Monday, June 29, 2009

Kidole kimoja

Kidole hicho kimoja, hakiwezi vunja chawa,
Hata ukikikongoja, bado hutofanikiwa,
Hata hiyo ngoja ngoja, matumbo huyasumbuwa,
Hicho kidole kimoja.

Chakula cha peke yako, radha haijatimia,
Ukiwa naye mwenzako, hakika 'tafurahia,
Hata kote uendako, nawe utajivunia,
Hicho kidole kimoja.

Huna haja ya kuwaza, na usingizi kukosa,
Yupo wa kukuliwaza, hata kukupa hamasa,
Yeye utamueleza, yale yanayokutesa,
Hicho kidole kimoja.

Upweke unayo sumu, siyo vema kuipata,
Mpe yeye umuhimu, jasho lako atafuta,
Mwache akupe wazimu, ila jiepushe juta,
Hicho kidole kimoja.

Kimoja hicho kidole, mbona kitakusumbua,
Na usiku usilale, na homa ukaugua,
Ukatamani ya wale, kama wewe ungekua,
Hicho kidole kimoja.

Kidole hicho rafiki, peke yake hakiwezi,
Usijipe bure dhiki, mpe yule akuenzi,
Kiona haambiliki, usimpe yako kazi,
Hicho kidole kimoja.

Kimoja ni bora kiwe, kuliko kujiumiza,
Ujitoe bure wewe, yeye akakuchagiza,
Nasema ni bora iwe, kuliko ukateleza,
Hicho kidole kimoja.

Friday, June 26, 2009

Pumzika kwa amani

Mshumaa umezima,
Moyowo ulipogoma,
Mautini ukazama,
Basi uende salama.

Hatutokuona tena,
Tuliokupenda sana,
Tunamwomba Maulana,
Akuweke pale pema.

Tutakumbuka thriller,
Hakukuwa na kulala,
Yapendwa kote mahala,
Basi uende salama.

Nenda Mike salama,
Ni ghafla umezima,
Kwa'o moyo wako mwema,
Ulale mahala pema.

Amina.

Wednesday, June 24, 2009

Nihesabu mimi

Rafiki nimesikia, umeanguka shidani,
Mabaya yametokea, yamekurudisha chini,
Wote wamekukimbia, mfariji humuoni,
Wewe nihesabu mimi.

Wote ulosaidia, walipokuwa shidani,
Kwako walokimbilia, nawe ukawathamini,
Leo wamekuachia, mzigo wako begani,
Wewe nihesabu mimi.

Huna haja ya kulia, usiumie moyoni,
Sana ukafikiria, ukakesha kitandani,
Shida ukiziwazia, na kukosa tumaini,
Wewe nihesabu mimi.

Neno hili nakwambia, latoka mwangu moyoni,
Kamwe sitokukimbia, ningali wako shidani,
Naloweza saidia, kamwe sitoweza hini,
Wewe nihesabu mimi.

Kamwe sitokuachia, hadi udondoke chini,
Mi' nitakushikilia, kama siku za rahani,
Nami nitakuombea, baraka kwake Manani,
Wewe nihesabu mimi.

Leo hapa naishia, wewe uwe na amani,
Siwezi kukukimbia, asilani abadani,
Ahadi nairudia, bado ninakuthamini,
Wewe nihesabu mimi.

Saturday, June 20, 2009

Dar es Salaam

Nimewasili jana na kushangaa,
Kumbe ni jiji lenye mingi mitaa,
Kila kona yake watu wamejaa,
Bidhaa mbalimbali zimezagaa,
Lakini wengine hulala na njaa,
Bado wapo Dar es Salaam.

Elibariki kaja kutoka Moshi,
Anashona viatu na kubrashi,
Anajitahidi azipate keshi,
Huku akipambana na kashkashi,
Wakati mwingine kwa ukaramshi,
Naye yupo Dar es Salaam.

Fatuma toto hilo la kimwambao,
Naye yumo akiuza zake nguo,
Nguo kalikali hadi mitandio,
Watanashati kwake ni kimbilio,
Kwani huziweka nguo za kileo,
Naye yupo Dar es Salaam.

Mahenge naye yule bwana Mkinga,
Kaja zake jijini toka Iringa,
Kwa biashara ghorofa kalijenga,
Kariakoo na watu wanapanga,
Kwenye maisha kawa hodari winga,
Naye yupo Dar es Salaam.

Matembo kaja toka kwao Songea,
Hadi chuo kikuu kajisomea,
Sasa taifa analitumikia,
Wanafunzi wetu kutufundishia,
Ila ubunge anataka gombea,
Naye yupo Dar es Salaam.

Isihaka kopo lake mkononi,
Katoka Dodoma na kuja mjini,
Kila siku huomba watu njiani,
Huzungukazunguka barabarani,
Aweze lea familia nyumbani,
Naye yupo Dar es Salaam.

Nyabigeso toka mkoa wa Mara,
Kamwoa Havintishi wa Mtwara,
Wanafanya kazi bila masikhara,
Abuu mwanasiasa wa Tabora,
Leo hii anaongoza wizara,
Naye yupo Dar es Salaam.

Kutoka kila kona ya Tanzania,
Mjini Dar wamepakimbilia,
Kijijini hawataki kusikia,
Kwani huduma hazijawafikia,
Ya nini kijijini wakabakia?
Wote wapo Dar es Salaam.

Thursday, June 18, 2009

Wasiwasi wa nini?

Wasiwasi wako ni wa nini?
Au ni kwamba hujiamini?
Wewe kuwa na raha moyoni,
Kwani mwingine simtamani....

Nakupenda hunacho kifani,
Nadhiri naiweka moyoni,
Hadi siku nafukiwa chini,
Nitakupa pendo la thamani....

Mwingine wala simbaini,
Watosha vema mwangu rohoni,
Huwa nahisi nipo peponi,
Kila uwapo mwangu pembeni....

Ondoa wasi huo moyoni,
Kuwa na furaha maishani,
Nifae rahani na shidani,
Nijaze ndani mwako moyoni.

Wednesday, June 17, 2009

Ulimi!

Huwaponza watu sana...
Huleta kuchukiana...
Watu wakishagombana...
Huleta kubaguana...
Na watu kusengenyana...
Kiungo kidogo sana...
Familia kulumbana...
Na ndugu kuchukiana...
Na kudharauliana...
Mataifa kupigana...
Hata watu kuuana...
Na wapenzi kuachana...
Marafiki kukosana...
Kushindwa salimiana...
Ulimi.

Thursday, June 4, 2009

Kote duniani

Ningezunguka kote nchini,
Humu humu bara ama pwani,
Nirande rande barabarani,
Asubuhi hata na jioni,
Nisingemwona mpinzani,
U pekee kote duniani.

Sikukujua tangu zamani,
Labda enzi za utotoni,
Wala sikuwa nawe shuleni,
Lakini u wangu maishani,
Nasema kweli toka moyoni,
U pekee kote duniani.

Raha ya kweli mwangu moyoni,
Inipayo faraja shidani,
Kila siku huwa na thamani,
Langu la muhimu tumaini,
Nilee nidumu furahani,
U pekee kote duniani.

Niseme nini tena jamani,
Kwani moyo si televisheni,
Ningefungua waone ndani,
Kwa namna nilivyo rahani,
Waone ukweli wa moyoni,
U pekee kote duniani.