Wednesday, June 24, 2009

Nihesabu mimi

Rafiki nimesikia, umeanguka shidani,
Mabaya yametokea, yamekurudisha chini,
Wote wamekukimbia, mfariji humuoni,
Wewe nihesabu mimi.

Wote ulosaidia, walipokuwa shidani,
Kwako walokimbilia, nawe ukawathamini,
Leo wamekuachia, mzigo wako begani,
Wewe nihesabu mimi.

Huna haja ya kulia, usiumie moyoni,
Sana ukafikiria, ukakesha kitandani,
Shida ukiziwazia, na kukosa tumaini,
Wewe nihesabu mimi.

Neno hili nakwambia, latoka mwangu moyoni,
Kamwe sitokukimbia, ningali wako shidani,
Naloweza saidia, kamwe sitoweza hini,
Wewe nihesabu mimi.

Kamwe sitokuachia, hadi udondoke chini,
Mi' nitakushikilia, kama siku za rahani,
Nami nitakuombea, baraka kwake Manani,
Wewe nihesabu mimi.

Leo hapa naishia, wewe uwe na amani,
Siwezi kukukimbia, asilani abadani,
Ahadi nairudia, bado ninakuthamini,
Wewe nihesabu mimi.

2 comments:

 1. Ni safi kuwa na rafiki na rafiki ni bora kuliko mwana sesele. Ukimpata mmoja mwenye kukusikiliza shida zako usimtupe.

  ReplyDelete
 2. Wengine wamekukimbia,
  marafiki wa kudhania,
  mimi nakukimbilia,
  matatizo kukusaidia,
  sitakuachia,
  kamwe kupotea,
  kadiri ninavyoweza,
  niko tayari kukusaidia.

  ReplyDelete