Thursday, June 4, 2009

Kote duniani

Ningezunguka kote nchini,
Humu humu bara ama pwani,
Nirande rande barabarani,
Asubuhi hata na jioni,
Nisingemwona mpinzani,
U pekee kote duniani.

Sikukujua tangu zamani,
Labda enzi za utotoni,
Wala sikuwa nawe shuleni,
Lakini u wangu maishani,
Nasema kweli toka moyoni,
U pekee kote duniani.

Raha ya kweli mwangu moyoni,
Inipayo faraja shidani,
Kila siku huwa na thamani,
Langu la muhimu tumaini,
Nilee nidumu furahani,
U pekee kote duniani.

Niseme nini tena jamani,
Kwani moyo si televisheni,
Ningefungua waone ndani,
Kwa namna nilivyo rahani,
Waone ukweli wa moyoni,
U pekee kote duniani.

7 comments:

 1. Ni vizuri kusema kile ulicho nacho moyoni. Ni furaha kwako. hapa nimejifunza kitu. Asante kwa mafundisho kaka Fadhy

  ReplyDelete
 2. Ahsante dada. Ni vema ungetushirikisha kile ulichojifunza.

  ReplyDelete
 3. Ndio maana huwa tunapitia kwenye blog yako, hatukosi cha kuondoka nacho

  ReplyDelete
 4. Nashukuru sana kwa kuweza kupata cha kuondoka nacho unapozuru kibarazani kwangu. Karibu tena na tena.

  ReplyDelete
 5. Fadhy
  Moyo kweli si televisheni
  Lakini...
  Maneno yeshatufikisha ndani

  ReplyDelete
 6. Ahsante da Serina kumbe maneno yeshakuwa televisheni..

  ReplyDelete
 7. Nakuonea wivu kwa kudakwa na mmoja!
  Na moyo ingekuwa Televisheni tungejionea mengi kama yale ya BABA mwenye nyumba ya kulia kumpenda mke wa jirani yake wa nyumba ya kushoto.:-(

  ReplyDelete