Tuesday, May 12, 2009

Utarudia tena?

Mshale wa saa watembea,
Kumbe wakati wasogea,
Siku nazo zapotea,
Wak'ti muafaka wakaribia,
Kuna jambo utanijibia,
Maana nataka kujua,
Kama makosa utayarudia,
Kama ilivyotokea,
Kura ukawapatia,
Hawa wasio kusaidia,
Wakakuacha ukiumia,
Huku wao wakiyafurahia.

Mwenzio nataka kujua,
Nini weye wakifikiria,
Ujingao sije kukusumbua,
Hadi lini 'tajijutia,
Ilhali weye 'lijitakia,
Mafisadi kuwafagilia,
Kurayo ukawapigia.

Nini kilichokuzuzua,
Kama si kanga walizokupatia,
Ama kofia ukazivaa,
Huku wao zikiwafagilia,
Ukashinda tena na njaa,
Kampeni ukiwapigia.

Hivi ni nani wamngojea,
Usingizini kukuzindua,
Amka upate kujionea.

Tena utarudia?

Nataka kukushangaa,
Ingawa hujaniambia,
Unachokifikiria,
Kama uamuzi hujachukua,
Lipo unalolingojea,
Nalo ni kusota na dunia,
Maana akili Mungu kakujalia,
Ila hujataka kuitumia.

Kazi kwako nakwambia!

2 comments:

 1. Nami nasema nilishangaa sana pia nilipokuwa huko nyumbani watu walikuwa wamesha anza hizo kampeni. Walikuwa wanakwenda sehemu na kuchukua mbolea za kampeni. Kazi kwelikweli

  ReplyDelete
 2. Nne twawapatia,
  kisha waenda kujichumia,
  kivulini wajitafunia,
  kabla tano waturudia,
  sahani watupatia,
  khanga watusambazia,
  bila kufikiria,
  hela zetu ndo twazitumia,
  nne moja,
  fomesheni tunaijua,
  kweli lazima,
  usingizini kuzinduka,
  nne twapoteza,
  maisha kama watumwa,
  moja watudanganyia,
  kumbe nne nyingine wajiandalia.


  Pamoja sana.

  ReplyDelete