Monday, May 25, 2009

Usiniache peke yangu

Rafiki yangu toka zamani,
Tokea enzi za utotoni,
Rafiki yangu toka shuleni,
Ambaye kwangu una thamani,
Rafiki yangu hata kazini,
Usiniache peke yangu.

Rafiki yangu wa maishani,
Nikupaye siri za moyoni,
Usiniache niende chini,
Rafiki wewe mwenye thamani,
Niinue tena ulingoni,
Usiniache peke yangu.

Niombee niwapo shidani,
Wewe ndiye langu tumaini,
Nifanye niwe mwenye amani,
Kwa pamoja tuwe furahani,
Ili niondoke majonzini,
Usiniache peke yangu.

Sin'ombee baya asilani,
Sin'wekee fitina kazini,
Sinitumbukize mi' shimoni,
Bali nipende toka moyoni,
Kwa pendo la kweli maishani,
Usiniache peke yangu.

Sisi sote tumo safarini,
Hatujui mwisho wetu lini,
Kwa hivyo tuwapo duniani,
Sichoke kamwe kunithamini,
Wala 'sithubutu kujihini,
Usiniache peke yangu.

5 comments:

 1. Ni kweli rafiki ni muhimu kuwa nayo.Kwani kila mtu anahitaji kuwa na rafiki. Nadhani rafiki yako mpo pamoja mtafute tu. wala hajakuacha labda kazidiwa na kazi.

  ReplyDelete
 2. Asiniache peke yangu....
  Awe rafiki wa kweli kwangu....
  Yake yeye iwe shida yangu....
  Huyu rafiki wa tangu na tangu....

  Ni hayo tu.!

  ReplyDelete
 3. Mmmh Fafhy! inaonekana huyo rafikiyo alikuwa au ni muhimu kweli kwako na mlipendana sana. Pole sana na nadhani akisoma huu ujumbe atakutafuta tu. Usijali

  ReplyDelete
 4. Ulizaliwa peke yako,
  utakufa peke yako,
  rafikiyo kando yako,
  si mwisho wala si mwanzo!

  ReplyDelete
 5. Serina,
  Nilizaliwa peke yangu toka tumboni....
  Lakini siwezi ishi peke yangu duniani....
  Mbona kila siku ntakuwa majonzini....
  Peke yangu niwe siku nafukiwa chini.....

  ReplyDelete