Monday, May 4, 2009

Kila Siku

Napambana bila kuchoka,
Tena mapema nadamka,
Riziki yangu naisaka,
Hadi jasho kunitoka,
Kila siku.

Wakati mwingine nawaza,
Vipi nitakavyoweza,
Kwenda bila kuteleza,
Ama kula na kusaza,
Kila siku.

Mambo mapya hutokea,
Huyu vile kakufanyia,
Mwingine kukuharibia,
Ikafikia hata ukachukia,
Kila siku.

Mambo mengine yanachosha,
Mengine tamaa kukatisha,
Hata hasira kukupandisha,
Utayawaza kwa kukesha,
Kila siku.

Wale ambao uliwaamini,
Ukashinda pale kituoni,
Kwa kura yao wapo madarakani,
Wanakuingiza we’ mjini,
Kila siku.

Watamani nawe useme kitu,
Tena mbele zao hao watu,
Jeuri yao yakujaza ufyatu,
Wakufanyapo we’ si malikitu,
Kila siku.

9 comments:

 1. Mtanga kamarade wangu
  Umeugusa mtima wangu
  Katika pepesa yangu
  Nimekuona ndugu yangu

  Mashairi burudani yangu
  Nayatunga pia mwenzangu
  Nimefurahi kamarade wangu
  Kukuona ndugu yangu

  Nakuahidi malenga wangu
  Kukutembelea mwenzangu
  Kukuwekea link kwangu
  Niwe nakusoma mwenzangu

  ReplyDelete
 2. Ewe Mwanasosholojia,
  Ahsante kunitembelea,
  Usichoke kukaribia,
  Nami nitakutembelea.

  ReplyDelete
 3. Mpaka raha jinsi mnavyobadilisha hizo beti kwa kweli mnanipa raha sana. hapo mmekutana washairi

  ReplyDelete
 4. Mtanga nami napitia...
  Sifa gani nitakubwagia?
  Maneno wajua kuyatumia,
  Aya kwa aya, nimezimia...
  Na asante kwangu kupitia.

  Serina.

  ReplyDelete
 5. Serina nawe karibia,
  Blog za Tanzania,
  Nami nakufurahia,
  Kwa tungo zako muruwa.

  ReplyDelete
 6. Kila siku mihangaiko,
  yatafutwa mishiko,
  tega sikio upate michapo,
  dili zitambue ziliko.

  Ipo siku 'tapata nafuu,
  utakuwa ngazi ya juu,
  kila siku jitume mkuu,
  mafanikio kesho tuu.

  ReplyDelete
 7. Sasa mimi si mjuzi,
  Wa mashairi si mtunzi,
  Ila kazizo nazienzi,
  Asante kwa hizi tenzi.

  Najaribu kupitia,
  maoni walioachia,
  kila mtu aya kachichia,
  Kwa raha zao wamejiachia.

  Hapa ni mahala pema,
  Kwa ndugu aya kuzitema,
  Tena zenye mambo mema,
  Kuhusu dunia ama letu hema.

  Nimesema siyajui haya,
  Wacha hii iwe mwisho aya,
  Naamini sijaweka baya,
  Mema yote nawaombea.

  ReplyDelete
 8. Mubelwa nawe mshairi,
  Tena mtunzi hodari,
  Naona sana fahari,
  Tenzi tukizitumia.

  Tungo hizi maridhawa,
  Moyoni raha zagawa,
  Maana husisimuwa,
  Na lugha kujivunia.

  ReplyDelete
 9. Hujambo Fadhy?
  Kuna kazi inakusubiri. Pitia kwangu kwa maelezo.
  Serina.

  ReplyDelete