Saturday, June 20, 2009

Dar es Salaam

Nimewasili jana na kushangaa,
Kumbe ni jiji lenye mingi mitaa,
Kila kona yake watu wamejaa,
Bidhaa mbalimbali zimezagaa,
Lakini wengine hulala na njaa,
Bado wapo Dar es Salaam.

Elibariki kaja kutoka Moshi,
Anashona viatu na kubrashi,
Anajitahidi azipate keshi,
Huku akipambana na kashkashi,
Wakati mwingine kwa ukaramshi,
Naye yupo Dar es Salaam.

Fatuma toto hilo la kimwambao,
Naye yumo akiuza zake nguo,
Nguo kalikali hadi mitandio,
Watanashati kwake ni kimbilio,
Kwani huziweka nguo za kileo,
Naye yupo Dar es Salaam.

Mahenge naye yule bwana Mkinga,
Kaja zake jijini toka Iringa,
Kwa biashara ghorofa kalijenga,
Kariakoo na watu wanapanga,
Kwenye maisha kawa hodari winga,
Naye yupo Dar es Salaam.

Matembo kaja toka kwao Songea,
Hadi chuo kikuu kajisomea,
Sasa taifa analitumikia,
Wanafunzi wetu kutufundishia,
Ila ubunge anataka gombea,
Naye yupo Dar es Salaam.

Isihaka kopo lake mkononi,
Katoka Dodoma na kuja mjini,
Kila siku huomba watu njiani,
Huzungukazunguka barabarani,
Aweze lea familia nyumbani,
Naye yupo Dar es Salaam.

Nyabigeso toka mkoa wa Mara,
Kamwoa Havintishi wa Mtwara,
Wanafanya kazi bila masikhara,
Abuu mwanasiasa wa Tabora,
Leo hii anaongoza wizara,
Naye yupo Dar es Salaam.

Kutoka kila kona ya Tanzania,
Mjini Dar wamepakimbilia,
Kijijini hawataki kusikia,
Kwani huduma hazijawafikia,
Ya nini kijijini wakabakia?
Wote wapo Dar es Salaam.

5 comments:

 1. Sielewi kwa nini watu wanapenda Dar es Salaam. Mi sipendi Dar napenda maisha ya kijijini tena Ruhuwiko:-)

  ReplyDelete
 2. Na kijijini wakirudi
  Matatizo ya mjini hawazungumzii kwa juhudi.

  Na chekibobu si kuhizi ni mtoto wamjini karudi .

  Na kimwana mtoto wa kijiji aweza mpaka UKIMWI akapewa kwa kuwa Jemadari karudi.

  Naendelea kuwaza hili swala MKuu....

  ReplyDelete
 3. Da Yasinta, kuna watu wanasema wameshatua mabegi Dar hawatoki tena.

  Kaka, Mtakatifu Simon, hao waliotua mabegi na kusema hawatoki tena hurudi kijijini na zawadi kwa binti unaesema anapewa na jemedari aliyerudi.
  Waza kisha rudi kusema nini hicho.

  Nawashukuruni sana.

  ReplyDelete
 4. Dar! Du! Dar!
  Hivi kweli maisha ya kijijini yakimshinda mtu, mtu huyu huyu ataweza kumudu maisha ya Dar?!???.

  ReplyDelete
 5. Kaka Kissima shukrani kwa ujio wako. Mtu akishindwa shamba hudhani atayaweza ya mjini. Matokeo yake, hayo humshinda zaidi.

  ReplyDelete