote Afrika, tupinge vita jamani.

Sarah Victor Ngwale.

Leo majira ya jioni nilikwenda Tabata Segerea kuitembelea familia ya mjomba wangu. Nimepigwa na mshangao kumkuta binamu yangu Sarah mwenye umri wa miaka 12 akiandika mashairi. Binamu yangu huyo anasoma darasa la VII shule ya msingi Tabata Segerea. Nikamwomba aniandikie beti moja kuhusu jambo lolote. Wakati huo huo TBC1 wakawa wanaonesha wakimbizi wa Kongo. Akaniambia anaandika kuhusu vita. Nimefurahi sana kupita ninavyoweza kueleza kugundua kuwa nina mrithi. Namwombea kila la kheri katika masomo yake, na katika mitihani yao ijayo ya taifa. Afanikiwe daima.

Ewe wangu muhibu

Siri yangu waijua, wewe usiniadhibu,
Ya moyoni nakwambia, yenye nguvu ya ajabu,
Ndiwe nayekuwazia, mara nyingi kwa hesabu.

Tangu nilipokujua, moyo ulipata ta'bu,
Nikashindwa kukwambia, nakuhitaji muhibu,
Pengine 'ngenishushua, kuwa nakosa adabu.

Wajua yalotokea, mengi hayana hesabu,
Nakubali nd'o dunia, ilojaa uharabu,
Mwenye moja ama mia, makatavu hayahibu.

Kwa mdomo 'mekwambia, nalihitaji tabibu,
Tabibu 'naenijua, 'ngenitibu kwa karibu,
Si tabibu wa bandia, 'taetaka kujaribu.

Nami nimekutakia, kwa pendo na usahibu,
Kwa mengi wanivutia, ukarimuwo dhahabu,
Nami nakufurahia, u nukato mahabubu.

Tunu ninakuletea, siyafanyi majaribu,
Nalotaka nakwambia, ili upate ratibu,
Moyo umeuingia, tuzo yako ni thawabu.

Kwako kweli nina nia, kwa herufi na irabu,
Mema utaniambia, n'uelewe ughaibu,
Baya sitokufanyia, usilolitaka taibu.

Nadhani 'menisikia, kwa rai na taratibu,
Rai 'meniishia, kwa mapenzi nimeghibu,
Kama nimekukosea, naahidi nitatubu.

Ni hayo tu!